< Ufunuo 17 >

1 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba akaja akaniambia, “Njoo, nitakuonyesha adhabu ya yule kahaba mkuu, aketiye juu ya maji mengi.
Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia, “Njoo, mimi nitakuonyesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule uliojengwa juu ya maji mengi.
2 Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu wakaao duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.”
Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake.”
3 Kisha yule malaika akanichukua katika Roho akanipeleka jangwani. Huko nikamwona mwanamke mmoja ameketi juu ya mnyama mwekundu aliyejaa majina ya kumkufuru Mungu mwili mzima. Mnyama huyo alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.
Kisha, Roho akanikumba, akaniongoza mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.
4 Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake.
Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo machafu yanayoonyesha uzinzi wake.
5 Kwenye kipaji chake cha uso palikuwa pameandikwa jina: “Siri, Babeli Mkuu, Mama wa makahaba na wa machukizo ya dunia.”
Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo “Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani.”
6 Nikaona kuwa huyo mwanamke alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu, yaani, damu ya wale watu waliouawa kwa ushuhuda wa Yesu. Nilipomwona huyo mwanamke, nilistaajabu sana.
Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumtangaza Yesu. Nilipomwona nilishangaa mno.
7 Ndipo yule malaika akaniambia, “Kwa nini unastaajabu? Nitakufafanulia siri ya huyo mwanamke na huyo mnyama aliyempanda, mwenye vichwa saba na pembe kumi.
Lakini malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana vichwa saba na pembe kumi.
8 Huyo mnyama ambaye ulimwona, wakati fulani alikuwepo, lakini sasa hayupo, naye atapanda kutoka lile Shimo na kwenda kwenye maangamizo yake. Watu waishio duniani ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima tangu kuumbwa kwa ulimwengu watastaajabu kumwona huyo mnyama, kwa maana alikuwepo wakati fulani, na sasa hayupo, lakini atakuwepo. (Abyssos g12)
Huyo mnyama uliyemwona alikuwa hai hapo awali, lakini sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali, aliishi, kisha akafa na sasa anatokea tena! (Abyssos g12)
9 “Hapa ndipo penye wito wa akili pamoja na hekima. Vile vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke amevikalia.
“Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba ni vilima saba, na huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme saba.
10 Pia hivyo vichwa saba ni wafalme saba ambao miongoni mwao watano wamekwisha kuanguka, yupo mwingine hajaja bado, lakini atakapokuja, atalazimika kukaa kwa muda mfupi.
Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia, mmoja anatawala bado, na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki kwa muda mfupi.
11 Yule mnyama aliyekuwepo wakati fulani na ambaye sasa hayupo, yeye ni mfalme wa nane. Ni miongoni mwa wale saba, naye anakwenda kwenye maangamizi yake.
Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini sasa haishi tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na anakwenda zake kuharibiwa.
12 “Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi ambao bado hawajapokea ufalme, lakini watapokea mamlaka kuwa wafalme kwa saa moja pamoja na yule mnyama.
“Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado hawajaanza kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja pamoja na yule mnyama.
13 Hawa wana nia moja, nao watamwachia yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.
Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama nguvu na mamlaka yao yote.
14 Watafanya vita na Mwana-Kondoo, lakini Mwana-Kondoo atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Yeye atakuwa pamoja na watu wake walioitwa ambao ni wateule wake na wafuasi wake waaminifu.”
Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale aliowaita na kuwachagua, ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme.”
15 Kisha yule malaika akaniambia, “Yale maji uliyoyaona yule kahaba akiwa ameketi juu yake ni jamaa, makutano, mataifa na lugha.
Malaika akaniambia pia, “Yale maji uliyoyaona pale alipokaa yule mzinzi, ni mataifa, watu wa kila rangi na lugha.
16 Zile pembe kumi ulizoziona, pamoja na huyo mnyama, watamchukia huyo kahaba, watamfilisi na kumwacha uchi, watamla nyama yake na kumteketeza kwa moto.
Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia huyo mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto.
17 Kwa maana Mungu ameweka mioyoni mwao kutimiza kusudi lake kwa kukubali kumpa yule mnyama mamlaka yao ya utawala mpaka maneno ya Mungu yatakapotimia.
Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha yake, yaani kwa kukubaliana wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya kutawala, mpaka hapo neno la Mungu litakapotimia.
18 Yule mwanamke uliyemwona ni ule mji mkubwa unaotawala juu ya wafalme wa dunia.”
“Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu unaowatawala wafalme wa dunia.”

< Ufunuo 17 >