< Wahebrania 12 >

1 Kwa sababu hii, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa namna hii la mashahidi, basi na tuweke kando kila kitu kinachotuzuia na ile dhambi inayotuzinga kwa urahisi, nasi tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa kwa ajili yetu.
Kwahiyo, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa la mashaidi, na tutupe kila kitu kinacho tulemea pamoja na dhambi ambayo inatuzingira kwa urahisi. Tupige mbio kwa saburi katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu.
2 Basi na tumtazame sana Yesu mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu, yeye ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahimili msalaba, bila kujali aibu ya huo msalaba, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
Tuyaelekeze macho yetu kwa Yesu, aliye mwanzilishi na mwenye kutimiliza imani yetu, ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahmili msalaba, akiidharau aibu yake, na akakaa chini mkono wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.
3 Mtafakarini sana yeye aliyestahimili upinzani mkuu namna hii kutoka kwa watu wenye dhambi, ili kwamba msije mkachoka na kukata tamaa.
Maana mtafakarini yeye aliye stahimili maneno ya chuki kutoka kwa wenye dhambi, dhidi yake mwenyewe ili kwamba msije mkachoka au kuzimia mioyo yenu.
4 Katika kushindana kwenu dhidi ya dhambi, bado hamjapigana kiasi cha kumwaga damu yenu.
Hamjataabika au kuteseka mkishindana na dhambi kiasi cha kuishiwa damu.
5 Nanyi mmesahau yale maneno ya kuwaonya yanayowataja ninyi kuwa wana, yakisema: “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usikate tamaa akikukemea,
Tena mmesahau kule kutiwa moyo ambako kunawaelekeza kama watoto wa kiume: “Mwanangu, usiyachukuwe kwa wepesi marudia ya Bwana, wala usikate tamaa unapo rekebishwa na yeye.”
6 kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, na humwadhibu kila mmoja anayemkubali kuwa mwana.”
Kwa kuwa Bwana humrudi yeyote ambaye anampenda, na humwadhibu kila mwana ambaye humpokea.
7 Vumilieni taabu kwa ajili ya kufunzwa adabu. Mungu anawatendea ninyi kama watoto wake, kwa maana ni mtoto yupi asiyeadibishwa na mzazi wake?
Stahimili majaribu kama kurudiwa. Mungu hushughulika nanyi kama anavyoshughulika na watoto, maana ni mtoto yupi ambaye baba yake hawezi kumrudi?
8 Kama hakuna kuadibishwa (ambalo ni fungu la watoto wote), basi ninyi ni watoto wa haramu wala si watoto halali.
Lakini kama hakuna kurudiwa, ambako sisi sote tunashiriki, basi ninyi ni haramu na si watoto wake.
9 Tena, sisi sote tunao baba wa kimwili, waliotuadibisha nasi tukawaheshimu kwa ajili ya hilo. Je, si inatupasa kujinyenyekeza zaidi kwa Baba wa roho zetu ili tuishi?
Zaidi ya yote, tulikuwa na baba zetu kidunia wa kuturudi, na tuliwaheshimu. Je haitupasi hata zaidi kumtii Baba wa kiroho na kuishi?
10 Baba zetu walituadibisha kwa kitambo kidogo kama wao wenyewe walivyoona vyema, lakini Mungu hutuadibisha kwa faida yetu ili tupate kushiriki utakatifu wake.
Kwa hakika baba zetu walituadhibu kwa miaka michache kama ilivyoonekana sawa kwao, lakini Mungu hutuadhibu kwa faida yetu ili tushiriki utakatifu wake.
11 Kuadibishwa wakati wowote hakuonekani kuwa kitu cha kufurahisha bali chenye maumivu kinapotekelezwa. Lakini baadaye huzaa matunda ya haki na amani kwa wale waliofunzwa nayo.
Hakuna adhabu inayofurahisha kwa wakati huo. Huwa na maumivu. Hata hivyo, baadaye huzaa tunda la amani ya utauwa kwa wale waliofundishwa nayo.
12 Kwa hiyo, itieni nguvu mikono yenu iliyo dhaifu na magoti yenu yaliyolegea.
Kwa hiyo inueni mikono yenu iliyolegea na kufanya magoti yenu yaliyo dhaifu kuwa yenye nguvu tena;
13 Sawazisheni mapito ya miguu yenu, ili kitu kilicho kiwete kisidhoofishwe bali kiponywe.
nyosheni mapito ya nyayo zenu, ili kwamba yeyote aliye mlemavu hataongozwa upotevuni lakini apate kuponywa.
14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu, ambao bila kuwa nao hakuna mtu atakayemwona Bwana.
Tafuteni amani na watu wote, na pia utakatifu ambao bila huo hakuna atakayemwona Bwana.
15 Angalieni sana mtu yeyote asiikose neema ya Mungu na kwamba shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.
Muwe waangalifu ili kwamba asiwepo atakayetengwa mbali na neema ya Mungu, na kwamba lisije shina la uchungu litakalochipuka na kusababisha shida na kukengeusha wengi.
16 Angalieni miongoni mwenu asiwepo mwasherati au mtu asiyemcha Mungu kama Esau, ambaye kwa ajili ya mlo mmoja aliuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza.
Angalieni kuwa hakuna zinaa au mtu asiye mtauwa kama vile Esau, ambaye kwa sababu ya mlo mmoja aliuza haki yake ya kuzaliwa.
17 Baadaye kama mnavyofahamu, alipotaka kurithi ile baraka, alikataliwa, maana hakupata nafasi ya kutubu, ingawa aliitafuta kwa machozi.
Kwa kuwa mnajua kwamba baadaye, alipotamani kurithi baraka, alikataliwa, kwa sababu hakupata fursa ya kutubu pamoja na baba yake, hata ingawa alitafuta sana kwa machozi.
18 Hamjaufikia mlima ule uwezao kuguswa na ambao unawaka moto; wala kwenye giza, utusitusi na dhoruba;
Kwa kuwa hamkuja katika mlima ambao unaweza kuguswa, Mlima unaowaka moto, giza, kukatisha tamaa na dhoruba.
19 kwenye mlio wa tarumbeta, au kwenye sauti isemayo maneno ya kutisha kiasi ambacho wale walioisikia waliomba wasiambiwe neno jingine zaidi,
Hamkuja kwa sauti za tarumbeta, au kwa maneno yatokanayo na sauti ambayo ilisababisha kila wasikiao wasiombe neno lolote kusemwa kwao.
20 kwa sababu hawangeweza kustahimili neno lile lililoamriwa: “Hata kama mnyama atagusa mlima huu, atapigwa mawe.”
Kwa kuwa hawakuweza kuvumilia kile kilichoamuliwa: “Ikiwa hata mnyama agusaye mlima, lazima apigwe kwa mawe.”
21 Waliyoyaona yalikuwa ya kutisha kiasi kwamba Mose alisema, “Ninatetemeka kwa hofu.”
Ya kutisha zaidi aliyoyaona Musa alisema, “Nimeogopa sana kiasi cha kutetemeka”.
22 Lakini ninyi mmekuja Mlima Sayuni, Yerusalemu ya mbinguni, mji wa Mungu aliye hai. Mmekuja penye kusanyiko kubwa la malaika maelfu kwa maelfu wasiohesabika wanaoshangilia,
Badala yake, mmekuja mlima Sayuni na katika mji wa Mungu aliye hai, Yerualem ya mbinguni, na kwa malaika elfu kumi wanaosherehekea.
23 kwenye kanisa la wazaliwa wa kwanza wa Mungu, ambao majina yao yameandikwa mbinguni. Mmekuja kwa Mungu, mhukumu wa watu wote, kwenye roho za wenye haki waliokamilishwa,
Mmekuja katika kusanyiko la wazaliwa wa kwanza wote waliosajiliwa mbinguni, kwa Mungu hakimu wa wote, na kwa roho za watakatifu ambao wamekamilishwa.
24 kwa Yesu mpatanishi wa agano jipya, na kwa damu iliyonyunyizwa, ile inenayo mambo mema kuliko damu ya Abeli.
Mmekuja kwa Yesu mpatanishi wa agano jipya, na kwa damu iliyonyunyizwa ambayo hunena mema zaidi kuliko damu ya Habili.
25 Angalieni, msije mkamkataa yeye anenaye. Ikiwa wao hawakuepuka adhabu walipomkataa yeye aliyewaonya hapa duniani, sisi je, tutaokokaje tusipomsikiliza yeye anayetuonya kutoka mbinguni?
Angalia kuwa usije ukamkataa mmoja ambaye anenaye. Kwa kuwa kama hawakuepuka walipomkataa mmoja aliye waonya duniani, kwa hakika hatutaepuka ikiwa tutageuka mbali kutoka kwa yule atuonyaye kutoka mbinguni.
26 Wakati ule sauti yake ilitetemesha dunia, lakini sasa ameahidi, “Kwa mara moja tena nitatetemesha si nchi tu bali na mbingu pia.”
Kwa wakati huo sauti yake ilitikisa dunia. Lakini sasa ameahidi na kunena, “Bado mara nyingine tena sitatikisa dunia pekee, bali mbingu pia.”
27 Maneno haya “kwa mara moja tena” yanaonyesha kuondoshwa kwa vile vitu vinavyoweza kutetemeshwa, yaani vile vitu vilivyoumbwa, kwa kusudi vile tu visivyoweza kutetemeshwa vibaki.
Maneno haya, “Mara moja tena,” inaonesha kutoweshwa kwa vitu vile vitetemeshwavyo, hivi ni, vitu vile ambavyo vimeumbwa, ili kwamba vile vitu visivyotetemeshwa vibakie.
28 Kwa hiyo, kwa kuwa tunapokea ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa, basi na tuwe na shukrani, na hivyo tumwabudu Mungu kwa namna inayompendeza, kwa unyenyekevu na uchaji,
Kwa hiyo, tupokee ufalme ambao hautetemeshwi, tufurahi katika hali ya kumwabudu Mungu kwa kukubali pamoja na kunyenyekea katika kicho,
29 kwa kuwa “Mungu wetu ni moto ulao.”
kwa maana Mungu wetu ni moto ulao.

< Wahebrania 12 >