< Torati 28 >
1 Kama ukimtii Bwana Mungu wako kwa bidii na kufuata amri zake zote ninazokupa leo kwa bidii, Bwana Mungu wako atakuweka juu ya mataifa yote katika dunia.
Utakaposikiliza kwa makini sauti ya Yahwe Mungu wako ili kwamba ushikilie amri zake zote ambazo nakuamuru leo, Yahwe Mungu wako atakuweka juu ya mataifa yote ya ulimwengu.
2 Baraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii Bwana Mungu wako:
Baraka hizi zote zitakuja kwako na kukupita, kama utasikiliza sauti ya Yahwe Mungu wako.
3 Utabarikiwa mjini na utabarikiwa mashambani.
Utabarikiwa ndani ya mji, na utabarikiwa shambani.
4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na mazao ya nchi yako na wanyama wako wachanga wa kufugwa, yaani ndama wa makundi yako ya ngʼombe, na wana-kondoo wa makundi yako.
Matunda ya mwili wako yatabarikiwa, na matunda ya ardhi yako, na matunda ya wanyama wako, ongezeko la ng’ombe wako, na wachanga wa mifugo wako.
5 Kapu lako na vyombo vyako vya kukandia vitabarikiwa.
Kitabarikiwa kikapu chako na chombo cha kukandia.
6 Utabarikiwa uingiapo na utabarikiwa utokapo.
Utabarikiwa utakaporudi ndani, na utabarikiwa utakapotoka nje.
7 Bwana atasababisha adui wainukao dhidi yako kushindwa mbele yako. Watakujia kwa njia moja lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.
Yahwe atasababisha maadui zako wanaoinuka dhidi yako kupigwa chini mbele yako; watajitokeza dhidi yako kwa njia moja lakini watakimbia mbele zako kwa njia saba.
8 Bwana ataagiza baraka juu ya ghala zako na juu ya kila kitu utakachogusa kwa mkono wako. Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi anayokupa.
Yahwe ataamuru baraka kuja kwako katika maghala yako na katika kila unapoweka mkono wako; atakubariki katika nchi anayokupatia.
9 Bwana atakufanya kuwa taifa lake takatifu, kama alivyokuahidi kwa kiapo, kama ukishika maagizo ya Bwana Mungu wako na kwenda katika njia zake.
Yahwe atawaimarisha kama watu waliotengwa kwa ajili yake, kama alivyoapa kwenu, iwapo mtashikilia amri za Yahwe Mungu wenu, na kutembea katika njia zake.
10 Kisha mataifa yote ya dunia wataona kuwa unaitwa kwa jina la Bwana, nao watakuogopa.
Watu wote wa ulimwengu wataona ya kwamba mmeitwa kwa jina la Yahwe, nao watawaogopa.
11 Bwana atakupa kustawi kwa wingi, katika tunda la uzao wa tumbo lako, katika wanyama wachanga wa mifugo yako na katika mazao ya ardhi yako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwapa.
Yahwe atakufanya kuwa na mafanikio sana katika matunda ya mwili wako, katika matunda ya ng’ombe zako, katika matunda ya ardhi yako, katika nchi aliyoapa kwa mababu zako kuwapatia.
12 Bwana atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa yeyote.
Yahwe atafungua kwako ghala lake la mbingu kuruhusu mvua juu ya ardhi katika muda sahihi, na kubariki kazi zote za mikono yako; utakopesha kwa mataifa mengi, lakini wewe hautakopa.
13 Bwana atakufanya kichwa, wala si mkia. Kama utazingatia maagizo ya Bwana Mungu wako ninayokupa siku hii ya leo na kuyafuata kwa bidii, daima utakuwa juu, kamwe hutakuwa chini.
Yahwe atakufanya kuwa kichwa, na sio mkia; utakuwa juu tu, na hautakuwa chini, iwapo utaisikiliza amri za Yahwe Mungu wako ambazo ninakuamuru leo, ili kuzishikilia na kuzitenda,
14 Usihalifu amri zangu zozote ninazokupa leo, kwa kwenda kuume au kushoto, kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia.
na usipogeuka kinyume na maneno yoyote ninayokuamuru leo, kulia kwako wala kushoto kwako, na kufuata miungu mingine na kuwatumikia.
15 Hata hivyo, kama hutamtii Bwana Mungu wako na kuzishika kwa bidii amri zake zote na maagizo ninayokupa leo, laana hizi zote zitakuja juu yako na kukupata:
Lakini usiposikiliza sauti ya Yahwe Mungu wako, na kushikilia amri zake zote na sheria zake ninazokuamuru leo, basi laana hizi zote zitakuja kwako na kukupita.
16 Utalaaniwa mjini na utalaaniwa mashambani.
Utalaaniwa utakapokuwa mjini, na utalaaniwa utakapokuwa shambani.
17 Kapu lako na chombo chako cha kukandia kitalaaniwa.
Kitalaaniwa kikapu chako na chombo chako cha kukandia.
18 Uzao wa tumbo lako utalaaniwa, mazao ya ardhi yako, ndama wa makundi yako ya ngʼombe na wana-kondoo wa makundi yako.
Litalaaniwa tunda la mwili wako, tunda la ardhi yako, ongezeko la ng’ombe wako, na wachanga wa mifugo.
19 Utalaaniwa uingiapo na utokapo.
Utalaaniwa utakaporudi, na utalaaniwa utokapo.
20 Bwana ataleta laana juu yako, fadhaa na kukaripiwa katika kila kitu unachokigusa kwa mkono wako, mpaka uwe umeharibiwa na kuangamizwa ghafula kwa ajili ya maovu uliyoyafanya kwa kumwacha yeye.
Yahwe atatuma laana juu yako, kuchanganyikiwa, na shutuma katika kila jambo uwekalo mikono yako, hadi utakapoangamizwa, na hadi utakapotoweka haraka kwa sababu ya matendo yako maovu ambayo utakuwa umenitelekeza mimi.
21 Bwana atakupiga kwa magonjwa mpaka akuangamize kutoka nchi unayoingia kuimiliki.
Yahwe atafanya pigo likung’ang’anie mpaka kukuangamiza kutoka katika nchi utakayoenda kumiliki.
22 Bwana atakupiga kwa magonjwa ya kudhoofisha, kwa homa na kuwashwa, hari na kwa ukame, kutu na kuwa na uchungu ambavyo vitakupiga mpaka uangamie.
Yahwe atakushambulia kwa magonjwa ya kuambukiza, kwa homa, kwa uvimbe, na kwa kiangazi na jua kali, na kwa upepo mkali na ukungu. Hivi vitakufukuza hadi uangamie.
23 Anga juu yako itakuwa shaba, na ardhi chini yako itakuwa chuma.
Mbingu zilizo juu ya vichwa vyenu zitakuwa shaba, na ardhi chini yenu itakuwa chuma.
24 Bwana atafanya mvua ya nchi yako kuwa mavumbi na mchanga; vitakujia kutoka angani mpaka uangamie.
Yahwe atafanya mvua ya ardhi yako kuwa unga na vumbi, kutoka mbinguni vitashuka kwako, hadi utakapoangamizwa.
25 Bwana atakufanya ushindwe mbele ya adui zako. Utawajia kwa njia moja lakini utawakimbia mbele yao kwa njia saba, nawe utakuwa kitu cha kuchukiza kwa falme zote za dunia.
Yahwe atakusababishia upigwe mbele ya maadui zako; utawafuata kwa njia moja dhidi yao lakini utakimbia mbele zao kwa njia saba. Utapelekwa huku na kule miongoni mwa falme za nchi.
26 Mizoga yenu itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwepo mtu yeyote wa kuwafukuza.
Mzoga wako utakuwa chakula kwa ndege wote wa angani na kwa wanyama wa ulimwengu; hakutakuwa na mtu wa kuwatisha.
27 Bwana atakupiga kwa majipu ya Misri na kwa vidonda vitokavyo usaha na kuwashwa, ambako huwezi kuponywa.
Yahwe atawashambulia na majipu ya Misri na vidonda, kiseyeye na mwasho ambazo hautapona.
28 Bwana atakupiga kwa wazimu, upofu na kuchanganyikiwa kwa akili.
Yahwe atakushambulia kwa ukichaa, kwa upofu, pamoja na kuchanganyikiwa kwa akili.
29 Wakati wa adhuhuri utapapasapapasa huku na huko kama mtu kipofu katika giza. Hutafanikiwa katika lolote ufanyalo; siku baada ya siku utaonewa na kunyangʼanywa, wala hakuna yeyote atakayekuokoa.
Utapapasa papasa mchana kama kipofu apapasavyo usiku, na hautafanikiwa katika njia zako; daima utakandamizwa na kuporwa, na hakutakuwa na mtu wa kukuokoa.
30 Utaposa mke, lakini mtu mwingine atakutana naye kimwili. Utajenga nyumba, lakini hutaishi ndani yake. Utapanda shamba la mizabibu, lakini hutakula matunda yake.
Utamchumbia mwanamke, lakini mwanamume mwingine atamkamata na kumbaka. Utajenga nyumba lakini hautaishi ndani mwake; utapanda shamba la mizabibu lakini hautafurahia matunda yake.
31 Ngʼombe wako atachinjwa mbele ya macho yako lakini hutakula nyama yake. Punda wako atachukuliwa kwa nguvu kutoka kwako wala hatarudishwa. Kondoo wako watapewa adui zako, wala hakuna mtu yeyote wa kuwaokoa.
Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, lakini hautakula nyama yake; punda wako atachukuliwa kwa nguvu mbele yako na hatarejeshwa kwako. Kondoo wako watapewa maadui zako, na hautakuwa na mtu wa kukusaidia.
32 Wanao na binti zako watatolewa kwa mataifa mengine, nawe utayachosha macho yako ukiwatazamia siku baada ya siku, hutakuwa na nguvu kuinua mkono.
Watoto wa kiume na mabinti zako watapewa kwa watu wengine; macho yako yatawatafuta siku nzima, lakini yatashindwa kwa shauku juu yao. Hakutakuwa na nguvu mikononi mwako.
33 Taifa usilolijua watakula mazao ya nchi yako na taabu ya kazi yako, hutakuwa na chochote, bali kuonewa kikatili siku zako zote.
Mavuno ya ardhi yako na ya kazi yako yote – taifa usilolijua litayatafuna; daima utaonewa na kugandamizwa,
34 Vitu utakavyoviona kwa macho yako vitakufanya wazimu.
ili upatwe na wazimu kwa yale utakayoona yakitendeka.
35 Bwana atayapiga magoti yako na miguu yako kwa majipu yenye maumivu makali yasiyoponyeka, yakienea kutoka nyayo za miguu yako hadi utosini.
Yahwe atakushambulia kwenye magoti na miguu kwa majibu makali ambayo hutaweza kupona, kutoka chini ya miguu yako mpaka juu ya kichwa chako.
36 Bwana atakupeleka wewe na mfalme uliyemweka juu yako uende kwenye taifa ambalo hukulijua wewe wala baba zako. Huko utaabudu miungu mingine, miungu ya miti na mawe.
Yahwe atawachukua pamoja na mfalme ambaye mtakuwa mmemuweka juu yenu kwa taifa ambalo hamjalijua, wala nyie au mababu zenu; kule mtaabudu miungu mingine ya mbao na mawe.
37 Utakuwa kitu cha kuchukiza, tena kitu cha kudharauliwa na kudhihakiwa kwa mataifa yote huko Bwana atakakokupeleka.
Nawe utakuwa chanzo cha kitisho, mithali, na uvumi, miongoni mwa watu wote ambako Yahwe atakupeleka.
38 Utapanda mbegu nyingi katika shamba lakini utavuna haba, kwa sababu nzige watazila.
Utaweka mbegu nyingi shambani, lakini utakusanya mbegu chache, kwa maana nzige itaziangamiza.
39 Utapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hutakunywa divai yake wala hutakusanya zabibu, kwa sababu wadudu watazila.
Utapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hautakunywa divai yoyote, wala hautakusanya matunda yoyote, kwa maana funza watayala.
40 Utakuwa na mizeituni katika nchi yako yote, lakini hutatumia hayo mafuta yake, kwa sababu zeituni zitapukutika.
Utakuwa na miti ya mizeituni katika eneo lako, lakini hautajipaka mafuta yoyote juu yako, kwa maana mti wako wa mzeituni utaangusha matunda yake.
41 Utakuwa na wana na binti lakini hawatakuwa nawe, kwa sababu watachukuliwa mateka.
Utakuwa na wana wa kiume na mabinti, lakini hawatabaki kuwa wako, kwani watachukuliwa mateka.
42 Makundi ya nzige yatavamia miti yako yote na mazao ya nchi yako.
Miti yako yote na matunda ya ardhi yako – nzige watajitwalia.
43 Mgeni anayeishi miongoni mwako atainuka juu zaidi na zaidi kuliko wewe, lakini wewe utashuka chini zaidi na zaidi.
Mgeni aliye miongoni mwako atainuka juu zaidi yako juu na juu; wewe mwenyewe utashuka chini na chini.
44 Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha. Yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia.
Atakukopesha, lakini hautamkopesha; atakuwa kichwa, nawe utakuwa mkia.
45 Laana hizi zote zitakuja juu yako. Zitakufuatia na kukupata mpaka uangamizwe, kwa sababu hukumtii Bwana Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake aliyokupa.
Laana hizi zote zitakujia juu yako na kukuandama na kukupita hadi utakapoangamizwa. Hii itatokea kwa sababu haukuisikia sauti ya Yahwe Mungu wako, ili kushikilia amri na maagizo yake aliyokuamuru.
46 Zitakuwa ishara na ajabu kwako na kwa wazao wako milele.
Laana hizi zitakuwa juu yako kama ishara na miujiza, na juu ya uzao wako milele.
47 Kwa sababu hukumtumikia Bwana Mungu wako kwa furaha na kwa moyo wakati wa kufanikiwa kwako,
Kwa sababu hukumuabudu Yahwe Mungu wako kwa shangwe na furaha moyoni mwako ulipokuwa na mafanikio,
48 kwa hiyo katika njaa na kiu, katika uchi na umaskini wa kutisha, utawatumikia adui ambao Bwana atawatuma dhidi yako. Yeye ataweka nira ya chuma shingoni mwako hadi amekwisha kukuangamiza.
kwa hiyo utatumikia maadui ambao Yahwe atatuma dhidi yako; utawatumikia katika njaa, katika kiu, katika uchi, na katika umaskini. Ataweka mzigo wa chuma juu ya shingo yako hadi akuangamize.
49 Bwana ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka miisho ya dunia, kama tai ashukiavyo mawindo chini, taifa ambalo hutaijua lugha yake,
Yahwe ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka mwisho wa ulimwengu, kama tai arukaye kwa mhanga wake, taifa ambalo lugha yake hauelewi;
50 taifa lenye uso mkali lisilojali wazee wala kuwahurumia vijana.
taifa lenye sura katili ambalo haliheshimu wazee na halionyeshi fadhila kwa wadogo.
51 Watakula wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako mpaka umeangamia. Hawatakuachia nafaka, divai mpya au mafuta, wala ndama wowote wa kundi lako au wana-kondoo wa kundi lako mpaka umekuwa magofu.
Watakula wachanga wa ng’ombe wako na matunda ya ardhi yako hadi utakapoangamizwa. Hawatawaachia nafaka, divai mpya, au mafuta, wachanga wa ng’ombe au mifugo yako, hadi watakaposababisha kutoweka kwako.
52 Nao wataizingira miji yote katika nchi yako mpaka kuta ndefu za ngome ambazo unazitegemea zimeanguka. Watazingira miji yote katika nchi ambayo Bwana Mungu wako anakupa.
Watawazingira katika malango ya miji yenu, hadi kuta zenu ndefu na imara zitakaposhuka chini ardhini, kuta ambazo mliziamini. Watawazingira ndani ya malango ya miji yenu kotekote katika nchi ambayo Yahwe Mungu wenu amewapatia.
53 Utakula uzao wa tumbo lako, nyama ya wana wako na binti zako ambao Bwana Mungu wako amekupa, kwa sababu ya mateso yale adui zako watakayokuletea wakati wa kukuzingira.
Utakula tunda la mwili wako mwenyewe, nyama ya watoto wa kiume na binti zako, ambao Yahwe Mungu wako aliwapatia, katika uvamizi na katika dhiki ambayo adui zako wataweka juu yako.
54 Hata yule mtu muungwana sana na makini miongoni mwako hatakuwa na huruma kwa ndugu yake mwenyewe au kwa mke ampendaye au watoto wake waliosalia,
Mwanamume laini na mlegevu miongoni mwenu – atakuwa na wivu kwa kaka yake na kwa mkewe, na kwa watoto wowote waliosalia.
55 naye hatampa hata mmoja wao nyama ya watoto wake ambao anawala. Kwa kuwa hakuna kitu kingine kilichosalia kwake katika mazingirwa makali ambayo adui yako watakuletea kwa miji yako yote.
Kwa hiyo hatawapatia kati yao nyama ya watoto wake ambayo ataenda kuila, kwa sababu hatabakiwa na chochote katika uvamizi na dhiki ambayo adui yako ataiweka juu yako ndani ya malango yote ya mji wako.
56 Mwanamke ambaye ni muungwana sana na makini miongoni mwako, yaani ambaye ni makini sana na muungwana kiasi kwamba asingethubutu kugusa ardhi kwa wayo wa mguu wake, yeye atakuwa mchoyo kwa mume ampendaye na mwanawe mwenyewe au binti yake,
Mwanamke laini na mlegevu miongoni mwenu, ambaye hatadiriki kuweka tako la mguu wake ardhini kwa sababu ya ulaini na maringo yake – atakuwa na wivu kwa mume kipenzi wake mwenyewe, kwa mtoto wake wa kiume, na kwa binti yake,
57 kondoo wa nyuma kutoka kwenye tumbo lake na watoto anaowazaa. Kwa kuwa anakusudia kuwala kwa siri wakati wa kuzingirwa na katika taabu zile ambazo adui yako atazileta juu yako na miji yako.
na kwa mtoto wake mchanga atakayetoka katikati ya miguu yake, na kwa watoto atakayewazaa. Atawala kwa siri kwa kukosa kitu kingine, katika uvamizi na dhiki ambayo adui yako ataweka juu yako ndani ya malango ya mji wako.
58 Kama hutafuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii, ambayo yameandikwa katika kitabu hiki na kama hutalicha hili jina la fahari na la kutisha, yaani la Bwana Mungu wako,
Iwapo hautashika maneno yote ya sheria yaliyoandikwa katika kitabu hiki, ili kuheshimu jina hili tukufu na la kutisha, Yahwe Mungu wako,
59 Bwana ataleta mapigo ya kutisha juu yako na kwa wazao wako, maafa makali na ya kudumu, magonjwa mazito na ya kudumu.
basi Yahwe atafanya mapigo yako kuwa ya kutisha, na yale ya wazao wako; yatakuwa mapigo makuu, ya muda mrefu, na magonjwa makali, ya muda mrefu.
60 Atakuletea juu yako magonjwa yote ya Misri yale uliyoyaogopa, nayo yataambatana nawe.
Ataleta juu yako mara nyingine magonjwa yote ya Misri ambayo ulikuwa unayaogopa; yatakung’ang’ania.
61 Pia Bwana atakuletea kila aina ya ugonjwa na maafa ambayo hayakuandikwa humu katika kitabu hiki cha sheria, mpaka utakapokuwa umeangamizwa.
Pia kila gonjwa na pigo ambalo halijaandikwa katika kitabu cha sheria hii, hayo pia Yahwe atayaleta juu yako hadi utakapoangamizwa.
62 Ninyi ambao mlikuwa wengi kama nyota za angani mtaachwa wachache tu, kwa sababu hamkumtii Bwana Mungu wenu.
Utabaki wachache kwa idadi, ingawa ulikuwa kama nyota wa mbinguni kwa idadi, kwa sababu haukuisikiliza sauti ya Yawhe Mungu wako.
63 Kama ilivyompendeza Bwana kuwafanya ninyi mstawi na kuongezeka kwa idadi, ndivyo itakavyompendeza kuwaharibu na kuwaangamiza ninyi. Mtangʼolewa kutoka nchi mnayoiingia kuimiliki.
Kama vile hapo awali Yawhe alivyofurahia juu yako na kutenda mema, na kuwazidisha, basi atafurahia juu yako kwa kufanya upotee na kwa kukuangamiza. Utang’olewa katika nchi utakayoenda kuimiliki.
64 Kisha Bwana atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka mwisho mmoja wa dunia hadi mwingine. Huko mtaabudu miungu mingine, miungu ya miti na ya mawe, ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua.
Yahwe atakusambaza miongoni mwa watu wote kutoka mwisho mmoja wa dunia hadi mwisho mwingine wa dunia; huko utaabudu miungu mingine ambayo hujawajua, wewe wala mababu zako, miungu ya mbao na jiwe.
65 Miongoni mwa mataifa hayo hamtapata raha wala mahali pa kupumzisha wayo wa mguu wenu. Huko Bwana atawapa mahangaiko ya mawazo, macho yaliyochoka kwa kungojea na moyo uliokata tamaa.
Miongoni mwa mataifa haya hautapata utulivu, na hakutakuwa na pumziko chini ya miguu yako; badala yake, Yahwe atakupatia huko moyo wa kutetemeka, macho yanayofeli na nafsi inayoomboleza.
66 Utaishi katika mahangaiko siku zote, ukiwa umejaa hofu usiku na mchana, wala hutakuwa kamwe na uhakika wa maisha yako.
Maisha yako yataning’inia kwa mashaka mbele yako; utaogopa kila usiku na mchana na hutakuwa na uhakika kabisa maishani mwako.
67 Wakati wa asubuhi utasema hivi, “Laiti ingekuwa jioni!” Jioni utasema, “Laiti ingekuwa asubuhi,” kwa sababu ya hofu ile itakayojaza moyo wako na vitu vile macho yako yatakavyoviona.
Asubuhi utasema, “Natamani ingekuwa jioni!” na jioni utasema, “Natamani ingekuwa asubuhi!” kwa sababu ya hofu mioyoni mwenu na vitu ambavyo macho yako italazimu kuona.
68 Bwana atawarudisha tena Misri kwa meli, safari niliyosema kamwe hamngeenda tena. Huko mtajiuza ninyi wenyewe kwa adui zenu kama watumwa wa kiume na wa kike, lakini hakuna yeyote atakayewanunua.
Yahwe atakuleta Misri mara nyingine kwa meli, kwa njia ambayo nilikuambia, “Hutaiona Misri tena”. Kule utajitoa kuuzwa kwa maadui zako kama watumwa wa kiume na kike, lakini hakutakuwa na mtu wa kuwanunua.