< Yohana 11 >

1 Basi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Alitokea Bethania, kijiji cha Mariamu na dada yake Martha.
Basi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania kijiji cha Maria na Martha dada zake.
2 Alikuwa ni Mariamu yule yule aliyempaka Bwana Marhamu na kumfuta miguu yake kwa nywele zake, ambaye ndugu yake Lazaro alikuwa ni mgonjwa.
Huyu Maria, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye yule ambaye alimpaka Bwana mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake.
3 Ndipo dada hawa walituma ujumbe kwa Yesu na kusema, “Bwana, angalia yule umpendaye anaumwa.”
Hivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Yesu kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.”
4 Yesu aliposikia alisema, “Ugonjwa huu si wa mauti, lakini, badala yake ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu ili kwamba Mwana wa Mungu apate kutukuzwa katika huo Ugonjwa.”
Lakini Yesu aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti bali umetokea ili kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.”
5 Yesu alimpenda Martha na dada yake na Lazaro.
Pamoja na hivyo, ingawa Yesu aliwapenda Martha, Maria na Lazaro ndugu yao,
6 Aliposikia kuwa Lazaro ni mgonjwa, Yesu alikaa siku mbili zaidi mahali alipokuwa.
baada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, aliendelea kukawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi.
7 Ndipo baada ya hili aliwaambia wanafunzi wake, “Twendeni Uyahudi tena.”
Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Uyahudi.”
8 Wanafunzi wakamwambia, “Rabi, Wayahudi walikuwa wakijaribu kukuponda mawe, na wewe unataka kurudi huko tena?”
Wanafunzi wake wakamwambia, “Rabi, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?”
9 Yesu akawajibu, “Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu anapotembea mchana hawezi kujikwaa, kwa sababu anaona kwa nuru ya mchana.
Yesu akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wala watembeao mchana hawawezi kujikwaa kwa maana wanaona nuru ya ulimwengu huu.
10 Hata hivyo, ikiwa atatembea usiku, atajikwaa kwa sababu nuru haiko ndani yake.”
Lakini wale watembeao usiku hujikwaa kwa sababu hakuna nuru ndani yao.”
11 Yesu akasema mambo haya, na baada ya mambo haya, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini ninakwenda ili kwamba nipate kumuamsha kutoka usingizini.”
Baada ya kusema haya, Yesu akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.”
12 Ndipo wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala, ataamka.
Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.”
13 Wakati huu Yesu alikuwa akizungumza habari za kifo cha Lazaro, lakini wao walidhani anazungumza juu ya kulala usingizi.
Hata hivyo, Yesu alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu.
14 Ndipo Yesu akazungumza nao wazi wazi, “Lazaro amekufa.
Kwa hiyo Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa.
15 Nina furaha kwa ajili yenu, kwamba sikuwepo kule ili kwamba mpate kuamini. Twendeni kwake.”
Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwepo huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.”
16 Basi Tomaso, aliyeitwa Pacha, aliwaambia wanafunzi wenzake, “Nasi twendeni pia tukafe pamoja na Yesu.”
Tomaso aliyeitwa Pacha akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.”
17 Wakati Yesu alipokuja, alikuta kwamba Lazaro tayari amekwishakuwa kaburini siku nne.
Yesu alipowasili huko alikuta Lazaro amekuwa kaburini siku nne.
18 Nayo Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu kama kilomita arobaini na tano hivi.
Basi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu umbali wa karibu maili mbili,
19 Wengi kati ya Wayahudi wakaja kwa Martha na Mariamu kuwafariji kwa ajili ya ndugu yao.
na Wayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Maria kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao.
20 Ndipo Martha aliposikia kuwa Yesu anakuja, alienda kukutana naye, lakini Mariamu aliendelea kukaa nyumbani.
Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Maria alibaki nyumbani.
21 Ndipo Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungelikuwa hapa, kaka yangu asingelikufa.
Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.
22 Hata sasa, najua ya kuwa lolote utakaloomba kutoka kwa Mungu, atakupatia.”
Lakini sasa ninajua kuwa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.”
23 Yesu akamwambia, kaka yako atafufuka tena.”
Yesu akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”
24 Martha akamwambia, najua kwamba atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.”
Martha akamjibu, “Ninajua ya kuwa atafufuka wakati wa ufufuo wa wafu siku ya mwisho.”
25 Yesu akamwambia, “Mimi ni ufufuo na uzima; yeye aniaminiye, ingawa atakufa, hata hivyo atakuwa anaishi;
Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi
26 na yeye aishiye na kuniamini mimi hatakufa. Unaamini hili?” (aiōn g165)
na yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?” (aiōn g165)
27 Akamwambia, “Ndiyo, Bwana naamini kwamba wewe ni Kristo, Mwana wa Mungu, yeye ajaye katika ulimwengu.”
Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”
28 Alipokwisha kusema hili, alienda zake na kumwita dada yake Mariamu faraghani. Akasema, “Mwalimu yuko hapa na anakuita.”
Baada ya kusema haya Martha alikwenda, akamwita Maria dada yake faraghani na kumwambia, “Mwalimu yuko hapa anakuita.”
29 Mariamu aliposikia haya, aliinuka kwa haraka na kwenda kwa Yesu.
Maria aliposikia hivyo, akaondoka upesi akaenda mpaka alipokuwa Yesu.
30 Naye Yesu alikuwa hajaja bado ndani ya kijiji, bali alikuwa bado mahali alipokutana na Martha.
Yesu alikuwa hajaingia kijijini, bali alikuwa bado yuko mahali pale alipokutana na Martha.
31 Ndipo Wayahudi waliokuwa na Mariamu katika nyumba na wale waliokuwa wakimfariji, walipomuona akiinuka haraka na kutoka nje, walimfuata; walidhani kuwa anaenda kaburini ili akalie huko.
Wale Wayahudi waliokuwa pamoja na Maria nyumbani wakimfariji walipoona ameondoka haraka na kutoka nje, walimfuata wakidhani ya kwamba alikuwa anakwenda kule kaburini kulilia huko.
32 Ndipo Mariamu, alipofika pale Yesu alipokuwa alimuona na, alianguka chini ya miguu yake na kumwambia, “Bwana, kama ungelikuwa hapa, ndugu yangu asingelikufa.”
Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa, alipiga magoti miguuni Pake na kusema, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.”
33 Yesu alipomuona analia, na Wayahudi waliokuja pamoja naye walikuwa wakilia pia, aliomboleza katika roho na kufadhaika;
Yesu alipomwona Maria akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Yesu alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana.
34 akasema, “Mmemlaza wapi? wakamwambia, Bwana, njoo utazame.”
Akauliza, “Mmemweka wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”
35 Yesu akalia.
Yesu akalia machozi.
36 Ndipo Wayahudi wakasema, “Angalia alivyompenda Lazaro!”
Ndipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!”
37 Lakini wengine kati yao wakasema, “Siyo huyu, mtu aliyeyafumbua macho ya yule aliyekuwa kipofu, hakuweza kumfanya huyu mtu asife?”
Lakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”
38 Ndipo Yesu, hali akiomboleza nafsini mwake tena, alienda kwenye kaburi. Sasa lilikuwa pango, na jiwe limewekwa juu yake.
Yesu kwa mara nyingine akiwa amefadhaika sana, akafika penye kaburi. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe lilikuwa limewekwa kwenye ingilio lake.
39 Yesu akasema, “Liondoweni jiwe.” Martha, dada yake na Lazaro, yeye aliyekufa, akamwambia Yesu, “Bwana, kwa muda huu, mwili utakuwa umeoza, kwa sababu amekwishakuwa maiti kwa siku nne.”
Yesu akasema, “Liondoeni hilo jiwe.” Martha ndugu yake yule aliyekuwa amekufa akasema, “Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwa kaburini siku nne.”
40 Yesu akamwambia, “Mimi sikukuwaambia ya kwamba, kama ukiamini, utauona utukufu wa Mungu?”
Yesu akamwambia, “Sikukuambia kwamba kama ukiamini utauona utukufu wa Mungu?”
41 Kwa hiyo wakaliondoa jiwe. Yesu akainua macho yake juu na kusema, “Baba, nakushukuru kwa kuwa unanisikiliza.
Kwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Yesu akainua macho yake juu akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia.
42 Nilijua kwamba unanisikia mara zote, lakini ni kwa sababu ya kusanyiko ambalo limesimama kunizunguka kwamba nimesema haya, ili kwamba wapate kuamini kuwa wewe umenituma.”
Ninajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.”
43 Baada ya kusema haya, alilia kwa sauti kubwa, “Lazaro, toka nje!”
Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti yake akaita, “Lazaro, njoo huku!”
44 Mfu alitoka nje amefungwa mikono na miguu kwa sanda za kuzikia, na uso wake ulifungwa na kitambaa.” Yesu akawaambia, “Mfungueni mkamwache aende.”
Yule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake. Yesu akawaambia, “Mfungueni, mwacheni aende zake.”
45 Ndipo Wayahudi wengi waliokuja kwa Mariamu na kuona Yesu alichofanya, walimwamini;
Hivyo Wayahudi wengi waliokuwa wamekuja kumfariji Maria, walipoona yale Yesu aliyoyatenda wakamwamini.
46 lakini baadhi yao walienda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo aliyoyafanya Yesu.
Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo Yesu aliyoyafanya.
47 Ndipo wakuu wa Makuhani na Mafarisayo wakakusanyika pamoja katika baraza na kusema, “Tutafanya nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi.
Kwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa baraza. Wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi.
48 Ikiwa tutamwacha hivi peke yake, wote watamwamini; Warumi watakuja na kuchukua vyote mahali petu na taifa letu.”
Kama tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.”
49 Hata hivyo, mtu mmoja kati yao, Kayafa, aliyekuwa kuhani Mkuu mwaka huo, akawaambia, “Hamjui chochote kabisa.
Mmoja wao aliyeitwa Kayafa, ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, akasema, “Ninyi hamjui kitu chochote!
50 Hamfikirii kwamba yafaa kwa ajili yenu kwamba mtu mmoja yapasa kufa kwa ajili ya watu kuliko taifa lote kuangamia.”
Hamjui kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa lote liangamie?”
51 Haya hakuyasema kwa sababu yake mwenyewe, badala yake, kwa kuwa alikuwa kuhani mkuu mwaka ule, alitabiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa;
Hakusema haya kutokana na mawazo yake mwenyewe bali kama kuhani mkuu mwaka huo, alitabiri kuwa Yesu angelikufa kwa ajili ya taifa la Wayahudi,
52 na si kwa taifa peke yake, bali Yesu apate vile vile kuwakusanya watoto wa Mungu ambao wametawanyika sehemu mbali mbali.
wala si kwa ajili ya taifa hilo pekee, bali pia kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika, ili kuwaleta pamoja na kuwafanya wawe wamoja.
53 Kwa hiyo kuanzia siku hiyo na kuendelea wakapanga namna ya kumwua Yesu.
Hivyo tangu siku hiyo wakawa wanafanya mipango ili wamuue Yesu.
54 Yesu hakutembea tena wazi wazi kati ya Wayahudi, bali aliondoka hapo na kwenda nchi iliyo karibu na jangwa katika mji uitwao Efraimu. Hapo alikaa na wanafunzi.
Kwa hiyo Yesu akawa hatembei hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali alijitenga akaenda sehemu iliyo karibu na jangwa kwenye kijiji kiitwacho Efraimu. Akakaa huko na wanafunzi wake.
55 Basi Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu, na wengi wakapanda kwenda Yerusalemu nje ya mji kabla ya Pasaka ili wapate kujitakasa wenyewe.
Basi Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walitoka vijijini wakaenda Yerusalemu kabla ya Pasaka ili wakajitakase.
56 Walikuwa wakimtafuta Yesu, na kuzungumza kila mmoja walipokuwa wamesimama hekaluni, “Mnafikiri nini? Kwamba hatakuja katika sikukuu?”
Watu wakawa wanamtafuta Yesu, nao waliposimama kwenye eneo la Hekalu waliulizana, Je, mtu huyu hatakuja kamwe kwenye Sikukuu?
57 Wakati huu wakuu wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba ikiwa mmoja atajua Yesu alipo, anapaswa kutoa taarifa ili kwamba wapate kumkamata.
Viongozi wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kuwa yeyote atakayejua mahali Yesu aliko, lazima atoe taarifa ili wapate kumkamata.

< Yohana 11 >