< Yohana 12 >

1 Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alienda Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye alimfufua kutoka katika wafu.
Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alikwenda Bethania mahali ambako Lazaro aliyekuwa amefufuliwa na Yesu alikuwa anaishi.
2 Basi wakamwandalia chakula cha jioni huko, na Martha akamtumikia, wakati huo Lazaro alikuwa mmoja wapo wa wale walioketi chakulani pamoja na Yesu.
Wakaandaa karamu kwa heshima ya Yesu. Martha akawahudumia wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Yesu.
3 Kisha Mariamu akachukua ratli ya manukato yaliyotengenezwa kwa nardo safi, yenye thamani kubwa, akampaka Yesu miguuni, na kumfuta miguu kwa nywele zake; nyumba yote ilijaa harufu ya manukato.
Kisha Maria akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.
4 Yuda Iskariote, mmoja wa wale wanafunzi wake, ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,
Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wale wanafunzi ambaye ndiye angemsaliti Yesu, akasema,
5 “Kwanini manukato haya yasingeuzwa kwa dinari mia tatu na wakapewa maskini?”
“Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari 300 na fedha hizo wakapewa maskini?”
6 Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini, bali kwa sababu alikuwa mwizi: yeye ndiye aliyeshika mfuko wa fedha na alikuwa anachukua baadhi ya vilivyowekwa humo kwa ajili yake mwenyewe.
Yuda alisema hivi si kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi, kwani ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha akawa anaiba kile kilichowekwa humo.
7 Yesu alisema, “Mwache aweke alicho nacho kwa ajili ya siku ya maziko yangu.
Yesu akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu.
8 Maskini mtakuwa nao siku zote; lakini hamtakuwa nami siku zote.”
Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.”
9 Basi umati mkubwa wa Wayahudi walipata kujua ya kuwa Yesu yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili ya Yesu tu, ila wamwone na Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka katika wafu.
Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Yesu alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Yesu, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua.
10 Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri ili wamue Lazaro;
Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakafanya mpango wa kumuua Lazaro pia,
11 maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walienda zao na wakamwamini Yesu.
kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake Wayahudi wengi walikuwa wanamwendea Yesu na kumwamini.
12 Na siku ya pili yake umati mkubwa walikuja kwenye sikukuu. Waliposikia ya kuwa Yesu anakuja Yerusalemu,
Siku iliyofuata umati mkubwa uliokuwa umekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Yesu angekuja Yerusalemu.
13 walichukua matawi ya miti ya mitende na kutoka nje kwenda kumlaki na wakapiga kelele, “Hosana! Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli.”
Basi wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema, “Hosana!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Amebarikiwa Mfalme wa Israeli!”
14 Yesu alimpata mwana-punda akampanda; kama vile ilivyoandikwa,
Yesu akamkuta mwana-punda akampanda, kama ilivyoandikwa,
15 “Usiogope, binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda.”
“Usiogope, Ewe binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda!”
16 Wanafunzi wake hawakuyaelewa mambo haya hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka ya kuwa mambo haya aliandikiwa yeye na ya kwamba wametenda mambo haya kwake.
Wanafunzi wake Yesu mwanzoni hawakuelewa mambo haya, lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye.
17 Basi lile kundi la watu waliokuwepo pamoja na Yesu wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, wakashuhudia kwa wengine.
Wale waliokuwepo wakati Yesu alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu, waliendelea kushuhudia.
18 Na ilikuwa kwa sababu hii pia kwamba kundi la watu walikwenda kumlaki kwasababu walisikia ya kwamba ameifanya ishara hiyo.
Ni kwa sababu pia walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda muujiza huu ndiyo maana umati wa watu ukaenda kumlaki.
19 Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, “Tazama, sasa hamwezi kufanya lolote; tazama, ulimwengu umekwenda kwake.”
Hivyo Mafarisayo walipoona hayo wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lolote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”
20 Sasa baadhi ya Wayunani walikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakienda kuabudu kwenye sikukuu.
Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wamekwenda kuabudu wakati wa Sikukuu.
21 Hawa walimwendea Filipo, ambaye alitoka Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba wakisema, “Bwana, sisi tunatamani kumwona Yesu.”
Hawa wakamjia Filipo, ambaye alikuwa mwenyeji wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Yesu.”
22 Filipo akaenda akamwambia Andrea; Andrea na Filipo wakaenda na kumwambia Yesu.
Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Yesu.
23 Yesu akawajibu akasema, “Saa imefika kwa ajili ya Mwana wa Adamu kutukuzwa.
Yesu akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa.
24 Amini, amini, nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka katika nchi ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, itazaa matunda mengi.
Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa huzaa mbegu nyingi.
25 Yeye apendaye uhai wake ataupoteza; bali yeye auchukiaye uhai wake katika ulimemngu huu atausalimisha hata uzima wa milele. (aiōnios g166)
Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele. (aiōnios g166)
26 Mtu yeyote akinitumikia mimi, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Mtu yeyote akinitumikia, Baba atamheshimu.
Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.
27 Sasa roho yangu imefadhaika: nami nisemeje? 'Baba, uniokoe katika saa hii'? Lakini ni kwa kusudi hii nimeifikia saa hii.
“Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii.’ Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu.
28 Baba, ulitukuze jina lako.” Kisha sauti ikaja kutoka mbinguni na kusema, “Nimelitukuza nami nitalitukuza tena.”
Baba, litukuze jina lako.” Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.”
29 Basi mkutano uliosimama karibu naye wakasikia, wakasema ya kwamba kumekuwa ngurumo. Wengine walisema, “Malaika amesema naye.”
Ule umati wa watu uliokuwa mahali pale uliisikia nao ukasema, “Hiyo ni sauti ya radi,” wengine wakasema, “Malaika ameongea naye.”
30 Yesu akajibu na kusema, “Sauti hii haikuja kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu.
Yesu akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu.
31 Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo: Sasa mkuu wa ulimwngu huu atatupwa nje.
Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.
32 Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.”
Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.”
33 Aliyanena hayo akionesha ni mauti gani atakayokufa.
Yesu aliyasema haya akionyesha ni kifo gani atakachokufa.
34 Mkutano wakamjibu, “Sisi tumesikia katika sheria ya kwamba Kristo atadumu hata milele. Nawe wasemaje, 'Mwana Adamu lazima ainuliwe juu'? Huyu Mwana wa Mtu ni nani?” (aiōn g165)
Ule umati wa watu ukapiga kelele ukasema, “Tumesikia kutoka Sheria kwamba ‘Kristo adumu milele,’ wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?” (aiōn g165)
35 Basi Yesu akawaambia, “Nuru ingalipo pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru, ili kwamba giza lisije likawaweza. Yeye aendaye gizani hajui aendako.
Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingalipo pamoja nanyi. Enendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakokwenda.
36 Mngali mnayo nuru, iaminini nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Yesu aliyasema haya na kisha akaenda zake akajificha wasimwone.
Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone.
37 Ingawa Yesu alifanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, bado hawakumwamini
Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini.
38 ili litimie neno la nabii Isaya, alilosema: “Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?”
Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu, na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?”
39 Ndio sababu wao hawakuamini, maana Isaya alisema tena,
Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine:
40 “Amewapofusha macho, na ameifanya migumu mioyo yao; wasije wakaona kwa macho yao na wakafahamu kwa mioyo yao, na wakaongoka nami nikawaponya.”
“Amewafanya vipofu, na kuifanya mioyo yao kuwa migumu, ili wasiweze kuona kwa macho yao, wala kuelewa kwa mioyo yao, wasije wakageuka nami nikawaponya.”
41 Isaya alisema maneno hayo kwa kuwa aliuona utukufu wa Yesu na akanena habari zake.
Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Yesu na kunena habari zake.
42 Walakini, hata wakuu wengi walimwamini Yesu; lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakukiri ili wasije wakatengwa na sinagogi.
Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi.
43 Walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu.
Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zitokazo kwa Mungu.
44 Yesu akapaza sauti na kusema, “Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi tu bali na yeye aliyenituma mimi,
Yesu akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali yeye aliyenituma.
45 naye anionaye mimi anamuona yeye aliyenituma.
Yeyote anionaye mimi, amemwona yeye aliyenituma.
46 Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.
Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kwamba kila mtu aniaminiye asibaki gizani.
47 Ikiwa mtu yeyote atayasikia maneno yangu lakini asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, bali niuokoe ulimwengu.
“Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa.
48 Yeye anikataye mimi na asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye: neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.
Yuko amhukumuye yeye anikataaye mimi na kutokuyapokea maneno yangu, yaani, yale maneno niliyosema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho.
49 Maana mimi sikunena kwa nafsi yangu tu. Bali ni Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema.
Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema.
50 Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi - kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo kwao.” (aiōnios g166)
Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.” (aiōnios g166)

< Yohana 12 >