< Mhubiri 1 >

1 Maneno ya Mhubiri, mwana wa Daudi, mfalme huko Yerusalemu:
Haya ni maneno ya Mwalimu, mwana wa Daudi na mfalme katika Yerusalemu.
2 “Ubatili mtupu! Ubatili mtupu!” Mhubiri anasema. “Ubatili mtupu! Kila kitu ni ubatili.”
Mwalimu asema hivi, “Kama mvuke wa ukungu, kama upepo mwanana katika upepo, kila kitu hutoweka na kuacha maswali mengi.
3 Mwanadamu anafaidi nini kutokana na kazi yake yote anayotaabikia chini ya jua?
Ni faida gani wanadamu huipata kutoka katika kazi zote wazifanyazo chini ya jua?
4 Vizazi huja na vizazi hupita, lakini dunia inadumu milele.
Kizazi kimoja huenda, na kizazi kingine huja, lakini nchi yabaki milele.
5 Jua huchomoza na jua huzama, nalo huharakisha kurudi mawioni.
Jua huchomoza na jua huzama na kwenda kwa kasi, na kurudi mahali linapochomozea tena.
6 Upepo huvuma kuelekea kusini na kugeukia kaskazini, hurudia mzunguko huo huo, daima ukirudia njia yake.
Upepo huvuma kusini na huzunguka kasikazi, na mara zote ukizunguka katika njia yake na kurudi tena.
7 Mito yote hutiririka baharini, hata hivyo bahari kamwe haijai. Mahali mito inapotoka, huko hurudi tena.
Mito yote hutiririka katika bahari, lakini bahari haijai. Mahali mito inakoenda, ndiko inakoenda tena.
8 Vitu vyote vinachosha, zaidi kuliko mtu anavyoweza kusema. Jicho kamwe halitosheki kutazama, wala sikio halishibi kusikia.
Kila kitu huwa uchovu, na hakuna yeyote awezae kukielezea. Jicho halishibina kile linachokiona, wala sikio halishibi na kile linachosikia.
9 Kile kilichokuwepo kitakuwepo tena, kile kilichofanyika kitafanyika tena, hakuna kilicho kipya chini ya jua.
Chochote kilichopo ndicho kitakachokuwepo, kila kilichofanyika ndicho kitakachofanyika. Hakuna jipya chini ya jua.
10 Kuna kitu chochote ambacho mtu anaweza kusema, “Tazama! Kitu hiki ni kipya”? Kilikuwepo tangu zamani za kale, kilikuwepo kabla ya wakati wetu.
Je kuna jambo lolote ambalo watu wanaweza kusema, 'Tazama, hili ni jipya'? Chochote kilichopo kimekwisha kuwepo muda mwingi, wakati uliokuwepo kabla yetu.
11 Hakuna kumbukumbu ya watu wa zamani, hata na wale ambao hawajaja bado hawatakumbukwa na wale watakaofuata baadaye.
Hakuna anayeonekana kukumbuka kilichotokea nyakati za zamani. Na mambo yaliyo tokea siku zilizo pita na yale yatakayo tokea siku za mbele nayo hayatakumbukwa.”
12 Mimi, Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli katika Yerusalemu.
Mimi ni mwalimu, na nimekuwa mfalme juu ya Isareli katika Yerusalemu.
13 Nilitumia muda wangu wote kujifunza na kuvumbua kwa hekima yote yanayofanyika chini ya mbingu. Jinsi gani Mungu ameweka mzigo mzito juu ya wanadamu!
Nilitia akili yangu katika kusoma na kutafuta kwa hekima kila kitu kinachofanywa chini ya mbingu. Hili nalo ni jukumu zito ambalo Mungu amewapa wana wa watu kujishughulisha nalo.
14 Nimeshaona mambo yote yanayotendeka chini ya jua, hayo yote ni ubatili, hii ni kukimbiza upepo.
Nimeona matendo yote ambayo yanafanyika chini ya jua, na tazama yote ni mvuke ni kujaribu kuuchunga upepo.
15 Kilichopindika hakiwezi kunyooshwa, kile ambacho hakipo haiwezekani kukihesabu.
Palipopinda hapawezi kunyoshwa! Kisicho kuwepo hakiwezi kuhesabiwa!
16 Niliwaza mwenyewe, “Tazama, nimekua na kuongezeka katika hekima kuliko yeyote aliyewahi kutawala Yerusalemu kabla yangu. Nimekuwa na uzoefu mkubwa wa hekima na maarifa.”
Nimeuambia moyo wangu nikisema, “Tazama, nimepata hekima kubwa kuliko walioishi Yerusalemu kabla yangu. Akili yangu imeona hekima kubwa na ufahamu.”
17 Ndipo nilipojitahidi kufahamu kutofautisha hekima, wazimu na upumbavu, lakini nikatambua hata hili nalo ni kukimbiza upepo.
nimetia moyo wangu kujua hekima na upumbuvu na ujinga. Nikagundua kuwa hili nalo pia lilikuwa ni kujaribu kuuchunga upepo.
18 Kwa kuwa hekima nyingi huleta huzuni kubwa; maarifa yanapoongezeka, masikitiko yanaongezeka.
Kwa kuwa katika wingi wa hekima kuna masumbufu mengi, naye aongezae ujuzi, aongeza masikitiko.

< Mhubiri 1 >