< 1 Wafalme 10 >

1 Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni na uhusiano wake na jina la Bwana, akaja kumjaribu kwa maswali magumu.
Malkia wa Sheba aliposikia uvumi wa Sulemani kuhusu jina la BWANA, alikuja kumjaribu kwa maswali magumu.
2 Alifika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana: pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani; alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake.
Alikuja Yerusalemu na msafara mrefu, pamoja na ngamia waliokuwa wamebeba mizigo ya manukato, dhahabu nyingi, na mawe mengi ya thamani, akamwambia Sulemani yote yaliyokuwa moyoni mwake.
3 Solomoni akamjibu maswali yake yote, hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwa mfalme asiweze kumwelezea.
Sulemani akajibu maswali yake yote. Hapakuwepo na swali ambalo aliuliza na mfalme akashindwa kujibu.
4 Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga,
Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na ikulu aliyokuwa amejenga,
5 chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika hekalu la Bwana, alipatwa na mshangao.
chakula cha mezani kwake, kuketi kwa watumishi wake, kazi ya watumishi wake na kuvaa kwao, pia wanyweshaji wake, na jinsi alivyotoa sadaka za kuteketezwa katika nyumba ya BWANA, roho yake ilizimia.
6 Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli.
Akamwambia mfalme, “Ni kweli, ile taarifa ambayo nimeisikia nchini kwangu juu ya maneno yako na hekima yako.
7 Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia.
Sikuamini kile nilichosikia hadi nilipofika hapa, na sasa macho yangu yamejionea. Hata nusu ya hekima na utajiri wako! Umezidi uvumi ambao nilikuwa nimesikia.
8 Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wasimamao mbele yako daima na kusikia hekima yako!
Tazama jinsi walivyobarikiwa wake zako, na jinsi walivyobarikwa watumishi wako ambao daima husimama mbele yako, kwa sababu wanasikia hekima zako.
9 Ahimidiwe Bwana Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka juu ya kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wake Bwana wa milele ajili ya Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.”
BWANA, Mungu wako asifiwe, ambaye amependezwa na wewe, ambaye alikuweka kwenye kiti cha enzi cha Israeli. Kwa sababu BWANA aliipenda Israeli milele, na sasa amekufanya wewe kuwa mfalme, ili kwamba utoe hukumu ya kweli na ya haki.
10 Naye akampa mfalme talanta 120 za dhahabu, kiasi kikubwa sana cha vikolezi na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa tena vikolezi vingi hivyo kuletwa kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Solomoni.
Basi Malikia alimpatia mfalme zaidi ya kilo 4500 za dhahabu na kiasi kikubwa cha mawe ya thamani. Hapakuwahi kutokea kiasi kikubwa cha viungo kama hiki ambacho Malkia wa Sheba alitoa kwa mfalme Sulemani kuwahi kutolewa tena.
11 (Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena kutoka huko zilileta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani.
Ile merikebu ya Hiramu, ambayo ilileta dhahabu kutoka Ofri, pia ilileta Kutoka Ofri kiasi kikubwa cha miti ya msandali na vito vya thamani.
12 Mfalme akatumia miti ya msandali kuwa nguzo ya Hekalu la Bwana na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa au kuonekana humo tangu siku ile.)
Mfalme alitengeneza nguzo za hekalu kwa ajili ya hekalu la BWANA na kwa nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda kwa hao waimbaji. haijatokea kiasi cha miti ya misandali kama hicho ambacho kimewahi kutokea hadi leo.
13 Mfalme Solomoni akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, kando na vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
Mfame Sulemani alimpatia Malkia wa Sheba kila kitu ambacho alihitaji, na kila kitu alichoomba, na zaidi ya yote Sulemani alimpatia kwa ukarimu wake vitu vya kifalme. Kisha akarudi kwake na watumishi wake.
14 Uzito wa dhahabu ambayo Solomoni alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666,
Kiasi cha dhahabu ambazo zililetwa kwa Sulemani kwa mwaka mmoja kilikuwa takribani kilo elfu ishirini na tatu za dhahabu,
15 mbali na mapato kutoka kwa wafanyabiashara na wachuuzi, na kutoka kwa wafalme wote wa Kiarabu na watawala wa nchi.
zaidi ya dhahabu ambazo wafanya biashara na wachuuzi walileta. Wafame wote wa Uarabuni na maliwali wa nchi pia walileta dhahabu na fedha kwa Sulemani.
16 Mfalme Solomoni akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli 600
Mfalme Sulemani alitengeneza ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa, shekeli mia sita za dhahabu zilichukuliwa pamoja na ngao.
17 Akatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.
Pia alitengeneza ngao mia tatu za dhahabu iliyofuliwa. Mane tatu za dhahabu ziliambatana pamoja na ngao moja moja; mfalme aliviweka katika ikulu ya mwitu ya Lebanoni.
18 Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi.
Kisha mfalme akafanya kiti kikubwa cha enzi kwa pembe na akakisakafia kwa dhahabu laini.
19 Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na egemeo la nyuma lilikuwa la mviringo kwa juu. Pande zote za kiti kulikuwa na mahali pa kuegemeza mikono, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.
Hicho kiti kilikuwa na ngazi sita, na kitako chake kilikuwa cha mviringo. Na kilikuwa kimezungushiwa kwa mikono pande zake zote. Na simba wawili walisimama pembeni mwa ile mikono.
20 Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote.
Kulikuwa na simba kumi na wawili waliokuwa wamesimama kwenye ile ngazi. Moja katika kila upande wa ngazi hizo. Hapakuwepo na kiti kama hicho katika ufalme mwingine.
21 Vikombe vyote vya Mfalme Solomoni vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo siku za Solomoni.
Vikombe vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu. Na vikombe vyote vya kunywea vya ikulu ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hapakuwepo na kikombe cha fedha, kwa sababu fedha haikuwa na thamani katika siku za Sulemani.
22 Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara baharini zilizokuwa zikiandamana na meli za Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo.
Mfalme alikuwa na merikebu za kusafiri pamoja na merikebu za Hiramu. Mara moja kila mwaka merikebu zilileta dhahabu, fedha, na pembe za ndovu, pamoja na nyani na tumbili.
23 Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia.
Kwa hiyo mfalme Sulemani aliwazidi wafalme wote ulimwenguni katika utajiri n a hekiima.
24 Dunia yote ikatafuta kukutana na Solomoni ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake.
Dunia yote ilitafuta uwepo wa Sulemani ili kusikia hekima yake, ambayo Mungu alikuwa ameweka katika moyo wake.
25 Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja alileta zawadi: vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu.
Na wote waliomtembelea walilipa Kodi, vyombo vya fedha na vya dhahabu, na nguo na manukato na silaha na farasi na nyumbu, mwaka baada ya mwaka.
26 Solomoni akakusanya magari ya vita na farasi. Alikuwa na magari 1,400 na farasi 12,000, ambayo aliyaweka katika miji ya magari na mengine akawa nayo huko Yerusalemu.
Sulemani alikusanya pamoja magari n a wapanda farasi. Alikuwa na magari 1, 400 na wapanda farasi elfu kumi na mbili ambao alikuwa amewaweka kwenye miji ya magari pamoja naye Yerusalemu.
27 Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu vilimani.
Mfalme alikuwa na fedha kule Yerusalemu, pamoja na mawe ardhini. Alitengeneza miti ya mierezi kuwa mingi kama mikuyu iliyo katika nyanda za chini.
28 Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka Kue. Wafanyabiashara wa mfalme waliwanunua kutoka Kue.
Sulemani alimiliiki farasi waliokuwa wamenunuliwa kutoka Misri na Kilikia. Wachuuzi wa mfalme waliwanunua kwa makundi, kila kundi kwa bei yake.
29 Waliagiza magari kutoka Misri kwa bei ya shekeli 600 za fedha na farasi kwa shekeli 150. Pia waliwauza nje kwa wafalme wote wa Wahiti na wa Waaramu.
Magari yalinunuliwa kutoka Misri kwa shekeli mia sita za fedha kila moja, na farasi kwa shekeli 150 kila moja. Vitu vingi katika hivi baadaye viliuzwa kwa wafalme wote wa Wahiti na Aramu.

< 1 Wafalme 10 >