< Warumi 15 >
1 Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu.
2 Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani.
3 Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.”
4 Maana yote yalioandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na Maandiko hayo Matakatifu tupate kuwa na matumaini.
5 Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni ninyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu,
6 ili ninyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
7 Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni.
8 Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonyesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia;
9 ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Kwa sababu hiyo, nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako.”
10 Tena Maandiko yasema: “Furahini, enyi watu wa mataifa; furahini pamoja na watu wake.”
11 Na tena: “Enyi mataifa yote, msifuni Bwana; enyi watu wote, msifuni.”
12 Tena Isaya asema: “Atatokea mtu katika ukoo wa Yese, naye atawatawala watu wa mataifa; nao watamtumainia.”
13 Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
14 Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba ninyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana ninyi kwa ninyi.
15 Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu
16 ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, dhabihu iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.
17 Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu.
18 Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo,
19 kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo.
20 Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.
21 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Watu wote ambao hawakuambiwa habari zote wataona; nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.”
22 Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu.
23 Lakini maadam sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu,
24 natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi.
25 Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalem.
26 Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoka mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalem.
27 Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia.
28 Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni ninyi nikiwa safarini kwenda Spania.
29 Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo.
30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa ajili ya upendo uletwao na Roho, mniunge mkono kwa kuniombea kwa Mungu.
31 Ombeni nipate kutoka salama miongoni mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, nayo huduma yangu huko Yerusalem ipate kukubaliwa na watu wa Mungu walioko huko.
32 Hivyo, Mungu akipenda, nitaweza kuja kwenu na moyo wa furaha, nikapumzike pamoja nanyi.
33 Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina!