< Wahebrania 4 >
1 Kwa hiyo, kwa kuwa bado ahadi ya kuingia rahani iko wazi, tujihadhari ili hata mmoja wenu asije akaikosa.
Kwa hiyo, tunapaswa kuwa makini ili kwamba kati yenu asiwepo hata mmoja atakayeonekana kushindwa kufikia ahadi endelevu ya kuingia katika pumzika la Mungu.
2 Kwa maana sisi pia tumesikia Injili iliyohubiriwa kwetu, kama nao walivyosikia; lakini ujumbe ule waliousikia haukuwa na maana kwao, kwa sababu wale waliousikia hawakuuchanganya na imani.
Kwani tumekuwa na habari njema kuhusu pumziko la Mungu lililotangazwa kwetu kama Waisrael walivyokuwa nayo, lakini ujumbe huo haukuwasaidia wale ambao waliusikia bila kuunganisha imani kwa hilo.
3 Sasa sisi ambao tumeamini tunaingia katika ile raha, kama vile Mungu alivyosema, “Kwa hiyo nikaapa katika hasira yangu, ‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’” Lakini kazi yake ilikamilika tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
Kwa sisi, ambao tumekwisha amini-sisi ndio miongoni tutakaoingia katika lile pumuziko, Kama inavyosema, “Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia katika pumziko mwangu.” Alisema hili, ingawa kazi zote alizotengeneza zilikuwa zimekamilika tangu mwanzo wa ulimwengu.
4 Kwa maana mahali fulani amezungumza kuhusu siku ya saba, akisema: “Katika siku ya saba Mungu alipumzika kutoka kazi zake zote.”
Kwani ameshasema sehemu fulani kuhusu siku ya saba, “Mungu alipumzika siku ya saba katika yote aliyoyafanya.”
5 Tena hapo juu asema, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”
Tena ameshasema, “Hawataingia kwenye pumziko langu.”
6 Kwa hiyo inabaki kuwa wazi kwa wengine kuingia, nao wale wa kwanza waliopokea Injili walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokutii.
Kwa sababu hiyo, tangu pumziko la Mungu bado ni akiba kwa ajili ya baadhi kuingia, na tangu Waisraeli wengi ambao walisikia habari njema kuhusu pumziko lake hawakuingia kwa sababu ya kutotii,
7 Kwa hiyo Mungu ameweka siku nyingine, akaiita Leo, akisema kwa kinywa cha Daudi baadaye sana, kwa maneno yaliyotangulia kunenwa: “Leo, kama mkiisikia sauti yake, msiifanye mioyo yenu migumu.”
Mungu aliweka tena siku fulani, iitwayo “Leo.” Yeye aliiongeza siku hii alipozungumza kupitia Daudi, ambaye alisema kwa muda mrefu baada ya yaliyosemwa kwanza, “Leo kama mtasikia sauti yake, msifanye mioyo yenu kuwa migumu.”
8 Kwa maana kama Yoshua alikuwa amewapa raha, Mungu hangesema tena baadaye kuhusu siku nyingine.
Kwani kama Yoshua aliwapatia pumziko, Mungu asingelisema juu ya siku nyingine.
9 Kwa hiyo basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu;
Kwa hiyo bado kuna Sabato ya pumziko iliyotunzwa kwa ajili ya watu wa Mungu.
10 kwa kuwa kila mmoja aingiaye katika raha ya Mungu pia hupumzika kutoka kazi zake mwenyewe, kama vile Mungu alivyopumzika kutoka kazi zake.
Kwani anayeingia katika pumziko la Mungu yeye mwenyewe pia amepumzika kutokana na matendo yake, kama Mungu alivyofanya katika yeye.
11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili kwamba asiwepo yeyote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.
Kwa hiyo tuweni na shauku ya kuingia katika lile pumziko, ili kwamba asiwepo atakayeanguka katika aina ya uasi waliofanya.
12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu. Lina makali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili, hivyo linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Kwa maana neno la Mungu li hai na lina nguvu na linaukali kuliko upanga wowote wenye makali kuwili. Na huchoma hata kufikia kugawanya nafsi na roho, na viungo kutika uboho. Na lenye kuweza kufahamu fikira za moyo nia yake.
13 Wala hakuna kiumbe chochote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.
. Hakuna kilichoumbwa kilichojificha katika uso wa Mungu. Badala yake, kila kitu ni dhahiri na wazi kwa macho ya mmoja ambaye ni lazima tutoe hesabu.
14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu.
Baadaye kuwa na kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu Mwana wa Mungu, kwa uimara tushikilie imani zetu.
15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi.
Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu ambaye hawezi kuhisi huruma kwa ajili udhaifu wetu, lakini yeye ambaye kwa njia zote amekuwa akijaribiwa kama sisi, isipokuwa yeye ambaye hana dhambi.
16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
Na tuje kwa ujasiri katika kiti cha enzi cha neema, ili kwamba tupokee rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa hitaji.