< Zaburi 76 >

1 Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Asafu. Wimbo. Katika Yuda, Mungu anajulikana, jina lake ni kuu katika Israeli.
Mungu amefanya mwenyewe kujulikana katika Yuda; jina lake ni kuu katika Israeli.
2 Hema lake liko Salemu, makao yake katika Sayuni.
Hema yake iko salemu; makao yake yako yako Sayuni.
3 Huko alivunja mishale imetametayo, ngao na panga, silaha za vita.
Huko ndiko alivunja mishale ya upinde, ngao, upanga, na silaha zingine za vita. (Selah)
4 Wewe unangʼaa kwa mwanga, mwenye fahari zaidi ya milima yenye utajiri wa wanyama pori.
Wewe unang'aa sana na huufunua utukufu wako, ushukapo kutoka milimani, ambako uliwauwa mateka.
5 Mashujaa hulala wametekwa nyara, hulala usingizi wao wa mwisho; hakuna hata mmoja wa watu wa vita anayeweza kuinua mikono yake.
Wenye moyo shujaa walitekwa nyara; walilala mauti. Mashujaa wote walikuwa wanyonge.
6 Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo, farasi na gari la vita vilikaa kimya.
Kwa kukemea kwako, ewe Mungu wa Yakobo, wote gari na farasi walilala mauti.
7 Wewe peke yako ndiye wa kuogopwa. Ni nani awezaye kusimama mbele yako unapokasirika?
Wewe, ndiyo wewe, ni wa kuogopwa; ni nani awezaye kusimama mbele yako wakati ukiwa na hasira?
8 Kutoka mbinguni ulitamka hukumu, nayo nchi ikaogopa, ikawa kimya:
Kutoka mbinguni wewe uliifanya hukumu yako isikike; nchi iliogopa na ikaa kimya
9 wakati wewe, Ee Mungu, ulipoinuka kuhukumu, kuwaokoa wote walioonewa katika nchi.
wakati wewe, Mungu, ulipoinuka kutekeleza hukumu na kuwaokoa wote wa nchi walio onewa. (Selah)
10 Hakika ghadhabu yako dhidi ya wanadamu inakuletea sifa, na masalia ya ghadhabu yako unajifunga mshipi.
Hakika hukumu ya hasira yako dhidi ya binadamu itakuletea wewe sifa; wewe hujifunga mwenyewe hasira yako iliyo baki.
11 Wekeni nadhiri kwa Bwana Mungu wenu na kuzitimiza; nchi zote za jirani na walete zawadi kwa Yule astahiliye kuogopwa.
Wekeni nadhiri kwa Yahwe Mungu wenu na kuzihifadhi. Nao wote wamzungukao yeye mleteeni zawadi yeye ambaye ni wa kuogopwa.
12 Huvunja roho za watawala; anaogopwa na wafalme wa dunia.
Yeye huzikata roho za wakuu; huogopwa na wafalme wa nchi.

< Zaburi 76 >