< Ufunuo 2 >

1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika: “Haya ndiyo maneno ya yule aliyezishika zile nyota saba katika mkono wake wa kuume na ambaye hutembea kati ya vile vinara saba vya taa vya dhahabu.
“Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika hivi: “Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye ashikaye nyota saba katika mkono wake wa kulia, na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya dhahabu.
2 Nayajua matendo yako, bidii yako na saburi yako. Najua kuwa huwezi kuvumiliana na watu waovu na ya kwamba umewajaribu wale wanaojifanya kuwa mitume na kumbe sio, nawe umewatambua kuwa ni waongo.
Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu wako. Najua kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo.
3 Umevumilia na kustahimili taabu kwa ajili ya Jina langu, wala hukuchoka.
Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina langu, wala hukuvunjika moyo.
4 “Lakini nina neno dhidi yako: Umeuacha upendo wako wa kwanza.
Lakini ninayo hoja moja juu yako: wewe hunipendi tena sasa kama pale awali.
5 Kumbuka basi ni wapi ulikoangukia! Tubu na ukafanye matendo yale ya kwanza. Kama usipotubu, nitakuja kwako na kukiondoa kinara chako cha taa kutoka mahali pake.
Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukayaache madhambi yako, na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja kwako na kukiondoa kinara chako mahali pake.
6 Lakini una jambo hili kwa upande wako: Unayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo nami pia nayachukia.
Lakini nakusifu juu ya kitu kimoja: wewe unayachukia wanayoyatenda Wanikolai kama ninavyoyachukia mimi.
7 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa haki ya kula matunda toka kwa mti wa uzima, ambao uko katika paradisoya Mungu.
“Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Wale wanaoshinda nitawapa haki ya kula matunda ya mti wa uzima ulioko ndani ya bustani ya Mungu.
8 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika: “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye wa Kwanza na wa Mwisho, aliyekufa kisha akafufuka.
“Kwa malaika wa kanisa la Smurna andika hivi: “Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye wa kwanza na wa mwisho, ambaye alikufa na akaishi tena.
9 Naijua dhiki yako na umaskini wako, lakini wewe ni tajiri! Nayajua masingizio ya wale wasemao kuwa ni Wayahudi lakini sio, bali wao ni sinagogi la Shetani.
Najua taabu zako; najua pia umaskini wako, ingawaje kwa kweli wewe ni tajiri; najua kashfa walizokufanyia wale wanaojiita Wayahudi lakini si Wayahudi wa kweli, bali ni kundi lake Shetani.
10 Usiogope mateso yatakayokupata. Nakuambia ibilisi atawatia baadhi yenu gerezani ili kuwajaribu, nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.
Usiogope hata kidogo yale ambayo itakulazimu kuteseka. Sikiliza! Ibilisi anataka kuwajaribu kwa kuwatia baadhi yenu gerezani; nanyi mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Muwe waaminifu hata mpaka kufa, nami nitawapeni taji ya uzima.
11 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatadhuriwa kamwe na mauti ya pili.
“Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Wale wanaoshinda hawataumizwa na kifo cha pili.
12 “Kwa malaika wa Kanisa lililoko Pergamo andika: “Haya ndiyo maneno yake yeye aliye na upanga mkali wenye makali kuwili.
“Kwa malaika wa kanisa la Pergamoni andika hivi: “Huu ndio ujumbe wake yeye aliye na upanga mkali wenye kuwili.
13 Ninajua unakoishi, ni kule ambako Shetani ana kiti chake cha enzi. Lakini umelishika Jina langu. Wala hukuikana imani yako kwangu hata katika siku za shahidi wangu mwaminifu Antipa, ambaye aliuawa katika mji mkuu wenu, ambako ndiko anakoishi Shetani.
Najua unakoishi: Wewe unaishi kwenye makao makuu ya Shetani! Lakini bado unashikilia jina langu; hukuikana imani yako kwangu hata siku zile Antipa shahidi wangu mwaminifu, alipouawa pale mahali anapoishi Shetani.
14 “Hata hivyo, nina mambo machache dhidi yako: Unao watu wafuatao mafundisho ya Balaamu, yule aliyemfundisha Balaki kuwashawishi Waisraeli watende dhambi kwa kula vitu vilivyotolewa kafara kwa sanamu na kufanya uasherati.
Lakini ninayo machache dhidi yako: baadhi yenu ni wafuasi wa Balaamu aliyemfundisha Balaki kuwatega wana wa Israeli wale vyakula vilivyotambikiwa sanamu za kufanya uzinzi.
15 Vivyo hivyo unao wale wayashikayo mafundisho ya Wanikolai.
Vivyo hivyo, wako pia miongoni mwenu watu wanaofuata mafundisho ya Wanikolai.
16 Basi tubu! Ama sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga wa kinywa changu.
Basi, achana na madhambi yako. La sivyo, nitakuja kwako upesi na kupigana na watu hao kwa upanga utokao kinywani mwangu.
17 “Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa. Nitampa pia jiwe jeupe ambalo juu yake limeandikwa jina jipya asilolijua mtu, isipokuwa yule anayelipokea.
“Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia makanisa! “Wale wanaoshinda nitawapa ile mana iliyofichika. Nitawapa pia jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya ambalo hakuna mtu aliyelijua isipokuwa tu wale wanaolipokea.
18 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika: “Haya ndiyo maneno ya Mwana wa Mungu, ambaye macho yake ni kama mwali wa moto na ambaye miguu yake ni kama shaba iliyosuguliwa sana.
“Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi: “Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta kama moto, na miguu yake inang'aa kama shaba iliyosuguliwa.
19 Nayajua matendo yako, upendo wako na imani yako, huduma na saburi yako na kwamba matendo yako ya sasa yamezidi yale ya kwanza.
Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako, utumishi wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale awali.
20 “Hata hivyo, nina neno dhidi yako: Unamvumilia yule mwanamke Yezebeli ambaye anajiita nabii, lakini anawafundisha na kuwapotosha watumishi wangu ili wafanye uasherati na kula vyakula vilivyotolewa kafara kwa sanamu.
Lakini nina hoja moja juu yako: wewe unamvumilia yule mwanamke Yezabeli anayejiita nabii wa Mungu. Yeye huwafundisha na kuwapotosha watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu.
21 Nimempa muda ili atubu kwa ajili ya uasherati wake, lakini hataki.
Nimempa muda wa kutubu dhambi zake, lakini hataki kuachana na uzinzi wake.
22 Kwa hiyo nitamtupa kwenye kitanda cha mateso, na nitawafanya hao wanaozini naye kupata mateso makali wasipotubia njia zake.
Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na wote waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali. Naam, nitafanya hivyo, kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye.
23 Nami nitawaua watoto wake. Nayo makanisa yote yatajua kwamba Mimi ndiye nichunguzaye mioyo na nia, na kwamba nitamlipa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.
Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue kwamba mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu.
24 Basi nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, ninyi ambao hamyafuati mafundisho ya Yezebeli, wala hamkujifunza hayo yanayoitwa mambo ya ndani sana ya Shetani (sitaweka mzigo mwingine wowote juu yenu):
“Lakini ninyi wengine mlioko huko Thuatira ambao hamfuati mafundisho yake Yezabeli, na ambao hamkujifunza kile wanachokiita Siri ya Shetani, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine.
25 Lakini shikeni sana mlicho nacho, mpaka nitakapokuja.
Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja.
26 “Atakayeshinda na kutenda mapenzi yangu mpaka mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa:
“Wanaoshinda, na wale watakaozingatia mpaka mwisho kutenda ninayotaka, nitawapa mamlaka juu ya mataifa.
27 “‘Atawatawala kwa fimbo ya chuma, atawavunja vipande vipande kama chombo cha udongo’: kama vile mimi nilivyopokea mamlaka kutoka kwa Baba yangu.
Naam, nitawapa uwezo uleule nilioupokea kwa Baba: yaani, watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma na kuyavunjavunja kama chombo cha udongo.
28 Nami nitampa pia ile nyota ya asubuhi.
Tena nitawapa nyota ya asubuhi.
29 Yeye aliye na sikio na asikie yale ambayo Roho ayaambia makanisa.
“Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!

< Ufunuo 2 >