< Mathayo 2 >
1 Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Uyahudi, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu
Baada ya Yesu kuzaliwa katika Bethelehem ya Uyahudi katika siku za mfalme Herode, watu wasomi kutoka mashariki ya mbali walifika Yerusalemu wakisema,
2 wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.”
“Yuko wapi yeye ambaye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi? Tuliiona nyota yake mashariki nasi tumekuja kumwabudu.”
3 Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu.
Pindi Mfalme herode aliposikia haya alifadhaika, na Yerusalemu yote pamoja naye.
4 Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, akawauliza ni mahali gani ambapo Kristo angezaliwa.
Herode akawakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, naye akawauliza, “Kristo atazaliwa wapi?”
5 Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Uyahudi, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:
Wakamwabia, “Katika Bethelehemu ya Uyahudi, kwa kuwa hivi ndivyo ilivyoandikwa na nabii,
6 “‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, wewe si mdogo miongoni mwa watawala wa Yuda; kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala atakayekuwa mchungaji wa watu wangu Israeli.’”
Nawe Bethelehemu, katika nchi ya Yuda, si mdogo miongoni mwa viongozi wa Yuda, kwa kuwa kutoka kwako atakuja mtawala atakayewachunga watu wangu Israeli.”
7 Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana.
Hivyo Herode aliwaita wale wasomi kwa siri na kuwauliza ni wakati gani hasa nyota ilikuwa imeonekana.
8 Kisha akawatuma waende Bethlehemu akiwaambia, “Nendeni mkamtafute kwa bidii huyo mtoto. Nanyi mara mtakapomwona, mniletee habari ili na mimi niweze kwenda kumwabudu.”
Akawatuma Bethelehem, akisema, “Nendeni kwa uangalifu mkamtafute mtoto aliyezaliwa. Wakati mtakapomwona, nileteeni habari ili kwamba mimi pia niweze kuja na kumwabudu.”
9 Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata mpaka iliposimama mahali pale alipokuwa mtoto.
Baada ya kuwa wamemsikia mfalme, waliendelea na safari yao, na nyota ile waliyokuwa wameiona mashariki iliwatangulia hadi iliposimama juu ya mahali mtoto aliyezaliwa alipokuwa.
10 Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno.
Wakati walipoiona nyota, walifurahi kwa furaha kuu mno.
11 Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane.
Waliingia nyumbani na kumuona mtoto aliyezaliwa na Mariamu mama yake. Walimsujudia na kumwabudu. Walifungua hazina zao na kumtolea zawadi za dhahabu, uvumba, na manemane.
12 Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine.
Mungu aliwaonya katika ndoto wasirudi kwa Herode, hivyo, waliondoka kurudi katika nchi yao kwa njia nyingine.
13 Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”
Baada ya kuwa wameondoka, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto na kusema, “Inuka, mchukue mtoto na mama yake na mkimbilie Misri. Bakini huko mpaka nitakapowaambia, kwa kuwa Herode atamtafuta mtoto ili amwangamize.
14 Kisha Yosefu akaondoka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri
Usiku huo Yusufu aliamka na kumchukua mtoto na mama yake na kukimbilia Misri.
15 ambako walikaa mpaka Herode alipofariki. Hili lilifanyika ili litimie lile lililonenwa na Bwana kwa kinywa cha nabii kusema: “Nilimwita mwanangu kutoka Misri.”
Aliishi huko hadi Herode alipo kufa. Hii ilitimiza kile Bwana alichokuwa amenena kupitia nabii, “Kutoka Misri nimemwita mwanangu.”
16 Herode alipongʼamua kwamba wale wataalamu wa nyota wamemshinda kwa akili, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kufuatana na ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota.
Kisha Herode, alipoona kuwa amedhihakiwa na watu wasomi, alikasirika sana. Aliagiza kuuawa kwa watoto wote wa kiume waliokuwa Bethelehemu na wote katika eneo lile ambao walikuwa na umri wa miaka miwili na chini yake kulingana na wakati aliokuwa amekwisha thibitisha kabisa kutoka kwa wale watu wasomi.
17 Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia.
Ndipo lilipotimizwa lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yeremia,
18 “Sauti ilisikika huko Rama, maombolezo na kilio kikubwa, Raheli akilia kwa ajili ya wanawe, akikataa kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.”
“Sauti ilisikika Ramah, kilio na maombolezo makubwa, Raheli akiwalilia watoto wake, na alikataa kufarijiwa, kwa sababu hawapo tena.”
19 Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto huko Misri
Herode alipo kufa, tazama malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri na kusema,
20 na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wanatafuta uhai wa mtoto wamekufa.”
“Inuka mchukue mtoto na mama yake, na mwende katika nchi ya Israeli kwa maana waliokuwa wakitafuta uhai wa mtoto wamekufa.”
21 Basi Yosefu, akaondoka akamchukua mtoto na mama yake wakaenda mpaka nchi ya Israeli.
Yusufu aliinuka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake, na wakaja katika nchi ya Israeli.
22 Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Uyahudi mahali pa Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya,
Lakini aliposikia kuwa Arikelau alikuwa anatawala Yuda mahali pa baba yake Herode, aliogopa kwenda huko. Baada ya Mungu kumuonya katika ndoto, aliondoka kwenda mkoa wa Galilaya
23 akaenda akaishi katika mji ulioitwa Nazareti. Hivyo likawa limetimia neno lililonenwa na manabii, “Ataitwa Mnazarayo.”
na alienda kuishi katika mji uitwao Nazareti. Hili lilitimiza kile kilichokuwa kimekwisha kunenwa kwa njia ya manabii, kwamba ataitwa Mnazareti.