< Matendo 1 >

1 Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia, mpendwa Theofilo, kuhusu mambo yote Yesu aliyofanya na kufundisha tangu mwanzo,
Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake
2 hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maagizo kupitia kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua.
mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua.
3 Baada ya mateso yake, alijionyesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu Ufalme wa Mungu.
Kwa muda wa siku arobaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu.
4 Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake.
Wakati walipokutana pamoja aliwaamuru hivi: “Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeeni ile zawadi aliyoahidi Baba, zawadi ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake.
5 Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
6 Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”
Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, “Je Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?”
7 Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.
Lakini Yesu akawaambia, “Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini.
8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”
Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni ninyi, mtajazwa nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia.”
9 Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.
Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena.
10 Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao,
Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao,
11 wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”
wakasema, “Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mliivyomwona akienda mbinguni.”
12 Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato kutoka mjini.
Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini.
13 Walipowasili mjini Yerusalemu, walikwenda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Wale waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Tomaso, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo.
Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo.
14 Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwepo wanawake kadha, na Maria mama yake Yesu, pamoja na ndugu zake Yesu.
Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake.
15 Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao wote walikuwa watu wapatao 120), akasema,
Siku chache baadaye, kulikuwa na mkutano wa waumini, karibu watu mia moja na ishirini. Petro alisimama mbele yao,
16 “Ndugu zangu, ilibidi Andiko litimie ambalo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu.
akasema, “Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni.
17 Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”
Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu.
18 (Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje.
(“Mnajua kwamba yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu. Akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje.
19 Kila mtu Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu).
Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba Hekeli Dama, maana yake, Shamba la Damu.)
20 “Kama vile ilivyoandikwa katika kitabu cha Zaburi, “‘Mahali pake na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi humo,’ na, “‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake ya uongozi.’
Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi: Nyumba yake ibaki mahame; mtu yeyote asiishi ndani yake. Tena imeandikwa: Mtu mwingine achukue nafasi yake katika huduma hiyo.
21 Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Yesu alipoingia na kutoka katikati yenu,
Kwa hiyo, ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi kama shahidi wa ufufuo wake Bwana Yesu.
22 kuanzia ubatizo wa Yohana mpaka siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”
Anapaswa kuwa mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana alipokuwa anasafiri pamoja nasi, tangu wakati Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni.”
23 Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yosefu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya.
Basi, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia.
24 Kisha wakaomba, wakasema, “Bwana, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua
Kisha wakasali: “Bwana, wewe unajua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua
25 ili achukue nafasi ya huduma ya utume ambayo Yuda aliiacha ili aende mahali pake mwenyewe.”
ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe.”
26 Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.
Hapo, wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.

< Matendo 1 >