< Zaburi 26 >

1 Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, nithibitishe katika haki, maana nimeishi maisha yasiyo na lawama; nimemtumainia Bwana bila kusitasita.
Unihukumu mimi, Yahwe, kwa kuwa nimeenenda katika uadilifu; nimeamini katika Yahwe bila kusita.
2 Ee Bwana, unijaribu, unipime, uuchunguze moyo wangu na mawazo yangu;
Unichunguze, Yahwe, na unijaribu; uujaribu usafi wa sehemu zangu za ndani na moyoni mwangu!
3 kwa maana upendo wako uko mbele yangu daima, nami natembea siku zote katika kweli yako.
Kwa maana uaminifu wa agano lako uko mbele ya macho yangu, na mwenendo wangu ni katika uaminifu wako.
4 Siketi pamoja na watu wadanganyifu, wala siandamani na wanafiki,
Mimi sichangamani na watu waovu, wala sichangamani na watu wanafiki.
5 ninachukia kusanyiko la watenda mabaya na ninakataa kuketi pamoja na waovu.
Ninachukia waovu, na siishi na waovu.
6 Ninanawa mikono yangu kwa kuwa sina hatia, naikaribia madhabahu yako, Ee Bwana,
Ninaosha mikono yangu kounesha sina hatia, na kuikaribia madhabahu yako, Yahwe,
7 nikitangaza sifa yako kwa sauti kubwa, huku nikisimulia matendo yako ya ajabu.
kuimba wimbo wa sauti ya sifa na kutoa taarifa ya matendo yako yote ya ajabu.
8 Ee Bwana, naipenda nyumba yako mahali unakoishi, mahali ambapo utukufu wako hukaa.
Yahwe, ninaipenda nyumba ninayoishi, mahali ambapo utukufu wako unaishi!
9 Usiiondoe nafsi yangu pamoja na watenda dhambi, wala uhai wangu pamoja na wamwagao damu,
Usiniangamize pamoja na wenye dhambi, au maisha yangu na watu wenye kiu ya kumwaga damu,
10 ambao mikononi mwao kuna mipango miovu, ambao mikono yao ya kuume imejaa rushwa.
ambao katika mikono yao kuna njama, na ambao mkono wa kuume umejaa rushwa.
11 Bali mimi ninaishi maisha yasiyo na lawama; nikomboe na unihurumie.
Lakini kwangu mimi, nitaenenda katika uadilifu; uniokoe na unihurumie.
12 Miguu yangu imesimama katika uwanja tambarare; katika kusanyiko kuu nitamsifu Bwana.
Miguu yangu husimama sehemu salama; katika kusanyiko la watu nitambariki Yahwe!

< Zaburi 26 >