< Mathayo 1 >

1 Habari za ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu:
Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu.
2 Abrahamu akamzaa Isaki, Isaki akamzaa Yakobo, Yakobo akawazaa Yuda na ndugu zake,
Ibrahimu alikuwa baba wa Isaka, na Isaka baba wa Yakobo, na Yakobo baba wa Yuda na ndugu zake.
3 Yuda akawazaa Peresi na Zera, ambao mama yao alikuwa Tamari, Peresi akamzaa Hesroni, Hesroni akamzaa Aramu,
Yuda alikuwa baba wa Peresi na Sera kwa Tamari, Peresi baba wa Hezeroni, na Hezeroni baba wa Ramu.
4 Aramu akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni,
Ramu alikuwa baba wa Aminadabu, Aminadabu baba wa Nashoni, na Nashoni baba wa Salimoni.
5 Salmoni akamzaa Boazi, na mama yake Boazi alikuwa Rahabu, Boazi akamzaa Obedi, ambaye mama yake alikuwa Ruthu, Obedi akamzaa Yese,
Salimoni alikuwa baba wa Boazi kwa Rahabu, Boazi baba wa Obedi kwa Ruth, Obedi baba wa Yese,
6 Yese akamzaa Daudi ambaye alikuwa mfalme. Daudi akamzaa Solomoni, ambaye mama yake ni yule aliyekuwa mke wa Uria.
Yese alikuwa baba wa mfalme Daudi. Daudi alikuwa baba wa Sulemani kwa mke wa Uria.
7 Solomoni akamzaa Rehoboamu, Rehoboamu akamzaa Abiya, Abiya akamzaa Asa,
Sulemani alikuwa baba wa Rehoboamu, Rehoboamu baba wa Abiya, Abiya baba wa Asa.
8 Asa akamzaa Yehoshafati, Yehoshafati akamzaa Yoramu, Yoramu akamzaa Uzia,
Asa alikuwa baba wa Yehoshafati, Yehoshafati baba wa Yoramu, na Yoramu baba wa Uzia.
9 Uzia akamzaa Yothamu, Yothamu akamzaa Ahazi, Ahazi akamzaa Hezekia,
Uzia alikuwa baba wa Yothamu, Yothamu baba wa Ahazi, Ahazi baba wa Hezekia.
10 Hezekia akamzaa Manase, Manase akamzaa Amoni, Amoni akamzaa Yosia,
Hezekia alikuwa baba wa Manase, Manase baba wa Amoni na Amoni baba wa Yosia.
11 wakati wa uhamisho wa Babeli, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake.
Yosia alikuwa baba wa Yekonia na kaka zake wakati wa kuchukuliwa kwenda Babeli.
12 Baada ya uhamisho wa Babeli: Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli akamzaa Zerubabeli,
Na baada ya kuchukuliwa kwenda Babeli, Yekonia alikuwa baba wa Shatieli, Shatieli alikuwa babu yake na Zerubabeli.
13 Zerubabeli akamzaa Abiudi, Abiudi akamzaa Eliakimu, Eliakimu akamzaa Azori,
Zerubabeli alikuwa baba wa Abiudi, Abiudi baba wa Eliakimu, na Eliakimu baba wa Azori.
14 Azori akamzaa Sadoki, Sadoki akamzaa Akimu, Akimu akamzaa Eliudi,
Azori alikuwa baba wa Zadoki, Zadoki baba wa Akimu, na Akimu baba wa Eliudi.
15 Eliudi akamzaa Eleazari, Eleazari akamzaa Matani, Matani akamzaa Yakobo,
Eliudi alikuwa baba wa Elieza, Elieza baba wa Matani na Matani baba wa Yakobo.
16 naye Yakobo akamzaa Yosefu ambaye alikuwa mumewe Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.
Yakobo alikuwa baba wa Yusufu mume wa Mariamu, ambaye kwa yeye Yesu alizaliwa, aitwaye Kristo.
17 Hivyo, kulikuwepo na jumla ya vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi hadi wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli, na vizazi kumi na vinne tangu wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli hadi Kristo.
Vizazi vyote tangu Ibrahimu hadi Daudi vilikuwa vizazi kumi na vinne, kutoka Daudi hadi kuchukuliwa kwenda Babeli vizazi kumi na vinne, na kutoka kuchukuliwa kwenda Babeli hadi Kristo vizazi kumi na vinne.
18 Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana kuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikuwa kwa namna hii. Mama yake, Mariamu, alichumbiwa na Yusufu, lakini kabla hawajakutana, alionekana kuwa na mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.
19 Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.
Mume wake Yusufu, alikuwa mtu mwenye haki hakutaka kumwaibisha hadharani. Aliamua kusitisha uchumba wake naye kwa siri.
20 Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
Alipokuwa akifikiri juu ya mambo haya, Malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema,'' Yusufu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Mariamu kama mkeo, kwa sababu mimba aliyonayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
21 Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”
Atajifungua mtoto wa kiume na utamwita jina lake Yesu, kwa maana atawaokoa watu wake na dhambi zao.''
22 Haya yote yalitukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema:
Yote haya yalitokea kutimizwa kile kilichonenwa na Bwana kwa njia ya nabii, akisema,
23 “Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli”: maana yake, “Mungu pamoja nasi.”
“Tazama, bikira atachukua mimba na kuzaa mtoto wa kiume, na watamwita jina lake Imanueli”— maana yake, “Mungu pamoja nasi.”
24 Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake.
Yusufu aliamka kutoka usingizini na kufanya kama malaika wa Bwana alivyomwamuru na alimchukua kama mkewe.
25 Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.
Hata hivyo, hakulala naye mpaka alipojifungua mtoto wa kiume na alimwita jina lake Yesu.

< Mathayo 1 >