< Yohana 8 >
1 Lakini Yesu akaenda katika Mlima wa Mizeituni.
lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni.
2 Alfajiri na mapema Yesu akaja tena Hekaluni, watu wote wakakusanyika, akakaa akaanza kuwafundisha.
Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena Hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha.
3 Walimu wa sheria na Mafarisayo wakamleta mwanamke mmoja aliyefumaniwa akizini. Wakamsimamisha katikati ya umati wa watu wote.
Basi, walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao.
4 Wakamwambia Yesu, “Mwalimu, huyu mwanamke amekutwa akizini.
Kisha wakamwuliza Yesu, “Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi.
5 Katika sheria, Mose alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake wa namna hii, mpaka wafe. Sasa wewe wasemaje?”
Katika Sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?”
6 Walimuuliza swali hili kama mtego ili wapate sababu ya kumshtaki. Lakini Yesu akainama akaanza kuandika ardhini kwa kidole chake.
Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole.
7 Walipoendelea kumuulizauliza akainuka, akawaambia, “Kama kuna mtu yeyote miongoni mwenu ambaye hana dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe.”
Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, “Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe.”
8 Akainama tena na kuandika ardhini.
Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini.
9 Waliposikia haya, wakaanza kuondoka mmoja mmoja, wakianzia wazee, hadi Yesu akabaki peke yake na yule mwanamke akiwa amesimama mbele yake.
Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale.
10 Yesu akainuka na kumwambia, “Wako wapi wale waliokuwa wanakuhukumu kuwa mwenye hatia?”
Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, “Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?”
11 Yule mwanamke akajibu, “Hakuna hata mmoja Bwana.” Yesu akamwambia, “Hata mimi sikuhukumu. Nenda zako, kuanzia sasa usitende dhambi tena.”]
Huyo mwanamke akamjibu, “Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!” Naye Yesu akamwambia, “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena.”
12 Kisha Yesu akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”
Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, “Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima.”
13 Mafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.”
Basi, Mafarisayo wakamwambia, “Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali.”
14 Yesu akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli kwa sababu najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.
Yesu akawajibu, “Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.
15 Ninyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu, mimi simhukumu mtu yeyote.
Ninyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.
16 Lakini hata kama nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu peke yangu, bali niko pamoja na Baba, aliyenituma.
Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.
17 Imeandikwa katika Sheria yenu kwamba, ushahidi wa watu wawili ni thabiti.
Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.
18 Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.”
Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia.”
19 Ndipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.”
Hapo wakamwuliza, “Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu “Ninyi hamnijui mimi wala hamumjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia.”
20 Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia.
Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha Hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
21 Yesu akawaambia tena, “Ninaenda zangu, nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi ninyi hamwezi kuja.”
Yesu akawaambia tena, “Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kufika.”
22 Ndipo wale Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Je, hii ndiyo sababu amesema, ‘Niendako mimi ninyi hamwezi kuja’?”
Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, “Je, atajiua? Mbona anasema: Niendako ninyi hamwezi kufika?”
23 Akawaambia, “Ninyi mmetoka chini, mimi nimetoka juu. Ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
Yesu akawaambia, “Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
24 Niliwaambia kuwa mtakufa katika dhambi zenu, kwa maana msipoamini ya kwamba ‘Mimi Ndiye,’ mtakufa katika dhambi zenu.”
Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba Mimi ndimi, mtakufa katika dhambi zenu.”
25 Wakamuuliza, “Wewe ni nani?” Naye Yesu akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nimekuwa nikiwaambia tangu mwanzo.
Nao wakamwuliza, “Wewe ni nani?” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni tangu mwanzo!
26 Nina mambo mengi ya kusema juu yenu na mengi ya kuwahukumu. Lakini yeye aliyenituma ni wa kweli, nami nanena na ulimwengu niliyoyasikia kutoka kwake.”
Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake.”
27 Hawakuelewa kuwa alikuwa akiwaambia juu ya Baba yake wa Mbinguni.
Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.
28 Kisha Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha kumwinua juu Mwana wa Adamu, ndipo mtakapojua kuwa, ‘Mimi ndiye yule niliyesema na kwamba mimi sitendi jambo lolote peke yangu bali ninasema yale tu ambayo Baba yangu amenifundisha.
Basi, Yesu akawaambia, “Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu hapo ndipo mtakapojua kwamba Mimi ndimi, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha.
29 Yeye aliyenituma yu pamoja nami, hajaniacha, kwa kuwa siku zote nafanya mapenzi yake.’”
Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza.”
30 Wengi waliomsikia Yesu akisema maneno haya wakamwamini.
Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini.
31 Kisha Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkidumu katika maneno yangu, mtakuwa wanafunzi wangu kweli kweli.
Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu.
32 Ndipo mtaijua kweli nayo kweli itawaweka huru.”
Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru.”
33 Wao wakamjibu, “Sisi tu wazao wa Abrahamu, nasi hatujawa watumwa wa mtu yeyote. Wawezaje kusema kwamba tutawekwa huru?”
Nao wakamjibu, “Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: mtakuwa huru?”
34 Yesu akajibu, “Amin, amin nawaambia, kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.
Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi.
35 Mtumwa hakai nyumbani anakotumika siku zote, lakini mwana hukaa nyumbani daima. (aiōn )
Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu. (aiōn )
36 Hivyo Mwana akiwaweka huru mtakuwa huru kweli kweli.
Kama mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli.
37 Ninajua ya kuwa ninyi ni wazao wa Abrahamu, lakini mnatafuta wasaa wa kuniua kwa sababu ndani yenu hamna nafasi ya neno langu.
Najua kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamuyakubali mafundisho yangu.
38 Ninasema yale niliyoyaona mbele za Baba yangu, nanyi inawapa kufanya yale mliyosikia kutoka kwa baba yenu.”
Mimi nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu.”
39 Wakajibu, “Baba yetu ni Abrahamu.” Yesu akawaambia, “Kama mngekuwa wazao wa Abrahamu mngefanya mambo yale aliyofanya Abrahamu.
Wao wakamjibu, “Baba yetu ni Abrahamu!” Yesu akawaambia, “Kama ninyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu,
40 Lakini sasa ninyi mnatafuta kuniua, mtu ambaye nimewaambia kweli ile niliyosikia kutoka kwa Mungu, Abrahamu hakufanya jambo la namna hii.
Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo!
41 Ninyi mnafanya mambo afanyayo baba yenu.” Wakamjibu, “Sisi hatukuzaliwa kwa uzinzi. Tunaye Baba mmoja, Mungu pekee.”
Ninyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu.” Wao wakamwambia, “Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu.”
42 Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda, kwa maana nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
43 Kwa nini hamwelewi ninayowaambia? Ni kwa sababu hamwezi kusikia nisemacho.
Kwa nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu.
44 Ninyi ni watoto wa baba yenu ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo.
Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo.
45 Lakini kwa sababu nimewaambia kweli hamkuniamini!
Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini.
46 Je, kuna yeyote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa mwenye dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini?
Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini?
47 Yeye atokaye kwa Mungu husikia kile Mungu asemacho. Sababu ya ninyi kutosikia ni kwa kuwa hamtokani na Mungu.”
Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini ninyi hamsikilizi kwa sababu ninyi si (watu wa) Mungu.”
48 Wayahudi wakamjibu Yesu, “Je, hatuko sahihi tunaposema ya kwamba wewe ni Msamaria na ya kwamba una pepo mchafu?”
Wayahudi wakamwambia, “Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?”
49 Yesu akawajibu, “Mimi sina pepo mchafu, bali ninamheshimu Baba yangu, nanyi mnanidharau.
Yesu akajibu, “Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini ninyi hamniheshimu.
50 Lakini mimi sitafuti utukufu wangu mwenyewe, bali yuko anayetaka kunitukuza, naye ndiye mwamuzi.
Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu.
51 Amin, amin nawaambia, mtu yeyote akilitii neno langu hataona mauti milele.” (aiōn )
Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele.” (aiōn )
52 Ndipo Wayahudi wakamwambia, “Sasa tumejua kwamba una pepo mchafu. Ikiwa Abrahamu alikufa na vivyo hivyo manabii, nawe unasema ‘Mtu akitii neno langu hatakufa milele.’ (aiōn )
Basi, Wayahudi wakasema, “Sasa tunajua kweli kwamba wewe ni mwendawazimu! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele! (aiōn )
53 Je, wewe ni mkuu kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa na manabii ambao nao pia walikufa? Hivi wewe unajifanya kuwa nani?”
Je, unajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?”
54 Yesu akawajibu, “Kama nikijitukuza utukufu wangu hauna maana. Baba yangu, huyo ambaye ninyi mnadai kuwa ni Mungu wenu, ndiye anitukuzaye mimi.
Yesu akawajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye ninyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza.
55 Ingawa hamkumjua, mimi ninamjua. Kama ningesema simjui, ningekuwa mwongo kama ninyi, lakini mimi ninamjua na ninalitii neno lake.
Ninyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi. Mimi namjua na ninashika neno lake.
56 Baba yenu Abrahamu alishangilia kwamba angaliiona siku yangu, naye akaiona na akafurahi.”
Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi.”
57 Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza hata miaka hamsini, wewe wasema umemwona Abrahamu?”
Basi, Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?”
58 Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, kabla Abrahamu hajakuwako, ‘Mimi niko.’”
Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko.”
59 Ndipo wakaokota mawe ili kumpiga, lakini Yesu akajificha, naye akatoka Hekaluni.
Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka Hekaluni.