< Filemoni 1 >

1 Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, pamoja na Timotheo ndugu yetu: Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtendakazi mwenzetu,
Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na ndugu Timotheo kwa Filemoni, mpendwa rafiki yetu na mtenda kazi pamoja nasi,
2 kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako:
na kwa Afia dada yetu, na kwa Arkipas askari mwenzetu, na kwa kanisa lile linalokutana nyumbani kwako.
3 Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Neema iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
4 Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu,
Wakati wote namshukuru Mungu. Ninakutaja katika maombi yangu.
5 kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote.
Nimesikia upendo na imani uliyonayo katika Bwana Yesu na kwa ajili ya waumini wote.
6 Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo.
Ninaomba kwamba ushirika wa imani yenu iwe na ufanisi katika ujuzi wa kila jambo jema lililoko kati yetu katika Kristo.
7 Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.
Kwa kuwa nimekuwa na furaha na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa sababu mioyo ya waumini imekuwa ikitulizwa nawe, ndugu.
8 Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningeweza kuwa na ujasiri na kukuagiza yale yakupasayo kutenda,
Kwa hiyo, ingawa nina ujasiri wote katika Kristo kukuamuru wewe kufanya kile unachoweza kufanya,
9 lakini ninakuomba kwa upendo, mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu,
lakini kwa sababu ya upendo, badala yake nakusihi - mimi, Paulo niliye mzee, na sasa ni mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu.
10 nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo, aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo.
Ninakusihi kuhusu mwanangu Onesmo, niliyemzaa katika vifungo vyangu.
11 Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia.
Kwa kuwa mwanzoni hakukufaa, lakini sasa anakufaa wewe na mimi.
12 Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa.
Nimemtuma- yeye ambaye ni wa moyo wangu hasa - kurudi kwako.
13 Ningependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili.
Nataraji angeendelea kubaki pamoja nami, ili anitumikie badala yako, wakati niwako kifungoni kwa ajili ya injili.
14 Lakini sikutaka kufanya lolote bila idhini yako, ili wema wowote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari.
Lakini sikutaka kufanya jambo lolote bila ruhusa yako. Nilifanya hivi ili kwamba jambo lolote zuri lisifanyike kwa sababu nilikulazimisha, bali kwa sababu ulipenda mwenyewe kulitenda.
15 Huenda sababu ya yeye kutengwa nawe kwa kitambo kidogo ni ili uwe naye daima. (aiōnios g166)
Labda ni sababu alitengwa nawe kwa muda, ilikuwa hivyo ili uwe pamoja naye milele. (aiōnios g166)
16 Si kama mtumwa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana.
Ili kwamba asiwe tena mtumwa, bali bora zaidi ya mtumwa, kama ndugu mpendwa, hasa kwangu, na zaidi sana kwako, katika mwili na katika Bwana.
17 Hivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika wako, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe.
Na hivyo kama wanichukulia mimi mshirika, mpokee kama ambavyo ungenipokea mimi.
18 Kama amekukosea lolote au kama unamdai chochote, nidai mimi.
Lakini kama amekukosea jambo lolote, au unamdai kitu chochote, kidai hicho kutoka kwangu.
19 Ni mimi Paulo, ninayeandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakulipa. Sitaji kwamba nakudai hata nafsi yako.
Mimi Paulo, ninaandika kwa mkono wangu mwenyewe: mimi nitakulipa. Sisemi kwako kwamba nakudai maisha yako hasa.
20 Ndugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana, uuburudishe moyo wangu katika Kristo.
Naam ndugu, acha nipate furaha ya Bwana toka kwako: uburudishe moyo wangu katika Kristo.
21 Nikiwa na hakika ya utii wako, nakuandikia, nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale ninayokuomba.
Nikiwa na imani kuhusu utii wako, nakuandikia nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya vile ninavyokuomba.
22 Jambo moja zaidi: Niandalie chumba cha wageni, kwa kuwa nataraji kurudishwa kwenu kama jibu la maombi yenu.
Wakati huo huo andaa chumba cha wageni kwa ajili yangu, kwa kuwa ninatumaini kupitia maombi yako nitakutembelea hivi karibuni.
23 Epafra, aliye mfungwa mwenzangu katika Kristo Yesu, anakusalimu.
Epafra, mfungwa mwenzangu katika Kristo Yesu anakusalimu,
24 Vivyo hivyo Marko, Aristarko, Dema na Luka, watendakazi wenzangu wanakusalimu.
na kama afanyavyo Marko, Aristarko, Dema, Luka, watendakazi pamoja nami.
25 Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.
Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho yako. Amina.

< Filemoni 1 >