< Yohana 10 >
1 “Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, ni mwizi na mnyangʼanyi.
Yesu alisema “Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang'anyi.
2 Yeye anayeingia kwa kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo.
Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo.
3 Mlinzi humfungulia lango na kondoo huisikia sauti yake. Huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi.
Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje.
4 Akiisha kuwatoa wote nje, hutangulia mbele yao na kondoo humfuata kwa kuwa wanaijua sauti yake.
Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake.
5 Lakini kondoo hawatamfuata mgeni bali watamkimbia, kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.”
Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake.”
6 Yesu alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia.
Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia.
7 Kwa hiyo Yesu akasema nao tena akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo.
Basi, akasema tena, “Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo.
8 Wote walionitangulia ni wevi na wanyangʼanyi, lakini kondoo hawakuwasikia.
Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang'anyi, nao kondoo hawakuwasikiliza.
9 Mimi ndimi lango, yeyote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho.
Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho.
10 Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele.
Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima—uzima kamili.
11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.
“Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake.
12 Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Amwonapo mbwa mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya.
Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya.
13 Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.
Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu.
14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua.
Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi,
15 Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.
kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.
16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.
Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.
17 Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena.
“Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena.
18 Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”
Hakuna mtu anayeninyang'anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye.”
19 Kwa maneno haya Wayahudi waligawanyika.
Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya.
20 Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.”
Wengi wao wakasema, “Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?”
21 Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”
Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?”
22 Wakati huo ilikuwa Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu huko Yerusalemu, nao ulikuwa wakati wa majira ya baridi.
Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi.
23 Naye Yesu alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika ukumbi wa Solomoni.
Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni.
24 Wayahudi wakamkusanyikia wakamuuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo tuambie waziwazi.”
Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, “Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi.”
25 Yesu akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia.
Yesu akawajibu, “Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia.
26 Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu.
Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu.
27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata,
Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata.
28 nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu. (aiōn , aiōnios )
Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. (aiōn , aiōnios )
29 Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake.
Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.
30 Mimi na Baba yangu tu umoja.”
Mimi na Baba, tu mmoja.”
31 Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo,
Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie.
32 lakini Yesu akawaambia, “Nimewaonyesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni ipi katika hiyo mnataka kunipiga mawe?”
Yesu akawaambia, “Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?”
33 Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ingawa ni mwanadamu unajifanya kuwa Mungu.”
Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu.”
34 Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Sheria ya kwamba, ‘Nimesema kuwa, ninyi ni miungu?’
Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: Mimi nimesema, ninyi ni miungu?
35 Kama aliwaita ‘miungu,’ wale ambao neno la Mungu liliwafikia, nayo Maandiko hayawezi kutanguka,
Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima.
36 je, mwawezaje kusema kwamba yule ambaye Baba amemweka wakfu na kumtuma ulimwenguni anakufuru, kwa sababu nilisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’
Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: Unakufuru, eti kwa sababu nilisema: Mimi ni Mwana wa Mungu?
37 Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini,
Kama sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini.
38 lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ndani yake.”
Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake.”
39 Ndipo wakajaribu kumkamata kwa mara nyingine, lakini akaponyoka kutoka mikononi mwao.
Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao.
40 Akaenda tena ngʼambo ya Mto Yordani mpaka mahali pale ambapo Yohana alikuwa akibatiza hapo awali, naye akakaa huko.
Yesu akaenda tena ng'ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko.
41 Watu wengi wakamjia, nao wakawa wakisema, “Yohana hakufanya muujiza wowote, lakini kila jambo alilosema kumhusu huyu mtu ni kweli.”
Watu wengi walimwendea wakasema, “Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa.”
42 Nao wengi wakamwamini Yesu huko.
Watu wengi mahali hapo wakamwamini.