< Mithali 1 >

1 Mithali za Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:
Mithali za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli.
2 Kwa kupata hekima na nidhamu; kwa kufahamu maneno ya busara;
Mithali hizi zinafundisha hekima na maarifa, kufundisha maneno ya busara,
3 kwa kujipatia nidhamu na busara, kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea;
ili mpate maarifa kwa ajili ya kuishi kwa kutenda wema, haki na adili.
4 huwapa busara wajinga, maarifa na akili kwa vijana;
Mithali hizi zinatoa hekima kwa wale ambao hawakufunzwa, na kuwapa vijana maarifa na hadhari.
5 wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao, wenye kupambanua na wapate mwongozo;
Watu wenye busara wasikie na kuongeza elimu yao na watu wenye ufahamu wapate mwongozo,
6 kwa kufahamu mithali na mifano, misemo na vitendawili vya wenye hekima.
kwa kuelewa mithali, misemo, vitendawili na maneno ya wenye busara.
7 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha maarifa, lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.
Hofu ya Yehova ni chanzo cha maarifa- wapumbavu hudharau hekima na nidhamu.
8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako, wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
Mwanangu, sikia fundisho la baba yako na wala usiziache kanuni za mama yako;
9 Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako, na mkufu wa kuipamba shingo yako.
zitakuwa kilemba cha neema katika kichwa chako na jebu zinazoning'inia kwenye shingo yako.
10 Mwanangu, kama wenye dhambi wakikushawishi, usikubaliane nao.
Mwanangu wenye dhambi wakikushawishi katika dhambi zao, kataa kuwafuata.
11 Kama wakisema, “Twende tufuatane; tukamvizie mtu na kumwaga damu, njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia;
Kama watasema, “haya tufuatae, tuvizie ili kufanya mauaji, tujifiche ili tuwashambulie watu wasio na hatia, pasipo sababu.
12 tuwameze wakiwa hai kama kaburi, wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni. (Sheol h7585)
Haya tuwameza wakiwa hai, kama kuzimu inavyowachukua wenye afya, na kuwa kama wale waangukao kwenye shimoni. (Sheol h7585)
13 Tutapata aina zote za vitu vya thamani na kujaza nyumba zetu kwa nyara.
Tutapata vitu vyote vya thamani; tutazijaza nyumba zetu vile tunavyoiba kwa wengine.
14 Njoo ushirikiane nasi, vitu vyote tutakavyopata tutagawana.”
Weka vitu vyako kwetu; tutakuwa na mfuko moja kwa pamoja.”
15 Mwanangu, usiandamane nao. Usiweke mguu wako katika njia zao,
Mwanangu, usitembee katika njia moja pamoja nao; usiruhusu mguu wako kugusa katika mapito yao;
16 kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi, ni wepesi kumwaga damu.
miguu ya hukimbilia mabaya na huharakisha kumwaga damu.
17 Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu wakati ndege wote wanakuona!
Kwa kuwa haina maana kumtegea ndege mtego wakati ndege anaona.
18 Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe; hujivizia tu wenyewe!
Watu hawa huvizia kujiua wenyewe—wanatega mtego kwa ajili yao wenyewe.
19 Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila; huuondoa uhai wa wale wenye mali.
Ndivyo zilivyo njia za kila ambaye hupata utajiri kwa udhalimu; mapato ya udhalimu huondoa uhai wa wenye utajiri.
20 Hekima huita kwa sauti kuu barabarani, hupaza sauti yake kwenye viwanja vikubwa;
Hekima inalia kwa sauti mtaani, inapaza sauti katika viwanja;
21 kwenye makutano ya barabara za mji zenye makelele mengi hupaza sauti, kwenye malango ya mji hutoa hotuba yake:
katika mitaa inalia kwa sauti kuu, kwenye maingilio ya milango ya mji inasema “
22 “Enyi wajinga, mtangʼangʼania ujinga wenu hadi lini? Mpaka lini wenye mizaha watafurahia mizaha, na wapumbavu kuchukia maarifa?
Mpaka lini enyi wajinga mtapenda kuwa wajinga? Mpaka lini enyi wenye dhihaka mtapenda dhihaka, na hadi lini enyi wapumbavu, mtachukia maarifa?
23 Kama mngekuwa mmeitikia karipio langu, ningekuwa nimemimina roho yangu kwenu na kuwafahamisha maneno yangu.
Zingatia karipio langu; nitatoa mawazo yangu kwa ajili yenu; nitawafahamisha maneno yangu.
24 Lakini kwa kuwa mlinikataa nilipowaita na hakuna yeyote aliyekubali niliponyoosha mkono wangu,
Nimeita, nanyi mkakataa kusikiliza; nimeunyosha mkono wangu, wala hakuna aliyezingatia.
25 kwa kuwa mliyapuuza mashauri yangu yote na hamkukubali karipio langu,
Lakini mumedharau mafundisho yangu yote na wala hamkuzingatia maelekezo yangu.
26 mimi nami nitawacheka katika maafa yenu, nitawadhihaki wakati janga litawapata:
Nitacheka katika taabu yenu, nitawadhihaki wakati wa kupatwa taabu-
27 wakati janga litawapata kama tufani, wakati maafa yatawazoa kama upepo wa kisulisuli, wakati dhiki na taabu zitawalemea.
hofu ya kutisha itawapata kama tufani na maafa yatawakumba kama upepo wa kisulisuli, taabu na uchungu vitawapata.
28 “Ndipo watakaponiita lakini sitawajibu; watanitafuta lakini hawatanipata.
Halafu wataniita, nami sitawajibu; wataniita katika hali ya kukata tamaa lakini hawataniona.
29 Kwa kuwa walichukia maarifa, wala hawakuchagua kumcha Bwana,
Kwa sababu wamechukia maarifa na hawakuchagua kuwa na hofu ya Yehova,
30 kwa kuwa hawakukubali mashauri yangu, na kukataa maonyo yangu,
hawakufuata mafundisho yangu na wakayadharau masahihisho yangu yote.
31 watakula matunda ya njia zao, na watashibishwa matunda ya hila zao.
Watakula matunda ya njia zao, na watashibishwa kwa matunda ya hila zao wenyewe.
32 Kwa kuwa ukaidi wa wajinga utawaua, nako kuridhika kwa wajinga kutawaangamiza.
kwa maana wajinga hufa wanaporudi nyuma, na kutojali kwa wapumbavu kutawaangamiza.
33 Lakini yeyote anisikilizaye ataishi kwa usalama, atatulia, bila kuwa na hofu ya madhara.”
Bali kila anisikilizaye ataishi kwa usalama na atapumzika salama pasipo hofu ya maafa.

< Mithali 1 >