< Zaburi 86 >

1 Maombi ya Daudi. Ee Bwana, sikia na unijibu, kwa maana mimi ni maskini na mhitaji.
Sikia, Ee Yahwe, na unijibu, kwa kuwa ni maskini na mnyonge.
2 Linda maisha yangu, kwa maana nimejiweka kwako, wewe ni Mungu wangu, mwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
Unilinde, maana mimi ni mwaminifu; Mungu wangu, umuokoe mtumishi wako anayekuamini.
3 Ee Bwana, nihurumie mimi, kwa maana ninakuita mchana kutwa.
Unihurumie, Bwana, maana ninakulilia wewe mchana kutwa.
4 Mpe mtumishi wako furaha, kwa kuwa kwako wewe, Ee Bwana, ninainua nafsi yangu.
Umfurahishe mtumishi wako, maana ni kwako, Bwana, ninaomba.
5 Ee Bwana, wewe ni mwema na mwenye kusamehe, umejaa upendo kwa wote wakuitao.
Wewe, Bwana, ni mwema, na uko tayari kusamehe, na huonesha huruma kubwa kwa wale wanao kulilia wewe.
6 Ee Bwana, sikia maombi yangu, sikiliza kilio changu unihurumie.
Yahwe, sikiliza maombi yangu; sikia sauti ya ombi langu.
7 Katika siku ya shida yangu nitakuita, kwa maana wewe utanijibu.
Katika siku ya shida ninakuita wewe, kwa maana utanijibu.
8 Ee Bwana, katikati ya miungu hakuna kama wewe, hakuna matendo ya kulinganishwa na yako.
Katikati ya miungu hakuna wa kufananishwa na wewe, Bwana. Hakuna matendo kama matendo yako.
9 Ee Bwana, mataifa yote uliyoyafanya yatakuja na kuabudu mbele zako; wataliletea utukufu jina lako.
Mataifa yote ambayo umeyafanya yatakuja kwako na kusujudu mbele zako, Bwana. nao wataliheshimu jina lako.
10 Kwa maana wewe ni mkuu, na unafanya mambo ya ajabu; wewe peke yako ndiwe Mungu.
Kwa kuwa wewe ni mkuu na utendaye mambo ya ajabu; wewe pekee ndiwe Mungu.
11 Ee Bwana, nifundishe njia yako, nami nitakwenda katika kweli yako; nipe moyo usiositasita, ili niweze kulicha jina lako.
Unifundishe njia zako, Yahwe. Kisha nitatembea katika kweli yako. Unifanye kukuheshimu wewe.
12 Ee Bwana wangu, nitakusifu kwa moyo wote; nitaliadhimisha jina lako milele.
Bwana Mungu wangu, nitakusifu kwa moyo wangu wote; nitalitukuza jina lako milele.
13 Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu; umeniokoa kutoka kwenye vilindi vya kaburi. (Sheol h7585)
Kwa maana uaminifu wa agano lako ni mkuu kwangu; wewe umeokoa uhai wangu kutoka chini kuzimuni. (Sheol h7585)
14 Ee Mungu, wenye majivuno wananishambulia; kundi la watu wakatili linatafuta uhai wangu: watu wasiokuheshimu wewe.
Ee Mungu, wenye kiburi wameinuka dhidi yangu. Kundi la watu wenye vurugu wanautafuta uhai wangu. Nao hawakuheshimu wewe.
15 Lakini wewe, Ee Bwana, ni Mungu wa huruma na neema, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu.
Lakini wewe, Bwana, ni mwenye huruma na neema, hukasiliki haraka, na mwingi katika uaminifu wa agano lako na kweli.
16 Nigeukie na unihurumie; mpe mtumishi wako nguvu zako, mwokoe mwana wa mtumishi wako wa kike.
Unigeukie na unihurumie; mpe nguvu zako mtumishi wako; umuokoe mwana wa mjakazi wako.
17 Nipe ishara ya wema wako, ili adui zangu waione nao waaibishwe, kwa kuwa wewe, Ee Bwana, umenisaidia na kunifariji.
Unioneshe ishara ya fadhila zako. Kisha wale wanichukiao wataziona na kuaibishwa kwa sababu yako; Yahwe, umenisaidia na kunifariji.

< Zaburi 86 >