< Yohana 4 >

1 Mafarisayo wakasikia kwamba Yesu alikuwa anapata na kubatiza wanafunzi wengi zaidi kuliko Yohana,
Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane.
2 ingawa kwa kweli si Yesu mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake.
(Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.)
3 Bwana alipojua mambo haya, aliondoka Uyahudi akarudi tena Galilaya.
Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya;
4 Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria.
na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria.
5 Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yosefu.
Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu.
6 Huko ndiko kulikokuwa na kile kisima cha Yakobo. Naye Yesu alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
7 Mwanamke mmoja Msamaria akaja kuteka maji, Yesu akamwambia, “Naomba maji ninywe.”
Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, “Nipatie maji ninywe.”
8 (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)
(Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)
9 Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe nikupe maji ya kunywa?” (Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.)
Lakini huyo mwanamke akamwambia, “Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?” (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu.)
10 Yesu akajibu akamwambia, “Kama ungelijua karama ya Mungu, naye ni nani anayekuambia, Nipe maji ninywe, wewe ungelimwomba yeye, naye angelikupa maji yaliyo hai.”
Yesu akamjibu, “Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekwambia: Nipatie maji ninywe, ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yaliyo hai.”
11 Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi?
Huyo mama akasema, “Mheshimiwa, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai?
12 Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?”
Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake walikunywa maji ya kisima hiki.”
13 Yesu akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki ataona kiu tena.
Yesu akamjibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena.
14 Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele.” (aiōn g165, aiōnios g166)
Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na kumpatia uzima wa milele.” (aiōn g165, aiōnios g166)
15 Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena na wala nisije tena hapa kuteka maji!”
Huyo mwanamke akamwambia, “Mheshimiwa, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; nisije tena mpaka hapa kuteka maji.”
16 Yesu akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.”
Yesu akamwambia, “Nenda ukamwite mumeo uje naye hapa.”
17 Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume.
Huyo mwanamke akamwambia, “Mimi sina mume.” Yesu akamwambia, “Umesema kweli, kwamba huna mume.
18 Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.”
Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli.”
19 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii.
Huyo Mwanamke akamwambia, “Mheshimiwa, naona ya kuwa wewe u nabii.
20 Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.”
Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu.”
21 Yesu akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu.
Yesu akamwambia, “Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu.
22 Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi.
Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi.
23 Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta.
Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wanaoabudu kweli, watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio Baba anaotaka.
24 Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa nguvu ya Roho wake.”
25 Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Masiya (aitwaye Kristo) anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.”
Huyo mama akamwambia, “Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu.”
26 Yesu akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.”
Yesu akamwambia, “Mimi ninayesema nawe, ndiye.”
27 Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemuuliza, “Unataka nini kwake?” Au “Kwa nini unazungumza naye?”
Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: “Unataka nini?” au, “Kwa nini unaongea na mwanamke?”
28 Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini akawaambia watu,
Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu,
29 “Njooni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Kristo?”
“Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?”
30 Basi wakamiminika watu kutoka mjini wakamwendea Yesu.
Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.
31 Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Rabi, kula angalau chochote.”
Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: “Mwalimu, ule chakula.”
32 Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.”
Lakini Yesu akawaambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.”
33 Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?”
Wanafunzi wake wakaulizana, “Je, kuna mtu aliyemletea chakula?”
34 Lakini Yesu akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake.
Yesu akawaambia, “Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.
35 Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune?’ Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa!
Ninyi mwasema: Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika! Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa.
36 Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele. Ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. (aiōnios g166)
Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja. (aiōnios g166)
37 Hivyo kule kusema, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa.
Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: Mmoja hupanda na mwingine huvuna.
38 Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda, wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”
Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho, wengine walifanya kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho lao.”
39 Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Yesu kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.”
Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: “Ameniambia mambo yote niliyofanya.”
40 Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili.
Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili.
41 Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini.
Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake.
42 Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kweli ya kwamba huyu ndiye Kristo, Mwokozi wa ulimwengu.”
Wakamwambia yule mama, “Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu.”
43 Baada ya zile siku mbili, Yesu aliondoka kwenda Galilaya.
Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya.
44 (Basi Yesu mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.)
Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, “Nabii hapati heshima katika nchi yake.”
45 Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu.
Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo.
46 Hivyo Yesu akaja tena mpaka Kana ya Galilaya, kule alikokuwa amebadili maji kuwa divai. Huko kulikuwepo na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu.
Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu.
47 Huyo mtu aliposikia kwamba Yesu alikuwa amewasili Galilaya kutoka Uyahudi, alimwendea na kumwomba ili aje kumponya mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.
Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi.
48 Yesu akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”
Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!”
49 Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”
Huyo ofisa akamwambia, “Mheshimiwa, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa.”
50 Yesu akamjibu, “Enenda zako, mwanao yu hai.” Yule afisa akaamini yale maneno Yesu aliyomwambia, akaondoka akaenda zake.
Yesu akamwambia, “Nenda tu, mwanao yu mzima.” Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake.
51 Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima.
Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima.
52 Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana yapata saa saba, homa ilimwacha.”
Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, “Jana saa saba mchana, homa ilimwacha.”
53 Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati ambapo Yesu alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye pamoja na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Yesu.
Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: “Mwanao yu mzima.” Basi, yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote.
54 Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Yesu alifanya aliporudi Galilaya kutoka Uyahudi.
Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya.

< Yohana 4 >