< Torati 22 >

1 Hautakiwi kumtazama ng’ombe au kondoo wa Muisraeli mwenzako akikosea njia na ukajificha kwao; hakika unapaswa kuwarejesha kwake.
Kama ukimwona ngʼombe au kondoo wa ndugu yako anapotea, usipuuze, bali uhakikishe unamrudisha kwa mwenyewe.
2 Iwapo Muisraeli mwenzako hayupo karibu nawe, au kama haumfahamu, basi unapaswa kumleta mnyama huyo nyumbani kwako, na lazima uwe naye mpaka pale mwenyewe atakapomtafuta, na kisha lazima umrejeshee mwenyewe.
Ikiwa huyo ndugu haishi karibu nawe au kama hufahamu yeye ni nani, mchukue nyumbani kwako huyo mnyama umweke mpaka mwenyewe aje kumtafuta. Ndipo umrudishie.
3 Unapaswa kufanya vivyo hivyo kwa punda wake; unapaswa kufanya vivyo hivyo na vazi lake; unapaswa kufanya vivyo hivyo kwa kila kitu alichopoteza Muisraeli mwenzako, kitu chochote alichopoteza na ukakipata; hautakiwi kujificha.
Fanya vivyo hivyo ukimkuta punda wa nduguyo au joho lake au chochote alichopoteza. Usipuuze jambo hilo.
4 Haupaswi kumwona punda wa Muisraeli mwenzako au ng’ombe wake kaanguka chini barabarani na kujificha dhidi yao; hakika unapaswa kumsaidia kumwinua tena.
Kama ukimwona punda wa nduguyo au ngʼombe wake ameanguka barabarani, usipuuze jambo hilo. Msaidie asimame kwa miguu yake.
5 Mwanamke hatakiwi kuvaa kinachokusudiwa kwa mwanamume, vilevile mwanamume hapaswi kuvaa mavazi ya mwanamke; kwa maana yeyote afanyaye vitu hivi ni chukizo kwa Yahwe Mungu wako.
Haimpasi mwanamke kuvaa nguo za kiume wala mwanaume kuvaa nguo za kike, kwa maana Bwana Mungu wenu anachukia yeyote ambaye hufanya hivi.
6 Iwapo kiota cha ndege kikaonekana barabarani mbele yako, kwenye mti wowote au juu ya ardhi, kikiwa na makinda ya ndege au mayai ndani mwake, na mama yao akiwa juu yao au juu ya mayai, haupaswi kumchukua mama pamoja na makinda au mayai yake.
Kama ukikuta kiota cha ndege kando ya barabara, iwe juu ya mti au chini, naye ndege amelala juu ya makinda au mayai, usimchukue huyo ndege pamoja na makinda yake.
7 Hakika unapaswa kumuacha mama aende zake, ila makinda yake unaweza kuyachukua. Tii amri hii ili uenende vyema, na siku zako ziweze kurefushwa.
Waweza kuchukua makinda, lakini uwe na hakika ya kumwacha huyo ndege, ili upate kufanikiwa na uweze kuishi maisha marefu.
8 Ujengapo nyumba mpya, basi unapaswa kujenga kitalu kwa ajili ya paa yako ili usilete damu juu ya nyumba yako mtu akianguka kutoka pale.
Wakati unapojenga nyumba mpya, fanya ukuta wa kuzuia kandokando ya dari ili usijiletee hatia ya kumwaga damu juu ya nyumba yako ikiwa yeyote ataanguka kutoka humo.
9 Haupaswi kupanda shamba lako la mizabibu kwa mbegu mbili, ili kwamba mavuno yote yasichukuliwe na sehemu takatifu, mbegu uliyoipanda pamoja na matunda ya mzabibu.
Usipande aina mbili za mbegu katika shamba lako la mizabibu; ikiwa utafanya hivyo, si mazao utakayopanda tu yatakuwa najisi, bali nayo matunda ya shamba la mizabibu pia.
10 Haupaswi kulimia ng’ombe na punda kwa pamoja.
Usilime kwa maksai aliyefungwa nira pamoja na punda.
11 Haupaswi kuvaa kitambaa kilichotengenezwa kwa sufu na kitani kwa pamoja.
Usivae nguo za sufu na kitani zilizofumwa pamoja.
12 Unapaswa kutengeneza pindo katika pembe nne za nguo unayoivaa.
Fanya vishada kwenye pembe nne za joho unalovaa.
13 Iwapo mwanamume kachukua mke, kisha kalala naye, na baadae kumchukia,
Ikiwa mtu atamwoa mke na, baada ya kufanya naye tendo la ndoa, akamchukia,
14 na kisha kumtuhumu kwa vitu vya aibu na kumharibia sifa yake kwa kusema, “Nilimchukua huyu mwanamke, lakini nilipomkaribia sikukuta ushahidi waubikra kwake”.
akimsingizia na kumwita jina baya, akisema, “Nilimwoa mwanamke huyu, lakini nilipomkaribia sikupata uthibitisho wa ubikira wake”
15 Kisha baba na mama mzazi wa binti wanatakiwa kupeleka ushahidi wa ubikra wake kwa wazee mlangoni mwa mji.
ndipo baba na mama wa msichana wataleta uthibitisho kwamba alikuwa bikira kwa wazee wa mji kwenye lango.
16 Baba wa binti anapaswa kuwaambia wazee, “nilimpatia binti yangu kwa mwanamume huyu awe mkewe, naye anamchukia.
Baba wa msichana atawaambia wazee, “Nilimwoza binti yangu kwa huyu mwanaume, lakini hampendi.
17 Tazama, amemtuhumu na vitu vya aibu na kusema, “Sikukuta ushahidi wa ubikra kwa binti yako”. Lakini ushahidi huu hapa wa ubikra wa binti yangu”. Kisha watatandaza shuka mbele ya wazee wa mji.
Sasa amemsingizia na kusema, ‘Sikumkuta huyu binti akiwa bikira.’ Lakini hapa kuna uthibitisho wa ubikira wa binti yangu.” Kisha wazazi wake wataonyesha nguo zake kwa wazee wa mji,
18 Wazee wa mji wanapaswa kumchukua mwanamume huyo na kumuadhibu;
nao wazee watamchukua huyo mwanaume na kumwadhibu.
19 nao wanapaswa kumtoza faini ya shekeli mia moja ya fedha, na kumpatia baba wa binti, kwa sababu mwanamume kasababisha sifa mbaya kwa bikra wa Israeli. Binti huyu anapaswa kuwa mke wake; mwanamume huyu hatakiwi kumfukuza katika siku zake zote.
Watamtoza shekeli mia moja za fedha na kupewa wazazi wa msichana, kwa sababu mwanaume huyu amempa bikira wa Kiisraeli jina baya. Ataendelea kuwa mke wake; kamwe hawezi kumpa talaka siku zote za maisha yake.
20 Ila kama jambo hili ni la kweli, kwamba ushahidi wa bikra ya binti haukupatikana,
Hata hivyo, kama shtaka ni la kweli na hakuna uthibitisho juu ya ubikira wa huyo msichana ulioweza kupatikana,
21 basi wanapaswa kumpeleka binti mlangoni kwa baba yake, na kisha wanamume wa mji wake wanatakiwa kumpiga kwa mawe hadi afe, kwa sababu amefanya jambo la aibu katika Israeli, kwa kutenda kama kahaba chini ya nyumba ya baba yake, nanyi mtakuwa mmeondoa uovu miongoni mwenu.
huyo msichana ataletwa kwenye mlango wa nyumba ya baba yake, na hapo watu wa mji wake watampiga kwa mawe hadi afe. Amefanya kitu cha aibu katika Israeli kwa kufanya ukahaba akiwa nyumbani kwa babaye. Lazima mwondoe uovu katikati yenu.
22 Iwapo mwanamume kakutwa analala na mwanamke ambaye ni mke wa mtu, basi wote wanapaswa kufa, mwanamume aliyelala na mwanamke pamoja na mwanamke mwenyewe; nanyi mtakuwa mmeondoa uovu miongoni mwenu.
Ikiwa mwanaume atakutwa akizini na mke wa mtu mwingine, wote wawili, mwanaume na mwanamke aliyezini naye, lazima wauawe. Lazima mwondoe uovu katika Israeli.
23 Iwapo kuna msichana bikra, ambaye amechumbiwa na mwanamume, kisha mwanamume mwingine kamkuta mjini na kulala naye,
Ikiwa mwanaume atakutana na bikira mjini ambaye ameposwa na mtu akazini naye,
24 wachukueni wote wawili malangoni mwa mji, na kuwapiga mawe. Unapaswa kumpiga msichana mawe, kwa sababu hakupaza sauti kuomba msaada, ingawa alikuwa ndani ya mji. Unapaswa kumpiga mwanamume mawe, kwa sababu amemwingilia mke wa jirani yake; nanyi mtakuwa mmeondoa uovu miongoni mwenu
utawachukua wote wawili kwenye lango la mji na kuwapiga kwa mawe mpaka wafe; yule msichana kwa kuwa alikuwa mjini na hakupiga kelele kuomba msaada, na yule mwanaume kwa sababu amemtenda jeuri mke wa mtu mwingine. Lazima mwondoe uovu katikati yenu.
25 Lakini kama mwanamume amemkuta msichana aliyechumbiwa shambani, na kama akamkamata na kulala naye, basi mwanamume pekee aliyelala naye ndiye lazima afe.
Lakini ikiwa itatokea mwanaume akakutana na msichana aliyeposwa huko mashambani, akambaka, mwanaume aliyefanya hivi peke yake ndiye atakayeuawa.
26 Lakini kwake msichana msifanye chochote; hakuna dhambi inayostahili kifo kwake msichana. Kwa maana suala hili ni kama mwanamume amshambuliapo jirani yake na kumuua.
Usimtendee msichana yule jambo lolote; hajafanya dhambi inayostahili kifo. Shauri hili ni kama lile la yeyote ambaye anamshambulia na kumuua kwa makusudi jirani yake,
27 Kwa maana alimkuta shambani; msichana huyu aliyechumbiwa alipaza sauti, lakini hapakuwa na mtu wa kumuokoa.
kwa maana mwanaume huyo alimkuta msichana huko mashambani, na ingawa msichana aliyeposwa alipiga kelele, hapakuwa na mtu wa kumwokoa.
28 Iwapo mwanamume amemkuta msichana ambaye ni bikra lakini hajachumbiwa, na kama akamkamata na kulala naye, na kama wakagundulika,
Ikiwa itatokea mwanaume akutane na bikira ambaye hajaposwa na kumbaka nao wakakutwa,
29 basi mwanamume aliyelala naye lazima atoe shekeli hamsini za fedha kwa baba wa msichana, naye lazima awe mke wake, kwa sababu amemdhalilisha. Hatakiwi kumfukuza katika siku zake zote.
mwanaume atamlipa baba wa msichana shekeli hamsini za fedha. Ni lazima amwoe huyo msichana, kwa maana amemfanyia jeuri. Kamwe hawezi kumpa talaka siku zote za maisha yake.
30 Mwanamume hapaswi kumchukua mke wa baba yake kama wake; hatakiwi kuchukua haki za ndoa za baba yake.
Mwanaume asimwoe mke wa baba yake; kamwe asidhalilishe kitanda cha baba yake.

< Torati 22 >