< Zaburi 91 >
1 Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana, atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.
Yeye aishiye katika makazi ya Aliye Juu atakaa katika uvuli wa mwenyezi.
2 Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.”
Nami nitasema kuhusu Yahwe, “Yeye ni kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ambaye niaamini katika yeye.”
3 Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji, na maradhi ya kuambukiza ya kuua.
Kwa maana yeye atakuokoa dhidi ya mtego wa mwindaji na dhidi ya pigo liletalo mauti.
4 Atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mbawa zake utapata kimbilio, uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.
Yeye atakufunika kwa mbawa zake, na chini ya mbawa zake utapata kimbilio. Uaminifu wake ni ngao na ulinzi.
5 Hutaogopa vitisho vya usiku, wala mshale urukao mchana,
Nawe hautaogopeshwa na vitisho wakati wa usiku, wala mishale ipaayo kwa siku,
6 wala maradhi ya kuambukiza yanayonyemelea gizani, wala tauni iharibuyo adhuhuri.
wala pigo lizungukalo gizani, wala ugonjwa ujao wakati wa mchana.
7 Ijapo watu elfu wataangukia kando yako, kumi elfu mkono wako wa kuume, lakini haitakukaribia wewe.
Maelfu waweza kuangukia upande wako na makumi elfu mkono wako wa kuume, lakini uovu hauwezi kukupata.
8 Utatazama tu kwa macho yako na kuona adhabu ya waovu.
Wewe utatazama tu na kuona hukumu ya waovu.
9 Kama ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako: naam, Bwana ambaye ni kimbilio langu,
Kwa kuwa Yahwe ni kimbilio langu! Umfanye Aliye Juu kuwa kimbilio lako pia.
10 basi hakuna madhara yatakayokupata wewe, hakuna maafa yataikaribia hema yako.
Hakuna uovu utakao kushinda wewe; mateso hayatakuja karibu na nyumba yako.
11 Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako, wakulinde katika njia zako zote.
Maana yeye atawaelekeza malaika moja kwa moja kukulinda wewe, na kukuwekea ulinzi katika njia zako zote.
12 Mikononi mwao watakuinua, ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.
Nao watakuinua juu kwa mikono yao ili usiweze kujigonga mguu wako kwenye jiwe.
13 Utawakanyaga simba na nyoka wakali, simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu.
Utawaangamiza simba na nyoka chini ya miguu yako; utawakanyaga wana-simba na nyoka.
14 Bwana asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa; nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.
Kwa sababu amejitoa kwangu, nitamuokoa. Nitamlinda kwa sababu yeye ni mwaminifu kwangu.
15 Ataniita, nami nitamjibu; nitakuwa pamoja naye katika taabu, nitamwokoa na kumheshimu.
Aniitapo, nitamjibu. Katika shida nitakuwa naye; nitampatia ushindi na nitamuheshimu.
16 Kwa siku nyingi nitamshibisha na kumwonyesha wokovu wangu.”
Nitamtosheleza kwa maisha malefu na kumuonesha wokovu wangu.