< Danieli 2 >

1 Katika mwaka wa pili wa utawala wa Nebukadneza, alikuwa na ndoto. Akili yake ilisumbuka, na hakuweza kulala.
Katika mwaka wa pili wa utawala wake, Nebukadneza aliota ndoto. Mawazo yake yakasumbuka na hakuweza kulala.
2 Ndipo mfalme alipowaita waganga na wale wenye kuongea na wafu. Lakini pia aliwaita wachawi na watu wenye hekima. Aliwataka wamwambie juu ya ndoto zake. Basi walikuja na kusimama mbele za mfalme.
Hivyo mfalme akawaita waganga, wasihiri, wachawi na wanajimu ili wamwambie ndoto yake aliyokuwa ameota. Walipoingia ndani na kusimama mbele ya mfalme,
3 Mfalme akawambia, “Nilikuwa na ndoto, na akili yangu ina mashaka nataka kujua ndoto hiyo nini maana yake.”
akawaambia, “Niliota ndoto inayonisumbua, nami nataka nijue maana yake.”
4 Kisha watu wenye hekima wakamwambia mfalme katika Kiaramaiki, “Mfalme, aishi milele! Twambie sisi ndoto, watumishi wako, nasi tutaifunua maana yake.”
Ndipo wanajimu wakamjibu mfalme kwa lugha ya Kiaramu, “Ee mfalme, uishi milele! Waambie watumishi wako hiyo ndoto, nasi tutaifasiri.”
5 Mfalme akawajibu watu wenye hekima, “Jambo hili limeshamalizika. Kama hamtaweza kuiweka wazi ndoto kwangu na kuitafsiri, miili yenu itakatwa vipande vipande na nyumba zenu zitafanywa kuwa vichuguu vya uchafu.
Mfalme akawajibu wanajimu, “Nimeamua hivi kwa uthabiti: Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu ilikuwa ipi na kuifasiri, mtakatwa vipande vipande na nyumba zenu zitafanywa kuwa vifusi.
6 Lakini kama mtaniambia ndoto na maana yake, mtapokea zawadi kutoka kwangu, thawabu, na heshima kubwa. Basi niambie ndoto na maana yake.”
Lakini mkiniambia ndoto yangu na kuielezea, mtapokea kwangu zawadi, tuzo na heshima kubwa. Basi niambieni ndoto yangu na mnifasirie.”
7 Wakamjibu tena na kusema, “Mfalme na atuambie, watumishi wake, ndoto nasi tukwambia maana yake.”
Wakajibu kwa mara nyingine, “Mfalme na awaambie watumishi wake ndoto yake, nasi tutaifasiri.”
8 Mfalme akawajibu, “Ninajua kwa hakika mnahitaji muda zaidi kwasababu mmeona maamuzi yangu ni magumu kuhusu jambo hili.
Ndipo mfalme akajibu, “Nina hakika kuwa mnajaribu kupata muda zaidi, kwa sababu mnatambua kuwa nimeamua hivi kwa uthabiti:
9 Lakini kama hamtaweza kuniambia ndoto, kuna sentensi moja tu kwa ajili yenu. Mmeamua kuandaa uongo na maneno ya kudanganya ambayo mmekubaliana kwa pamoja kuniambia mpaka pale nitakapobadili akili zangu. Basi, niambieni ndoto, na kisha nitajua kuwa mnaweza kuitafsiri kwa ajili yangu.”
Ikiwa hamtaniambia ndoto yangu, ipo adhabu moja tu kwenu. Mmefanya shauri kuniambia habari za kunipotosha na mambo maovu, mkitumaini kwamba hali itabadilika. Hivyo basi, niambieni hiyo ndoto, nami nitajua kuwa mwaweza kunifasiria.”
10 Watu wenye hekima wakamjibu mfalme, “Hakuna mtu katika dunia anayeweza kutimiza matakwa ya mfalme. Hakuna mfalme yoyote mkuu na mwenye nguvu ambaye alishataka jambo kama hilo kutoka kwa wachawi, wala wenye kuongea na wafu, wala mwenye hekima.
Wanajimu wakamjibu mfalme, “Hakuna mtu duniani ambaye anaweza kufanya analotaka mfalme! Vilevile hakuna mfalme hata awe mkuu na mwenye uweza namna gani, aliyeuliza kitu kama hicho kwa mganga au kwa msihiri, wala kwa mnajimu yeyote.
11 Kile anachokitaka mfalme ni kigumu, na hakuna yeyote awezaye kumwambia mfalme isipokuwa miungu, ambayo haishi miongoni mwa watu.”
Anachouliza mfalme ni kigumu mno. Hakuna yeyote awezaye kumfunulia mfalme isipokuwa miungu, nao hawaishi miongoni mwa wanadamu.”
12 Jambo hili lilimfanya mfalme akasirike na kughadhabika sana, na alitoa amri kuwaangamiza wale wote waliojulikana kuwa ni wenye hekima zao katika Babeli.
Jambo hili lilimkasirisha na kumghadhibisha mfalme mno hata kuagiza kuuawa kwa wenye hekima wote wa Babeli.
13 Hivyo, amri ilitoka kwamba wale wote waliojulikana kwa hekima yao ni lazima wauawe. Na kwa sababu ya amri hii, walimtafuta Daniel na rafiki zake ili kwamba wauawe.
Hivyo amri ikatolewa ya kuwaua wenye hekima, nao watu wakatumwa kuwatafuta Danieli na rafiki zake ili wawaue.
14 Ndipo Daniel alipomjibu kwa busara na umakini, Arioki, kamanda wa walinzi wa mfalme, ambaye alikuwa amekuja kuwaua wale wote waliojulikana kuwa na hekima katika Babeli.
Wakati Arioko, mkuu wa askari wa walinzi wa mfalme, alikuwa amekwenda kuwaua watu wenye hekima wa Babeli, Danieli akazungumza naye kwa hekima na busara.
15 Danieli alimwuliza kamanda wa mfalme, “Kwanini amri ya mfalme ni ya haraka hivyo?” Hivyo, Arioki akamwambia Danieli kile kilichotokea.
Akamuuliza huyo afisa wa mfalme, “Kwa nini mfalme ametoa amri kali hivyo?” Ndipo Arioko akamweleza Danieli jambo hilo.
16 Ndipo Danieli aliingia ndani na akaomba ahadi ya muda wa kuonana na mfalme ili kwamba aweze kuwasilisha tafsiri kwa mfalme.
Aliposikia jambo hili, Danieli akamwendea mfalme, akamwomba ampe muda ili aweze kumfasiria ile ndoto.
17 Kisha Danieli aliingia ndani ya nyumba na aliwaelezea Hanania, Mishaeli, na Azaria, kile kilichotokea.
Ndipo Danieli akarudi nyumbani kwake na kuwaeleza rafiki zake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo.
18 Aliwasihi kutafuta rehema kutoka kwa Mungu wa mbinguni kuhusiana na siri hii ili kwamba yeye na wao wasije wakauawa pamoja na watu wengine waliosalia waliojulikana kuwa na hekima katika Babeli.
Aliwasihi waombe rehema kutoka kwa Mungu wa mbinguni kuhusu siri hii, ili yeye na rafiki zake wasije wakauawa pamoja na wenye hekima wengine wa Babeli.
19 Usiku ule siri ilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Kisha Danieli akamtukuza Mungu wa mbinguni
Wakati wa usiku lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni,
20 na kusema, “Litukuzwa jina la Mungu milele na milele; kwa kuwa hekima na nguvu ni zake.
na akasema: “Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; hekima na uweza ni vyake.
21 Anabadili wakati na majira; anaondoa wafalme na kuweka wafalme katika viti vyao vya enzi. Anawapa hekima wenye hekima na ufahamu kwa wenye weledi.
Yeye hubadili nyakati na majira; huwaweka wafalme na kuwaondoa. Huwapa hekima wenye hekima, na maarifa wenye ufahamu.
22 Hufunua vitu vya chini na vilifichika kwa sababu anajua kile kilicho gizani, naye anaishi pamoja na mwanga.
Hufunua siri na mambo yaliyofichika; anajua yale yaliyo gizani, nayo nuru hukaa kwake.
23 Mungu wa baba zetu, ninakushukuru na kukutukuza wewe kwa ajili ya hekima na nguvu uliyonipa. Sasa umeyafanya yawe wazi kwetu yale tuliyokuomba; umetujulisha mambo yamhusuyo mfalme.”
Ninakushukuru na kukuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu: Umenipa hekima na uwezo, umenijulisha kile tulichokuomba, umetujulisha ndoto ya mfalme.”
24 Ndipo Danieli alienda kumwona Arioki ( yule ambaye mfalme alimchagua kuua kila mtu aliyekuwa na hekima katika Babeli). Alimwendea na kumwambia, “Usiwauwe watu wenye hekima katika Babeli. Nipeleke kwa mfalme na nitamwonesha mfalme tafsiri ya ndoto yake.”
Ndipo Danieli akamwendea Arioko, ambaye mfalme alikuwa amemteua kuwaua wenye hekima wa Babeli, akamwambia, “Usiwaue wenye hekima wa Babeli. Nipeleke kwa mfalme, nami nitamfasiria ndoto yake.”
25 Kisha Arioki kwa haraka alimleta Danieli mbele za mfalme na kusema, “Nimempata miongoni wa watu wa mateka wa Yuda mtu ambaye atafunua maana ya ndoto ya mfalme.”
Arioko akampeleka Danieli kwa mfalme mara moja na kumwambia, “Nimempata mtu miongoni mwa watu wa uhamisho kutoka Yuda ambaye anaweza kumwambia mfalme maana ya ndoto yake.”
26 Mfalme akamwambia Danieli (ambaye alikuwa akiitwa Beliteshaza), “Je unaweza kunimbia ndoto niliyoiona na maana yake?”
Mfalme akamuuliza Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza), “Je, unaweza kuniambia nilichoona katika ndoto yangu na kuifasiri?”
27 Danieli alimjibu mfalme na kusema, “Siri ambayo mfalme ameiomba haiwezi kufunuliwa na watu wenye hekima, wala wale wenye kuongea na wafu, wala wachawi, na wala wataalamu wa nyota.
Danieli akajibu, “Hakuna mwenye hekima, msihiri, mganga au mwaguzi anayeweza kumweleza mfalme siri aliyouliza,
28 Isipokuwa kuna Mungu ambaye anaishi mbinguni, ambaye hufunua siri, na amekwisha kukujulisha wewe, mfalme Nebukadneza, kile kitakachotokea katika siku zijazo. Hizi ndizo Ndoto na maono ya akili zako uliyoyaona wakati ulipokuwa umelala kitandani mwako.
lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri. Amemwonyesha Mfalme Nebukadneza kitakachotokea siku zijazo. Ndoto yako na maono yaliyopita mawazoni mwako ulipokuwa umelala kitandani mwako ni haya:
29 Na kwako Wewe, mfalme, mawazo yako kitandani mwako yalikuwa ni juu ya mambo yajayo, na yule afichuaye siri ameifanya ijulikane kwako kuhusu kile kilicho karibu kutokea.
“Ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotokea baadaye, naye mfunuaji wa siri akakuonyesha ni kitu gani kitakachotokea.
30 Na kuhusu mimi, siri hii haikufunuliwa kwangu kwa sababu ya hekima yoyote niliyo nayo zaidi ya mtu yoyote anayeishi. Siri hii imefunliwa kwangu ili kwamba wewe, mfalme, uweze kufahamu maana, na ili kwamba ujuwe mawazo yaliyo ndani mwako.
Kwangu mimi, nimefunuliwa siri hii, si kwa sababu nina hekima kubwa kuliko watu wengine wanaoishi, bali ni ili wewe, ee mfalme, upate kujua tafsiri, na ili uweze kuelewa kile kilichopita mawazoni mwako.
31 Mfalme, uliangalia juu na ukaona sanamu kubwa. Sanamu hii ambayo ilikuwa yenye nguvu na yenye kung'aa, ilisimama mbele yako. Mng'ao wake ulikuwa unatisha.
“Ee mfalme, ulitazama, na mbele yako ilisimama sanamu kubwa, kubwa mno kupita kiasi, sanamu iliyongʼaa na kutisha kwa kuonekana kwake.
32 Kichwa cha sanamu kilikuwa kimetengenezwa kwa dhahabu safi. Matiti yake na mikono ilikuwa ya fedha. Sehemu ya katikati na mapaja yake yalikuwa yametengenezwa kwa shaba,
Kichwa cha ile sanamu kilikuwa kimetengenezwa kwa dhahabu safi, kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha, tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba,
33 na miguu yake ilikuwa imetengenezwa kwa chuma. Miguu yake ilikuwa ilitengenezwa kwa sehemu chuma na sehemu kwa udongo.
miguu yake ilikuwa ya chuma, na nyayo zake zilikuwa chuma nazo sehemu nyingine zilikuwa udongo wa mfinyanzi uliochomwa.
34 Ulitazama juu, na jiwe lilikuwa limechongwa, ingawa si kwa mikono ya wanadamu, na liliipiga sanamu katika miguu yake ya chuma na udongo, na ponda ponda.
Ulipokuwa unaangalia, jiwe lilikatwa, lakini si kwa mikono ya mwanadamu. Lile jiwe liliipiga ile sanamu kwenye nyayo zake za chuma na udongo wa mfinyanzi, na kuivunja.
35 Kisha chuma, udongo, fedha, na dhahabu zilivunjwa katika vipande vipande kwa wakati mmoja na yakawa kama makapi yaliyo katika sakafu za kupuria kipindi cha kiangazi. Upepo huyapeperushia mbali na hakuna alama inayoachwa. Lakini jiwe lililoipiga sanammu likawa mlima mkubwa na kuijaza dunia yote.
Ndipo ile chuma, ule udongo wa mfinyanzi, ile shaba, ile fedha na ile dhahabu vikavunjika vipande vipande kwa wakati mmoja, na vikawa kama makapi katika sakafu ya kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperusha bila kuacha hata alama. Lakini lile jiwe lililoipiga ile sanamu likawa mlima mkubwa mno na kuijaza dunia yote.
36 Hii ndiyo ilikuwa ndotoyako. Na sasa tutamwambia mfalme maana yake.
“Hii ndiyo iliyokuwa ndoto, nasi sasa tutamfasiria mfalme.
37 Wewe, mfalme, ni mfalme wa wafalme kwa wale ambao Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, nguvu, uweza na heshima.
Ee mfalme, wewe ni mfalme wa wafalme. Mungu wa mbinguni amekupa wewe utawala, uweza, nguvu na utukufu.
38 Amevitia mkononi mwako sehemu ambazo binadamu huishi. Amekupa wanyama wa mwituni na ndege wa angani katika mkono wako, na amekufanya wewe utawale juu yao wote. Wewe u kichwa cha dhahabu cha sanamu.
Mikononi mwako amewaweka wanadamu, wanyama wa kondeni, na ndege wa angani. Popote waishipo amekufanya wewe kuwa mtawala juu yao wote. Wewe ndiye kile kichwa cha dhahabu.
39 Baada yako, ufalme mwingine utainuka ambao ni mdogo kwako, na hata ufalme wa tatu wa shaba utatawala juu ya dunia yote.
“Baada yako, ufalme mwingine utainuka, ulio dhaifu kuliko wako. Baadaye utafuata ufalme wa tatu, ule wa shaba, nao utatawala juu ya dunia yote.
40 Kutakuwa na ufalme wa tatu, wenye nguvu kama chuma, kwa kuwa chuma huvunja vipande vipande vitu vingine na kuponda ponda kila kitu. Itaviharibu vitu hivi vyote na kuvisaga.
Hatimaye, kutakuwako na ufalme wa nne, wenye nguvu kama chuma, kwa maana chuma huvunja na kupondaponda kila kitu; kama vile chuma ivunjavyo vitu vipande vipande, ndivyo ufalme huo utakavyopondaponda na kuvunjavunja nyingine zote.
41 Kama vile ulivyoona, miguu na vidole vilikuwa kwa sehemu vimetengenezwa kwa udongo na kwa sehemu vimefanywa kwa chuma, hivyo utakuwa ni ufalme uliogawanyika; baadhi ya nguvu za chuma zitakuwa ndani yake, kama tu ulivyoona kuwa chuma kimechanganyikana na udongo laini.
Kama vile ulivyoona kuwa kwa sehemu nyayo na vidole vilikuwa vya udongo wa mfinyanzi uliochomwa na kwa sehemu nyingine chuma, hivyo huu utakuwa ufalme uliogawanyika; hata hivyo utakuwa na sehemu zenye nguvu za chuma ndani yake, kama vile ulivyoona chuma imechanganywa na udongo wa mfinyanzi.
42 Kama vile vidole vya miguuni vilivyokuwa kwa sehemu vimetengenezwa kwa chuma na kwa sehemu vimetengenezwa kwa udongo, ndivyo ufalme utakuwa kwa sehemu una nguvu na kwa sehemu utakuwa dhaifu.
Kama vile vidole vyake vya miguu vilikuwa kwa sehemu chuma na sehemu udongo wa mfinyanzi, hivyo ufalme huo kwa sehemu utakuwa na nguvu na kwa sehemu udhaifu.
43 Kama ulivyoona chuma kimechanganywa na udongo laini, na hivyo na watu watakuwa wamechanganyikana; hawakaa kwa pamoja, kama vile chuma kisivyoweza kushikamana na udongo
Kama vile ulivyoona chuma kikiwa kimechanganyikana na udongo wa mfinyanzi uliochomwa, ndivyo watu watakavyokuwa mchanganyiko, wala hawatabaki wameungana tena, kama vile chuma kisivyoweza kuchanganyikana na udongo wa mfinyanzi.
44 Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni ataanzisha ufalme ambao hautaweza kuangushwa, wala kushindwa na watu wengine. Utazivunja falme zingine vipande vipande na kuzikomesha zote, nao utadumu milele.
“Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atauweka ufalme ambao kamwe hautaangamizwa, wala hautaachiwa taifa jingine. Utaziponda zile falme zote na kuzikomesha, bali wenyewe utadumu milele.
45 Kama tu ulivyoona, jiwe lilichongwa kutoka katika mlima, lakini si kwa mikono ya wanadamu. Lilivunja vunja chuma, shaba, udongo, fedha, na dhahabu katika vipande vipande. Mungu mkuu amekujulisha wewe, mfalme, kile kitakachotokea baada ya haya. Ndoto ni ya kweli na tafsiri yake ni ya kuaminika.
Hii ndiyo maana ya maono ya jiwe lililochongwa kutoka mlimani, lakini si kwa mikono ya mwanadamu, lile jiwe ambalo lilivunja chuma, shaba, udongo wa mfinyanzi, fedha na dhahabu vipande vipande. “Mungu Mkuu amemwonyesha mfalme kile kitakachotokea wakati ujao. Ndoto hii ni ya kweli na tafsiri yake ni ya kuaminika.”
46 Mfalme Nebukadneza alianguka kifudifudi mbele ya Daniel na alimweshimu; aliamuru kwamba sadaka zitolewe na manukato yatolewe kwake.
Ndipo Mfalme Nebukadneza akaanguka kifudifudi mbele ya Danieli kumpa heshima, akaagiza wamtolee Danieli sadaka na uvumba.
47 Mfalme alimwambia Danieli, “Hakika Mungu wako ni Mungu wa miungu, Bwana wa wafalme, na ambaye hufunua mafumbo, kwa kuwa umekuwa ukiweza kufumbua mafumbo haya.”
Mfalme akamwambia Danieli, “Hakika Mungu wako ni Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, na mfunuaji wa siri zote, kwa maana umeweza kufunua siri hii.”
48 Ndipo mfalme alimfanya Danieli kuwa wa kuheshiwa sana na alimpa zawadi nyingi nzuri. Alimfanya kuwa mtawala juu ya jimbo lote la Babeli. Danieli akawa liwali mkuu juu watu wenye hekima wa Babeli.
Ndipo mfalme akamweka Danieli nafasi ya juu, na kumpa zawadi nyingi tele. Akamfanya kuwa mtawala wa jimbo lote la Babeli, na kumweka kuwa mkuu wa wenye hekima wote.
49 Danieli alipeleka ombi kwa mfalme, na mfalme aliwateua Shadraka, Meshaki na Abedinego kuwa watawala juu ya jimbo la Babeli. Lakini Danieli alisalia katika ikulu ya mfalme.
Zaidi ya hayo, kwa ombi la Danieli, mfalme akawateua Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa wasimamizi wa jimbo la Babeli, huku Danieli akibaki katika ukumbi wa mfalme.

< Danieli 2 >