< Waamuzi 6 >
1 Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele za Bwana, naye kwa miaka saba Bwana akawatia mikononi mwa Wamidiani.
Wana wa Israeli wakafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana; naye akawatia mikononi mwa Midiani kwa miaka saba.
2 Mkono wa Midiani ukawa na nguvu dhidi ya Israeli na kwa ajili ya Wamidiani, Waisraeli wakajitengenezea mahali pa kujificha milimani, kwenye mapango na ngome.
Uwezo wa Midiani uliwanyanyasa Israeli. Kwa sababu ya Midiani, watu wa Israeli walitengeneza makao wenyewe kutoka kwenye mabwawa katika milima, mapango, na ngome.
3 Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao.
Kisha ikawa kwamba wakati wowote Waisraeli walipopanda mazao yao, Wamidiani na Waamaleki na watu kutoka mashariki waliwavamia Waisraeli.
4 Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe chochote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ngʼombe au punda.
Waliweza kutengenezajeshi lao juu ya ardhi na kuharibu mazao, mpaka njia ya Gaza. Hawakuacha chakula huko Israeli, wala kondoo wala ng'ombe wala punda.
5 Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia zao; wakavamia nchi ili kuiharibu.
Kila wakati wao na mifugo yao na mahema walipokuja, walikuja kama kundi la nzige, na haikuwezekana kuhesabu watu au ngamia zao. Walivamia ardhi ili kuiharibu.
6 Waisraeli wakafanywa kuwa maskini sana na Wamidiani, hata Israeli wakamlilia Bwana kuomba msaada.
Midiani iliwadhoofisha Waisraeli sana mpaka watu wa Israeli wakamwita Bwana.
7 Waisraeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Wamidiani,
Watu wa Israeli walipomwomba Bwana kwa sababu ya Midiani,
8 Bwana akawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa.
Bwana alimtuma nabii kwa wana wa Israeli. Nabii akawaambia, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimekuleta kutoka Misri; Nilikutoa nje ya nyumba ya utumwa.
9 Nikawanyakua kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu nami nikawapa ninyi nchi yao.
Naliwaokoa kutoka kwenye mikono ya Wamisri, na kutoka kwenye mkono wa wote waliokuwa wakikunyanyasa. Niliwafukuza mbele yenu, na nimewapa nchi yao.
10 Nikawaambia, ‘Mimi ndimi Bwana Mungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambayo mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.”
Niliwaambia, “Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu; Nimewaamuru msiabudu miungu ya Waamori, ambao mnaishi katika nchi yao. Lakini hamkuitii sauti yangu.”
11 Malaika wa Bwana akaja akaketi chini ya mti wa mwaloni huko Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi, Mwabiezeri, ambako Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione.
Basi malaika wa Bwana akaja na kukaa chini ya mwaloni huko Ofra, uliokuwa wa Yoashi (Mwabiyezeri), wakati Gidioni, mwana wa Yoashi, akitenganisha ngano katika sakafu, katika kikapu cha divai-kuificha toka kwa Wamidiani.
12 Malaika wa Bwana alipomtokea Gideoni, akamwambia, “Bwana yu pamoja nawe, Ewe shujaa mwenye nguvu.”
Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nanyi, mpiganaji mwenye nguvu!
13 Gideoni akajibu, “Ee Bwana wangu, kama Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi basi yale matendo yake makuu baba zetu waliyotusimulia juu yake waliposema, ‘Je, Bwana hakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasa Bwana ametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.”
Gideoni akamwambia, Oo, bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, kwa nini basi yote haya yanatupata? Je, yako wapi matendo yake yote mazuri ambayo baba zetu walituambia, waliposema, 'Je! si Bwana aliyetukomboa kutoka Misri?' Lakini sasa Bwana ametuacha na kututia mikononi mwa Midiani. '
14 Bwana akamgeukia na kusema “Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?”
Bwana akamtazama na kusema, “Nenda katika nguvu uliyo nayo tayari. Uiokoe Israeli kutoka mkononi wa Midiani. Je, sikukutuma?”
15 Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.”
Gideoni akamwambia, “Tafadhali, Bwana, nawezeje kuwaokoa Israeli? Angalia, familia yangu ni dhaifu zaidi katika Manase, na mimi si muhimu katika nyumba ya baba yangu.”
16 Bwana akamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.”
Bwana akamwambia, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utalishinda jeshi lote la Midiani kama mtu mmoja.”
17 Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonyesha kweli kwamba ni wewe unayesema nami.
Gideoni akamwambia, “Ikiwa unapendezwa na mimi, nipe basi ishara kwamba wewe ndio unenena nami.
18 Tafadhali ninakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea sadaka yangu na kuiweka mbele yako.” Naye Bwana akamwambia, “Nitangoja mpaka utakaporudi.”
Tafadhali, usiondoke hapa, mpaka nitakapokuja kwako na kuleta zawadi yangu na kuiweka mbele yako.” Bwana akasema, “Nitasubiri mpaka utakaporudi.”
19 Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mti wa mwaloni na kumpa.
Gideoni akaenda, akaandaa mwana mbuzi, na efa moja ya unga akafanya mikate isiyotiwa chachu. Akaiweka nyama hiyo katika kikapu, na akaweka mchuzi ndani ya sufuria na kuviletea chini ya mti wa mwaloni, akavitowa.
20 Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo.
Malaika wa Mungu akamwambia, “Chukua nyama na mikate isiyotiwa chachu, ukaweke juu ya mwamba huu, ukamwage mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo.
21 Malaika wa Bwana akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa Bwana akatoweka kutoka machoni pake.
Kisha malaika wa Bwana akashika ncha ya fimbo mkononi mwake. Kwa hiyo akagusa nyama na mikate isiyotiwa chachu; moto ukatoka nje ya mwamba, ukateketeza nyama na mikate isiyotiwa chachu. Kisha malaika wa Bwana akaenda, na Gideoni hakuweza kumwona tena.
22 Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa Bwana, akapiga kelele kwa mshangao, akasema, “Ole wangu, Bwana Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Bwana uso kwa uso!”
Gideoni alielewa kuwa yule alikuwa malaika wa Bwana. Gideoni akasema, “Ewe Bwana MUNGU! Kwa maana nimemwona malaika wa Bwana uso kwa uso!”
23 Lakini Bwana akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”
Bwana akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope, huwezi kufa.”
24 Hivyo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu mahali pale na kupaita, Yehova-Shalom. Mpaka leo ingalipo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.
Basi Gideoni akamjengea Bwana madhabahu huko. Aliiita, “Bwana ni Amani.” Hadi leo bado iko katika Ofra ya jamaa ya Waabiezeri.
25 Usiku ule ule Bwana akamwambia, “Mchukue ngʼombe dume wa baba yako, yaani, yule wa pili mwenye miaka saba, na ubomoe madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate Ashera iliyo karibu nayo.
Usiku huo, Bwana akamwambia, “Twaa ng'ombe wa baba yako, na ng'ombe wa pili wa umri wa miaka saba, ukaondoe madhabahu ya Baali, ambayo ni ya baba yako, na kukata Ashera iliyo karibu nayo.
26 Kisha mjengee Bwana Mungu wako, madhabahu halisi, kwa taratibu zake, juu ya huu mwamba. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.”
Jenga madhabahu kwa Bwana, Mungu wako juu ya mahali pa kukimbilia, na kuijenga njia sahihi. Toa ng'ombe ya pili kama sadaka ya kuteketezwa, ukitumia kuni kutoka Ashera uliyoikata. '
27 Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kama Bwana alivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana.
Gideoni akachukua watumishi wake kumi na kufanya kama Bwana alivyomwambia. Lakini kwa sababu aliogopa sana watu wa nyumba ya baba yake na watu wa mji hakufanya hivyo wakati wa mchana, alifanya hivyo usiku.
28 Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa na yule ngʼombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu yaliyojengwa upya!
Asubuhi wakati watu wa mji walipoamka, madhabahu ya Baali imebomolewa, na Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na ng'ombe wa pili ametolewa sadaka kwenye madhabahu iliyojengwa.
29 Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?” Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye alitenda hivi.”
Watu wa mji wakaambiana, “Ni nani aliyefanya jambo hili?” Walipokuwa wakiongea na wengine na kutafuta majibu, wakasema, 'Gidioni mwana wa Yoashi amefanya jambo hili.”
30 Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”
Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mtoe mtoto wako ili afe, kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali, na kwa sababu ameikata Ashera karibu nayo.”
31 Lakini Yoashi akauambia ule umati uliokuwa umezunguka ukiwa kinyume naye, “Je, ninyi mtamtetea Baali? Mnajaribu kumwokoa? Yeyote mwenye kumpigania atauawa kufikia kesho asubuhi! Kama Baali ni mungu kweli, anaweza kujitetea mwenyewe wakati mtu anapobomoa madhabahu yake.”
Yoashi akawaambia wote waliompinga, “Je, ninyi mtamsihi Baali? Je, mtamuokoa? Mtu yeyote atakayemtetea, basi atauawa asubuhi hii. Ikiwa Baali ni mungu, basi atajitetea mwenyewe wakati mtu anaibomoa madhabahu yake.”
32 Basi siku ile wakamwita Gideoni “Yerub-Baali,” yaani, “Baali na ashindane naye,” kwa sababu alibomoa madhabahu yake.
Kwa hiyo siku hiyo wakamwita Gideoni “Yerubaali,” kwa sababu alisema, “Baali ajijitetee dhidi yake,” kwa sababu Gidioni alivunja madhabahu ya Baali.
33 Basi Wamidiani wote, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki wakaunganisha majeshi yao, wakavuka ngʼambo ya Yordani na kupiga kambi katika Bonde la Yezreeli.
Basi Wamidiani wote, Waamaleki, na watu wa mashariki walikusanyika pamoja. Wakavuka Yordani na wakapanga katika bonde la Yezreeli.
34 Ndipo Roho wa Bwana akamjia Gideoni, akapiga tarumbeta, akiwaita Waabiezeri ili wamfuate.
Lakini Roho wa Bwana akaja juu ya Gideoni. Gideoni akapiga tarumbeta, akawaita jamaa ya Abiezeri, ili wapate kumfuata.
35 Akatuma wajumbe waende katika Manase yote, akiwataka wachukue silaha na pia katika Asheri, Zabuloni na Naftali, nao wakakwea ili kukutana nao.
Aliwatuma wajumbe wote katika Manase, na wao pia, waliitwa nje kumfuata. Naye akatuma wajumbe kwa Asheri, na Zabuloni, na Naftali; nao wakaenda kumlaki.
36 Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi:
Gideoni akamwambia Mungu, “Ikiwa ungependa kunitumia kuokoa Israeli, kama ulivyosema,
37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo kwenye kiwanja cha kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya ngozi tu, nayo ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.”
tazameni, ninaweka ngozi ya samazi kwenye sakafu. Ikiwa kuna umande tu juu ya ngozi, na ni kavu duniani, basi nitajua kwamba utanitumia kuokoa Israeli, kama ulivyosema.”
38 Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akaikamua ile ngozi, umande ukatoka, maji ya kujaa bakuli.
Hivi ndivyo ilivyotokea-Gideoni aliamka mapama asubuhi, akaikamua ngozi hiyo, na akatoa umande kwenye ngozi, wa kutosha kujaza bakuli kwa maji.
39 Kisha Gideoni akamwambia Bwana, “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa ngozi hii. Wakati huu uifanye ngozi hii kavu na ardhi yote ifunikwe na umande.”
Gideoni akamwambia Mungu, 'Usinikasirikie, nitasema tena kwa mara nyingine. Tafadhali niruhusu nijaribu tena kwa kutumia ngozi. Wakati huu uifanye kavu, na iwe na umande juu ya ardhi yote kuzunguka.
40 Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Ngozi ile ilikuwa kavu, nayo ardhi yote ikafunikwa na umande.
Mungu alifanya kile alichoomba usiku huo. Ngozi ilikuwa kavu, na kulikuwa na umande katika ardhi yote iliyozunguka.