< Kutoka 38 >

1 Naye akafanya madhabahu ya toleo la kuteketezwa kwa mbao za mshita. Mikono mitano urefu wake, na mikono mitano upana wake, ilikuwa mraba, na mikono mitatu kimo chake.
Akatengeneza madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa mbao za mti wa mshita, kimo chake dhiraa tatu; nayo ilikuwa mraba, urefu wake dhiraa tano, na upana wa dhiraa tano
2 Halafu akafanya pembe zake kwenye zile ncha zake nne. Pembe zake zilitoka kwake. Kisha akaifunika kwa shaba.
Akatengeneza upembe kwenye kila pembe ya hizo pembe nne, ili zile pembe na madhabahu zikawa zimeungana, akafunika madhabahu kwa shaba.
3 Baada ya hilo akavifanya vyombo vyote vya madhabahu, yale makopo na zile sepetu na yale mabakuli, zile nyuma na vile vyetezo. Vyombo vyake vyote alivifanya kwa shaba.
Akatengeneza vyombo vyake vyote kwa shaba: vyungu vyake vya kuondolea majivu, masepetu, mabakuli ya kunyunyizia, uma za nyama na vyombo vya kuchukulia moto.
4 Tena akaifanyia madhabahu kiunzi cha fito, mtandao wa shaba, chini ya ukingo wake, chini kuelekea katikati yake.
Akatengeneza wavu wa shaba chini ya ukingo wa madhabahu ili ufikie nusu ya kimo cha madhabahu.
5 Halafu akatengeneza pete nne kwenye ile miisho minne karibu na kile kiunzi cha shaba, ili kuitegemeza ile miti.
Akasubu pete za shaba za kushikilia ile mipiko kwa ajili ya zile pembe nne za huo wavu wa shaba.
6 Bezaleli akafanya miti ya mshita na kuifunika kwa shaba.
Akatengeneza mipiko ya mti wa mshita na kuifunika kwa shaba.
7 Kisha akaitia ile miti kwenye zile pete zilizo pande za madhabahu ili kuibeba. Akaifanya kuwa sanduku la mbao lenye uwazi.
Akaiingiza ile mipiko kwenye zile pete, ili iwe pande mbili za madhabahu kwa ajili ya kuibeba. Akaitengeneza madhabahu yenye uvungu ndani yake akitumia mbao.
8 Kisha akafanya beseni ya shaba na kinara chake cha shaba. Kwa kutumia vioo vya watumishi wanawake ambao walifanya utumishi uliopangwa kwenye mwingilio wa hema la mkutano.
Akatengeneza sinia la shaba lenye kitako cha shaba kutoka kwa vioo vya shaba vilivyotolewa na wanawake waliohudumu pale ingilio la Hema la Kukutania.
9 Naye akafanya ule ua. Upande unaokabili Negebu, kuelekea kusini, mapazia ya ua yalikuwa ya kitani bora kilichosokotwa, kwa mikono mia moja.
Kisha akatengeneza ua. Upande wa kusini ulikuwa na urefu wa dhiraa mia moja, na ulikuwa na mapazia ya kitani iliyosokotwa vizuri,
10 Nguzo zake ishirini na vikalio vyake ishirini vilikuwa vya shaba. Misumari ya nguzo na viungo vyake vilikuwa vya fedha
pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
11 Pia, kwa ajili ya upande wa kaskazini kulikuwa na mikono mia. Nguzo zake ishirini na vikalio vyake ishirini vilikuwa vya shaba. Misumari ya nguzo na viungo vyake vilikuwa vya fedha.
Upande wa kaskazini ulikuwa na urefu wa dhiraa mia moja, pamoja na nguzo ishirini na vitako vya shaba ishirini, pamoja na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
12 Lakini kwa ajili ya upande wa magharibi mapazia yalikuwa mikono hamsini. Nguzo zake zilikuwa kumi na vikalio vyake kumi. Misumari ya nguzo na viungo vyake vilikuwa vya fedha.
Upande wa mwisho wa magharibi ulikuwa na upana wa dhiraa hamsini na ulikuwa na mapazia, na nguzo kumi na vitako vyake kumi, pamoja na kulabu na tepe za fedha juu ya hizo nguzo.
13 Na kwa ajili ya upande wa mashariki kulikuwa na mikono hamsini.
Upande wa mwisho wa mashariki jua linakochomoza, pia ulikuwa na upana wa dhiraa hamsini.
14 Mapazia yalikuwa mikono kumi na mitano kwa upande mmoja. Nguzo zake zilikuwa tatu na vikalio vyake vitatu.
Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yalikuwa upande mmoja wa ingilio, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.
15 Na kwa ajili ya upande ule mwingine, huu na ule, wa lango la ua, mapazia yalikuwa mikono kumi na mitano. Nguzo zake zilikuwa tatu na vikalio vyake vitatu.
Mapazia yenye urefu wa dhiraa kumi na tano yalikuwa upande mwingine wa ingilio la ua, pamoja na nguzo tatu na vitako vitatu.
16 Mapazia yote ya ua kuzunguka pande zote yalikuwa ya kitani bora kilichosokotwa.
Mapazia yote yaliyozunguka ua yalikuwa ya kitani iliyosokotwa vizuri.
17 Navyo vikalio vya nguzo vilikuwa vya shaba. Vibanio vya vikalio na viungo vyake vilikuwa vya fedha navyo vilifunikwa kwa shaba sehemu ya juu, na kulikuwa na viungo vya shaba kwa ajili ya nguzo zote za ua.
Vitako vya nguzo vilikuwa vya shaba. Kulabu na tepe juu ya nguzo zilikuwa za fedha, na ncha zake zilifunikwa kwa fedha. Kwa hiyo nguzo zote za ua zilikuwa na tepe za fedha.
18 Nacho kisitiri cha lango la ua kilikuwa na mikono ishirini urefu. Cha uzi wa bluu na sufu iliyotiwa rangi ya zambarau na kitambaa chenye rangi nyekundu ya kochinili na kitani bora kilichosokotwa, na urefu wake ulikuwa mikono ishirini, nacho kimo kotekote kilikuwa mikono mitano sawasawa na mapazia ya ua.
Pazia la ingilio la ua lilikuwa la nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani iliyosokotwa vizuri, kazi ya mtarizi. Pazia hilo lilikuwa na urefu wa dhiraa ishirini kama zile za kwenye ua, na kimo chake kilikuwa dhiraa tano,
19 Na nguzo zake nne na vikalio vyake vinne vilikuwa vya shaba. Misumari yake ilikuwa ya fedha na utando wa vichwa vyake na viungo vyake ulikuwa wa fedha.
likiwa na nguzo nne na vitako vinne vya shaba. Kulabu zake na tepe zake zilikuwa za fedha, na ncha zake zilikuwa zimefunikwa kwa fedha.
20 Na misumari yote ya hema kwa ajili ya maskani na kwa ajili ya ua kuzunguka pande zote ilikuwa ya shaba
Vigingi vyote vya maskani na vya ua ulioizunguka vilikuwa vya shaba.
21 Hivi ndivyo vitu vilivyohesabiwa vya maskani, maskani ya Ushuhuda, vilivyohesabiwa kwa amri ya Musa, kuwa utumishi wa Walawi chini ya uongozi wa Ithamari mwana wa Aruni kuhani.
Ifuatayo ni orodha ya vifaa vilivyotumika kwa ajili ya ujenzi wa maskani, maskani ya Ushuhuda, ambavyo vilitayarishwa na Walawi kama alivyoagiza Mose, chini ya usimamizi wa Ithamari, mwana wa kuhani Aroni.
22 Naye Bezaleli mwana wa Uri mwana wa Huru wa kabila la Yuda alifanya yote ambayo Yahweh alikuwa amemwamuru Musa.
(Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, alifanya kila kitu Bwana alichomwamuru Mose,
23 Na pamoja naye alikuwa Oholiabu mwana wa Ahisamaki wa kabila la Dani, fundi na mtarizi na mfumaji wa uzi wa bluu na sufu iliyotiwa rangi ya zambarau na kitambaa chenye rangi nyekundu ya kochinili na kitani bora.
akiwa pamoja na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, fundi stadi wa kutia nakshi, kubuni michoro, mtarizi kwa rangi ya buluu, ya zambarau, nyekundu na kitani safi.)
24 Dhahabu yote iliyotumiwa kwa ajili ya kazi katika kazi yote ya mahali patakatifu ikawa jumla ya dhahabu ya toleo la kutikisa, talanta ishirini na tisa na shekeli 730 kulingana na shekeli ya mahali patakatifu.
Jumla ya dhahabu iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa kwa ajili ya kazi ya mahali patakatifu ilikuwa na uzito wa talanta 29 na shekeli 730, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu.
25 Nayo fedha ya wale walioandikishwa kati ya kusanyiko ilikuwa talanta mia moja na shekeli 1, 775 kulingana na shekeli ya mahali patakatifu,
Fedha iliyopatikana kutokana na jumuiya ya watu waliohesabiwa ilikuwa yenye uzito wa talanta mia moja na shekeli 1,775, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu.
26 ile nusu shekeli kwa ajili ya mtu mmoja ilikuwa nusu shekeli kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, Kwa kila mtu aliyekuwa akipita kuingia upande wa wale waliokuwa wameandikishwa kuanzia miaka ishirini na zaidi, jumla ya watu 603, 550.
Kila mtu alitoa beka moja, ambayo ni sawa na nusu shekeli ya fedha, kwa kazi ya mahali patakatifu, kutoka kwa kila mtu aliyekuwa amehesabiwa mwenye umri wa miaka ishirini au zaidi, ambao jumla yao walikuwa wanaume 603,550.
27 Na talanta mia moja za fedha zilitumiwa kutengeneza vikalio vya mahali patakatifu na vikalio vya lile pazia. Vikalio mia moja vilitoshana na talanta mia moja, talanta moja kwa kikalio kimoja.
Talanta hizo 100 za fedha zilitumika kusubu vile vitako mia moja kwa ajili ya mahali patakatifu na pazia: vitako mia moja kwa talanta mia, yaani, talanta moja kwa kila kitako.
28 Na kutokana na zile shekeli 1, 775 alifanyiza vibanio vya nguzo na kuvifunika sehemu yake ya juu na kuviunganisha pamoja.
Akatumia zile shekeli hizo 1,775 kutengeneza kulabu za nguzo, kufunika ncha za nguzo na kutengeneza vitanzi vyake.
29 Nayo shaba ya toleo la kutikisa ilikuwa talanta sabini na shekeli 2, 400.
Shaba iliyopatikana kutokana na sadaka ya kuinuliwa ilikuwa na uzito wa talanta 70 na shekeli 2,400.
30 Naye akaitumia kufanya vile vikalio vya mwingilio wa hema la mkutano na ile madhabahu ya shaba na kile kiunzi chake cha shaba, na vyombo vyote vya madhabahu,
Akaitumia hiyo shaba kutengeneza vitako vya ingilio la Hema la Kukutania, madhabahu ya shaba pamoja na ule wavu wake na vyombo vyake vyote,
31 na vile vikalio vya ua kuzunguka pande zote, na vile vikalio vya lango la ua, na misumari yote ya maskani na misumari yote ya ua kuzunguka pande zote.
vile vitako vya ule ua uliozunguka na vile vya ingilio, na vigingi vyote vya Maskani pamoja na ule ua uliozunguka.

< Kutoka 38 >