< Zaburi 102 >
1 Sikia maombi yangu, Ee Yahwe; sikia kulia kwangu kwako.
Maombi ya mtu aliyechoka. Anapoteseka na kumimina malalamiko yake kwa Bwana. Ee Bwana, usikie maombi yangu, kilio changu cha kuomba msaada kikufikie.
2 Usiufiche uso wako mbali nami wakati wa shida. Unisikilize. Nikuitapo, unijibu upesi.
Usinifiche uso wako ninapokuwa katika shida. Unitegee sikio lako, ninapoita, unijibu kwa upesi.
3 Kwa maana siku zangu zinapita kama moshi, na mifupa yangu kama moto.
Kwa kuwa siku zangu zinatoweka kama moshi, mifupa yangu inaungua kama kaa la moto.
4 Moyo wangu umeumizwa na niko kama majani yaliyo kauka. Ninasahau kula chakula chochote.
Moyo wangu umefifia na kunyauka kama jani, ninasahau kula chakula changu.
5 Kwa muendelezo wa kuugua kwangu, nimekonda sana.
Kwa sababu ya kusononeka kwangu kwa uchungu, nimebakia ngozi na mifupa.
6 Niko kama mwali wa jangwani; nimekuwa kama bundi magofuni.
Nimekuwa kama bundi wa jangwani, kama bundi kwenye magofu.
7 Ninalala macho kama shomoro faraghani, pekeyake juu ya paa.
Nilalapo sipati usingizi, nimekuwa kama ndege mpweke kwenye paa la nyumba.
8 Adui zangu wananilaumu mchana kutwa; wale wanao nidhihaki hutumia jina langu katika laana.
Mchana kutwa adui zangu hunidhihaki, wale wanaonizunguka hutumia jina langu kama laana.
9 Ninakula majivu kama mkate na kuchanganya kinywaji changu kwa machozi.
Ninakula majivu kama chakula changu na nimechanganya kinywaji changu na machozi
10 Kwa sababu ya hasira yako kali, umeniinua juu kunitupa chini.
kwa sababu ya ghadhabu yako kuu, kwa maana umeniinua na kunitupa kando.
11 Siku zangu ni kama kivuli kanachofifia, na ninanyauka kama majani.
Siku zangu ni kama kivuli cha jioni, ninanyauka kama jani.
12 Lakini wewe, Yahwe, unaishi milele, na kumbukumbu lako ni kwa vizazi vyote.
Lakini wewe, Ee Bwana, umeketi katika kiti chako cha enzi milele, sifa zako za ukuu zaendelea vizazi vyote.
13 Wewe utasimama na kuirehemu Sayuni. Sasa ni wakati wa mkurehemu yeye. Wakati ulio teuliwa umefika.
Utainuka na kuihurumia Sayuni, kwa maana ni wakati wa kumwonyesha wema; wakati uliokubalika umewadia.
14 Maana watumishi wako wameyaridhia mawe yake pendwa na kuyaonea huruma mavumbi ya magofu yake.
Kwa maana mawe yake ni ya thamani kwa watumishi wako, vumbi lake lenyewe hulionea huruma.
15 Mataifa wataliheshimu jina lako, Yahwe, na wafalme wote wa nchi watauheshimu utukufu wako.
Mataifa wataogopa jina la Bwana, wafalme wote wa dunia watauheshimu utukufu wako.
16 Yahwe ataijenga tena Sayuni na ataonekana katika utukufu wake.
Kwa maana Bwana ataijenga tena Sayuni na kutokea katika utukufu wake.
17 Wakati huo, atajibu maombi ya fukara; hatayakataa maombi yao.
Ataitikia maombi ya mtu mkiwa, wala hatadharau hoja yao.
18 Hii itaandikwa kwa ajili ya vizazi vijavyo, na watu ambao bado hawajazaliwa watamsifu Yahwe.
Hili na liandikwe kwa ajili ya kizazi kijacho, ili taifa litakaloumbwa baadaye waweze kumsifu Bwana:
19 Maana ametazama chini toka mahali pa juu patakatifu;
“Bwana alitazama chini kutoka patakatifu pake palipo juu, kutoka mbinguni alitazama dunia,
20 Toka mbinguni Yahwe ameiangalia nchi, ili kusikia kuugua kwa wafungwa, kuwafungua waliohukumiwa kufa.
kusikiliza vilio vya uchungu vya wafungwa na kuwaweka huru wale waliohukumiwa kufa.”
21 Kisha watu watalitangaza jina la Yahwe katika Sayuni na sifa zake katika Yerusalemu
Kwa hiyo jina la Bwana latangazwa huko Sayuni na sifa zake katika Yerusalemu,
22 pindi mataifa na falme watakapokusanyika pamoja kumtumikia Yahwe.
wakati mataifa na falme zitakapokusanyika ili kumwabudu Bwana.
23 Amechukua nguvu zangu katikati ya siku zangu za kuishi, amezifupisha siku zangu.
Katika kuishi kwangu alivunja nguvu zangu, akafupisha siku zangu.
24 Nilisema, “Mungu wangu, usinichukue katikati ya siku zangu; wewe uko hapa hata kizazi chote.
Ndipo niliposema: “Ee Mungu wangu, usinichukue katikati ya siku zangu; miaka yako inaendelea vizazi vyote.
25 Tangu zama za kale wewe uliiweka nchi mahali pake; mbingu ni kazi ya mikono yako.
Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.
26 Mbingu na nchi zitaangamia lakini wewe utabaki; zitachakaa kama mavazi; utaziondoa kama watu waondoavyo mavazi yaliyo chakaa, nazo hazitaonekana tena.
Hizi zitatoweka, lakini wewe utadumu, zote zitachakaa kama vazi. Utazibadilisha kama nguo nazo zitaondoshwa.
27 Lakini wewe ni yuleyule, na miaka yako haitakuwa na mwisho.
Lakini wewe, U yeye yule, nayo miaka yako haikomi kamwe.
28 Watoto wa watumishi wako wataendelea kuishi, na uzao wao utaishi katika uwepo wako.
Watoto wa watumishi wako wataishi mbele zako; wazao wao wataimarishwa mbele zako.”