< Zaburi 5 >

1 Kwa mwimbishaji. Kwa filimbi. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, tegea sikio maneno yangu, uangalie kupiga kite kwangu.
Sikiliza nikuitapo, Yahweh; tazama kuugua kwangu.
2 Sikiliza kilio changu ili unisaidie, Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa maana kwako ninaomba.
Sikiliza sauti yangu nikuitapo, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa kuwa ni kwako Bwana naomba.
3 Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee Bwana; asubuhi naleta haja zangu mbele zako, na kusubiri kwa matumaini.
Yahweh; sikia kilio changu asubuhi; na asubuhi nitaleta dua yangu kwako na kungoja kwa matarajio.
4 Wewe si Mungu unayefurahia uovu, kwako mtu mwovu hataishi.
Hakika wewe ni Mungu usiye kubaliana na uovu; watu waovu hawawezi kuwa wageni wako.
5 Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako, unawachukia wote watendao mabaya.
Wenye kiburi hawata simama katika uwepo wako; wewe unawachukia wote wanaofanya maovu.
6 Unawaangamiza wasemao uongo. Bwana huwachukia wamwagao damu na wadanganyifu.
Nawe utawaharibu waongo; Yahweh huwadharau vurugu na watu wadanganyifu.
7 Lakini mimi, kwa rehema zako kuu, nitakuja katika nyumba yako, kwa unyenyekevu, nitasujudu kuelekea Hekalu lako takatifu.
Lakini kwangu mimi, kwa sababu ya ukuu na uaminifu wa agano lako, nitakuja nyumbani mwako; na kwa heshima nitakuinamia mbele ya hekalu lako takatifu.
8 Niongoze katika haki yako, Ee Bwana, kwa sababu ya adui zangu, nyoosha njia yako mbele yangu.
Oh Bwana, uniongoze katika haki yako kwa sababu ya adui zangu; usawazishe njia yako mbele yangu.
9 Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika, mioyo yao imejaa maangamizi. Koo lao ni kaburi lililo wazi, kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu.
Kwa kuwa midomoni mwao hamna ukweli; utu wao wa ndani ni mwovu; makoo yao ni kaburi lililo wazi; husifu kinafiki kwa ulimi wao.
10 Uwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu! Hila zao ziwe anguko lao wenyewe. Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi, kwa kuwa wamekuasi wewe.
Mungu, wafanye kuwa na hatia; mipango yao iwe kuanguka kwao! Kwa ajili ya makosa yao mengi uwatoe nje, kwa kuwa wamekuasi wewe.
11 Lakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi, waimbe kwa shangwe daima. Ueneze ulinzi wako juu yao, ili wale wapendao jina lako wapate kukushangilia.
Bali wale wanao kukimbilia wafurahi; uwafanye wapige kelele kwa shangwe siku zote kwa sababu unawapigania; uwafanye wenye furaha ndani yako, wale walipendao jina lako.
12 Kwa hakika, Ee Bwana, unawabariki wenye haki, unawazunguka kwa wema wako kama ngao.
Kwa maana utawabariki wenye haki, Yahweh; utawazunguka kwa neema kama ngao.

< Zaburi 5 >