< Torati 29 >
1 Haya ndiyo maneno ya Agano Bwana aliyomwagiza Mose kufanya na Waisraeli huko Moabu, kuwa nyongeza ya Agano alilofanya nao huko Horebu.
Haya ni maneno ambayo Yahwe alimuamuru Musa kuwaambia watu wa Israeli katika nchi ya Moabu, maneno ambayo yaliongezwa katika agano alilolifanya pamoja nao kule Horebu.
2 Mose akawaita Waisraeli wote akawaambia: Macho yenu yameona yale yote Bwana aliyofanya kwa Mfalme Farao huko Misri, kwa maafisa wake wote na kwa nchi yake yote.
Musa aliwaita Waisraeli wote na kuwaambia, “Mmeona kila kitu ambacho Yahwe alifanya mbele ya macho yenu katika nchi ya Misri kwa Farao, kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote –
3 Kwa macho yenu wenyewe mliona yale majaribu makubwa, ishara zile za miujiza na maajabu makubwa.
mateso makubwa ambayo macho yenu yaliona, ishara, pamoja na ile miujiza mikubwa.
4 Lakini mpaka leo Bwana hajawapa akili ya kuelewa au macho yanayoona au masikio yanayosikia.
Lakini mpaka leo Yahwe hajawapatia moyo wa kufahamu, macho ya kuona, au masikio ya kusikia.
5 Kwa muda wa miaka arobaini niliyowaongoza jangwani, nguo zenu hazikuchakaa, wala viatu miguuni mwenu.
Nimewaongoza kwa miaka arobaini jangwani; mavazi yenu hayakuchakaa juu yenu, na ndala zenu hazikuchakaa miguuni mwenu.
6 Hamkula mkate na hamkunywa divai wala kileo chochote. Nilifanya hivi ili mpate kujua kuwa mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
Hamkula mkate wowote, na wala hamkunywa divai yoyote au kinywaji chochote chenye ulevi, ili kwamba muweze kujua kuwa mimi ni Yahwe Mungu wenu.
7 Wakati mlipofika mahali hapa, Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani walikuja kupigana dhidi yetu, lakini tuliwashinda.
Mlipokuja mahali hapa, Sihoni, mfalme wa Heshboni, na Ogu, mfalme wa Bashani, walikuja dhidi yetu kutupiga, na tukawapiga.
8 Tuliichukua nchi yao na kuwapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kama urithi wao.
Tulichukua ardhi yao na kuwapa kama urithi Wareubeni, kwa Wagadi, na kwa nusu ya kabila ya Manase.
9 Fuateni kwa bidii masharti ya Agano hili, ili kwamba mweze kustawi katika kila kitu mnachofanya.
Kwa hiyo shikilia maneno ya agano hili na kuyatenda, ili ufanikiwe katika kila kitu ufanyacho.
10 Ninyi nyote leo mnasimama mbele za Bwana Mungu wenu; mkiwa viongozi na wakuu wenu, wazee na maafisa wenu, na wanaume wengine wote wa Israeli,
Nyie wote, mnasimama leo, mbele ya Yahwe Mungu wenu; machifu wenu, makabila yenu, wazee wenu, na maafisa wenu – wanaume wote wa Israeli,
11 pamoja na watoto wenu, wake zenu na pia wageni waishio katika kambi zenu wanaowapasulia kuni na kuwachotea maji.
watoto wenu, wake zenu, na wageni ambao wamo miongoni wa kambi yenu, kutoka kwa yule anayekata mbao zenu mpaka kwa yule atekaye maji.
12 Mnasimama hapa ili kufanya Agano na Bwana Mungu wenu, Agano ambalo Mungu analifanya nanyi siku hii ya leo na kulitia muhuri kwa kiapo,
Mpo hapa ili kwamba muingie katika agano la Yahwe Mungu wenu na katika kiapo ambacho Yahwe Mungu wako anafanya na wewe leo,
13 kuwathibitisha ninyi siku hii ya leo kama taifa lake, ili aweze kuwa Mungu wenu kama alivyowaahidi na kama alivyowaapia baba zenu Abrahamu, Isaki na Yakobo.
ili kwamba awafanye leo kuwa watu wake, na kwamba aweze kuwa Mungu kwa ajili yako, kama alivyonena kwako, na kama alivyoapa kwa mababu zako, kwa Abrahamu, kwa Isaka na kwa Yakobo.
14 Ninafanya Agano hili pamoja na kiapo chake, sio na ninyi tu
Kwa maana ninafanya agano hili na kiapo hiki sio na wewe tu –
15 mnaosimama hapa na sisi leo mbele za Bwana Mungu wetu, bali pia pamoja na wale ambao hawapo hapa leo.
pamoja kila mtu aliyesimama hapa pamoja nasi leo mbele ya Yahwe Mungu wetu – bali na wale ambao hawapo pamoja nasi leo pia.
16 Ninyi wenyewe mnajua jinsi tulivyoishi nchini Misri na jinsi tulivyopita katikati ya nchi mpaka tukafika hapa.
Unajua jinsi tulivyoishi katika nchi ya Misri, na jinsi tulivyopenya miongoni mwa mataifa ambao uliwapita.
17 Mliona miongoni mwao vinyago vyao vya kuchukiza na sanamu za miti na mawe, za fedha na dhahabu.
Mmeona sanamu zao zinazokera zilizotengenezwa kwa mbao na mawe, fedha na dhahabu, ambazo zilikuwa miongoni mwenu.
18 Hakikisheni kwamba hakuna mwanaume au mwanamke, ukoo au kabila miongoni mwenu leo ambalo moyo wake utamwacha Bwana Mungu wetu, kwenda kuabudu miungu ya mataifa hayo. Hakikisheni hakuna mzizi miongoni mwenu unaotoa sumu chungu ya namna hii.
Hakikisha hakuna kati yenu mwanamume, mwanamke, ukoo, au kabila ambaye moyo wake unamuacha Yahwe Mungu wetu leo, ili kwenda na kuabudu miungu ya mataifa hayo. Hakikisha hakuna kati yenu mzizi utakaozaa nyongo na pakanga.
19 Wakati mtu wa namna hii asikiapo maneno ya kiapo hiki, hujibariki mwenyewe na kisha hufikiri, “Nitakuwa salama, hata kama nikiendelea kuifuata njia yangu mwenyewe.” Hili litaleta maafa juu ya nchi iliyonyeshewa sawasawa na nchi kame.
Wakati mtu huyo anaposikia maneno ya laana hii, atajifariji moyoni mwake na kusema, “Nitakuwa na amani, ingawa natembea katika ukaidi wa moyo wangu”. Hii itaangamiza ubichi pamoja na ukavu.
20 Bwana kamwe hatakuwa radhi kumsamehe, ghadhabu na wivu wa Mungu vitawaka dhidi ya mtu huyo. Laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamwangukia na Bwana atafuta jina lake chini ya mbingu.
Yahwe hatamsamehe, lakini badala yake, hasira ya Yahwe na wivu wake utambanika mtu huyo, na laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki vitakuwa juu yake, na Yahwe ataliondoa jina lake kutoka mbinguni.
21 Bwana atamtwaa peke yake kutoka makabila ya Israeli kwa maangamizo, kulingana na laana zote za Agano zilizoandikwa kwenye Kitabu hiki cha Sheria.
Yahwe atamuweka kando kwa ajili ya maafa kutoka katika makabila yote ya Israeli, kwa kuzingatia laana zote za agano ambazo zimeandikwa katika kitabu hiki cha sheria.
22 Watoto wako watakaofuata baada yako katika vizazi vya baadaye na wageni ambao watakuja kutoka nchi za mbali, wataona maafa, yaliyoipata nchi na magonjwa ambayo Bwana aliyaleta juu yake.
Kizazi kifuatacho, watoto wako watakaoinuka baada yako, na mgeni atakayekuja kutoka nchi ya mbali, watazungumza watakapoona mapigo juu ya nchi hii na magonjwa ambayo Yahwe ameyafanya yawe –
23 Nchi yote itakuwa jaa linaloungua la chumvi na kiberiti: hakutakuwa kilichopandwa, hakutakuwa kinachochipua, wala hakutakuwa mimea inayoota juu yake. Itakuwa kama maangamizo ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, ambazo Bwana aliangamiza kwa hasira kali.
na watakapoona kuwa nchi yote imekuwa salfa na chumvi ichomayo, ambapo hakuna kitu kipandwacho au kuzaa matunda, ambapo hapaoti mmea wowote, kama anguko la Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, ambayo Yahwe aliangamiza katika ghadhabu na hasira yake –
24 Mataifa yote yatauliza: “Kwa nini Bwana amefanya hivi juu ya nchi hii? Kwa nini hasira hii kali ikawaka?”
watasema kwa pamoja na mataifa mengine, “Kwa nini Yahwe amefanya hili katika nchi hii? Joto ya hasira hii kali inamaanisha nini?”
25 Na jibu litakuwa: “Ni kwa sababu watu hawa waliacha Agano la Bwana, Mungu wa baba zao, Agano alilofanya nao wakati alipowatoa katika nchi ya Misri.
Kisha watu watasema, “Ni kwa sababu walitelekeza agano la Yahwe, Mungu wa mababu zao, alilofanya nao alipowatoa kutoka Misri,
26 Walienda zao na kuabudu miungu mingine na kuisujudia, miungu wasioijua, miungu ambayo Mungu hakuwapa.
na kwa sababu waliondoka na kutumikia miungu mingine na kuzisujudu, miungu ambayo hawakujiua na ambayo hakuwapatia.
27 Kwa hiyo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya nchi hii, hivyo Mungu akaleta juu yake laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki.
Kwa hiyo hasira ya Yahwe imewaka dhidi ya nchi hii, ili kuleta juu yake laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki.
28 Katika hasira kali na katika ghadhabu kuu Bwana aliwangʼoa kutoka nchi yao na kuwasukumia katika nchi nyingine, kama ilivyo sasa.”
Yahwe amewang’oa kutoka nchini kwao kwa hasira, kwa ghadhanu, na kwa ghadhabu kali, na kuwatupa katika nchi nyingine, leo.
29 Mambo ya siri ni ya Bwana Mungu wetu, bali yaliyofunuliwa ni yetu na watoto wetu milele, ili tuweze kuyafanya maneno yote ya sheria hii.
Mambo ya siri ni ya Yahwe Mungu wetu pekee; lakini mambo yaliyofichuliwa ni ya kwetu milele pamoja na wazawa wetu, ili tufanye maneno yote ya sheria hii.