< Filemoni 1 >

1 Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, pamoja na Timotheo ndugu yetu: Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtendakazi mwenzetu,
Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu
2 kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako:
na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkupo.
3 Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana yesu Kristo.
4 Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu,
Kila wakati ninaposali nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu
5 kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote.
maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana wetu Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu.
6 Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo.
Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo.
7 Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.
Ndugu, upendo wako yameniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu.
8 Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningeweza kuwa na ujasiri na kukuagiza yale yakupasayo kutenda,
Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya.
9 lakini ninakuomba kwa upendo, mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu,
Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake.
10 nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo, aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo.
Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni.
11 Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia.
Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia.
12 Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa.
Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe.
13 Ningependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili.
Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Habari Njema.
14 Lakini sikutaka kufanya lolote bila idhini yako, ili wema wowote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari.
Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika.
15 Huenda sababu ya yeye kutengwa nawe kwa kitambo kidogo ni ili uwe naye daima. (aiōnios g166)
Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima. (aiōnios g166)
16 Si kama mtumwa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana.
Na sasa yeye si mtumwa tu, ila ni bora zaidi ya mtumwa: yeye ni ndugu yetu mpenzi. Na wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana.
17 Hivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika wako, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe.
Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe.
18 Kama amekukosea lolote au kama unamdai chochote, nidai mimi.
Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi.
19 Ni mimi Paulo, ninayeandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakulipa. Sitaji kwamba nakudai hata nafsi yako.
Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: Mimi Paulo nitalipa! (Tena sina haja ya kusema kwamba wewe unalo deni kwangu la nafsi yako.)
20 Ndugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana, uuburudishe moyo wangu katika Kristo.
Haya, basi, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo.
21 Nikiwa na hakika ya utii wako, nakuandikia, nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale ninayokuomba.
Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba.
22 Jambo moja zaidi: Niandalie chumba cha wageni, kwa kuwa nataraji kurudishwa kwenu kama jibu la maombi yenu.
Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni.
23 Epafra, aliye mfungwa mwenzangu katika Kristo Yesu, anakusalimu.
Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu.
24 Vivyo hivyo Marko, Aristarko, Dema na Luka, watendakazi wenzangu wanakusalimu.
Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu.
25 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.
Nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.

< Filemoni 1 >