< Wahebrania 8 >
1 Basi jambo tunalotaka kulisema ni hili: Tunaye Kuhani Mkuu ambaye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Aliye Mkuu mbinguni,
Basi, jambo muhimu katika hayo tunayosema ni hili: sisi tunaye Kuhani Mkuu wa namna hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu mbinguni.
2 yeye ahudumuye katika patakatifu, hema la kweli lililowekwa na Bwana, wala si na mwanadamu.
Yeye hutoa huduma ya Kuhani Mkuu katika Mahali Patakatifu sana, yaani ndani ya ile hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, siyo na binadamu.
3 Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe sadaka na dhabihu. Vivyo hivyo, ilikuwa jambo muhimu kwa huyu Kuhani naye awe na kitu cha kutoa.
Kila Kuhani Mkuu ameteuliwa kumtolea Mungu vipawa na dhabihu, na hivyo Kuhani Mkuu wetu lazima pia awe na kitu cha kutolea.
4 Kama angekuwa duniani, hangekuwa kuhani, kwa sababu tayari wapo watu watoao sadaka kama ilivyoelekezwa na sheria.
Kama yeye angekuwa wa hapa duninani, asingekuwa kamwe kuhani, kwani wako makuhani wengine wanaotoa sadaka kufuatana na Sheria.
5 Wanahudumu katika patakatifu palipo mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni. Hii ndiyo sababu Mose alionywa alipokaribia kujenga hema, akiambiwa: “Hakikisha kuwa unavitengeneza vitu vyote kwa mfano ulioonyeshwa kule mlimani.”
Huduma zao za kikuhani ni mfano tu na kivuli cha yale yaliyoko mbinguni. Ndivyo pia ilivyokuwa kwa Mose. Wakati alipokuwa karibu kuitengeneza ile hema, Mungu alimwambia: “Tengeneza kila kitu kufuatana na ule mfano ulioonyeshwa kule mlimani.”
6 Lakini huduma aliyopewa Yesu ni bora zaidi kuliko yao, kama vile agano ambalo yeye ni mpatanishi wake lilivyo bora zaidi kuliko lile la zamani, nalo limewekwa misingi wa ahadi zilizo bora zaidi.
Lakini sasa Yesu amepewa huduma ya kikuhani iliyo bora zaidi kuliko yao, kama vile agano alilothibitisha kati ya watu na Mungu ni bora zaidi, kwani lina msingi wake katika ahadi za mambo yaliyo bora zaidi.
7 Kwa maana kama hapakuwa na kasoro katika lile agano la kwanza, pasingekuwa na haja ya kutafuta nafasi kwa ajili ya jingine.
Maana kama lile agano la kwanza halingalikuwa na dosari, hakungalikuwa na haja ya agano la pili.
8 Lakini Mungu aliona kosa kwa watu, naye akasema: “Siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.
Lakini Mungu aliwalaumu watu wake aliposema: “Siku zinakuja, asema Bwana, ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na kabila la Yuda.
9 Agano langu halitakuwa kama lile nililofanya na baba zao nilipowashika mkono kuwaongoza watoke nchi ya Misri, kwa sababu hawakuendelea kuwa waaminifu katika agano langu, nami nikawaacha, asema Bwana.
Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao siku ile nilipowaongoza kwa mkono kutoka nchi ya Misri. Hawakuwa waaminifu kwa agano langu; na hivyo mimi sikuwajali, asema Bwana.
10 Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli baada ya siku zile, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu katika nia zao na kuziandika mioyoni mwao. Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
Na hili ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake, wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana,’ kwa sababu wote watanijua mimi, tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana.
Hakuna mtu atakayemfundisha mwananchi mwenzake, wala atakayemwambia ndugu yake: Mjue Bwana. Maana watu wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi.
12 Kwa sababu nitasamehe uovu wao, wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”
Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao.”
13 Kwa kuliita agano hili “jipya,” Mungu amefanya lile agano la kwanza kuwa kuukuu; nacho kitu kinachoanza kuchakaa na kuwa kikuukuu kiko karibu kutoweka.
Kwa kusema juu ya agano jipya, Mungu alilichakaza lile la kwanza; na chochote kinachochakaa na kuwa kikuukuu kitatoweka karibuni.