< Ufunuo 7 >
1 Baada ya hayo nikawaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za dunia wakishika pepo nne za dunia ili upepo usivume hata kidogo: wala katika nchi, wala baharini, wala kwenye miti.
Baada ya hili nikaona malaika wanne wakiwa wamesimama katika pembe nne za dunia, wakizuia hizo pepo nne za dunia, ili kwamba pasiwe na upepo utakaovuma juu ya nchi au juu ya bahari au juu ya mti wowote.
2 Kisha nikamwona malaika mwingine akipanda juu kutoka mashariki akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai. Akapaaza sauti na kuwaambia hao malaika wanne waliokabidhiwa jukumu la kuiharibu nchi na bahari,
Nikaona malaika mwingine akipanda kutoka mawio ya jua akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akawaita kwa sauti kubwa wale malaika wanne waliokuwa wamepewa mamlaka ya kuidhuru nchi na bahari, akisema,
3 “Msiharibu nchi, wala bahari, wala miti, mpaka tutakapokwisha wapiga mhuri watumishi wa Mungu wetu katika paji la uso.”
“Msiidhuru nchi wala bahari, wala miti, hadi tuwe tumetia muhuri kwenye vipaji vya nyuso za watumishi wa Mungu wetu.”
4 Kisha nikasikia idadi ya hao waliopigwa mhuri: Watu mia moja arobaini na nne elfu wa makabila yote ya watu wa Israeli.
Ndipo nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri: yaani 144,000 kutoka makabila yote ya Israeli.
5 Kabila la Yuda walikuwa watu kumi na mbili elfu; kabila la Reubeni, kumi na mbili elfu, kabila la Gadi, kumi na mbili elfu;
Kutoka kabila la Yuda 12,000 walitiwa muhuri, kutoka kabila la Reubeni 12,000, kutoka kabila la Gadi 12,000,
6 Kabila la Asheri, kumi na mbili elfu; kabila la Naftali, kumi na mbili elfu; kabila la Manase, kumi na mbili elfu;
kutoka kabila la Asheri 12,000, kutoka kabila la Naftali 12,000, kutoka kabila la Manase 12,000,
7 kabila la Simeoni, kumi na mbili elfu, kabila la Lawi, kumi na mbili elfu, kabila la Isakari, kumi na mbili elfu;
kutoka kabila la Simeoni 12,000, kutoka kabila la Lawi 12,000, kutoka kabila la Isakari 12,000,
8 kabila la Zabuloni, kumi na mbili elfu; kabila la Yosefu, kumi na mbili elfu, na kabila la Benyamini, kumi na mbili elfu.
kutoka kabila la Zabuloni 12,000, kutoka kabila la Yosefu 12,000, na kutoka kabila la Benyamini 12,000.
9 Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wakiwa wamevaa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao.
Baada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna yeyote awezaye kuuhesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao.
10 Wakapaaza sauti: “Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!”
Nao walikuwa wakipiga kelele kwa sauti kubwa wakisema: “Wokovu una Mungu wetu, yeye aketiye kwenye kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo!”
11 Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na vile viumbe hai vinne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu,
Malaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu,
12 wakisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!” (aiōn )
wakisema: “Amen! Sifa na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu viwe kwa Mungu wetu milele na milele. Amen!” (aiōn )
13 Mmoja wa hao wazee akaniuliza, “Hawa waliovaa mavazi meupe ni watu gani? Na wametoka wapi?”
Kisha mmoja wa wale wazee ishirini na wanne akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”
14 Nami nikamjibu, “Mheshimiwa, wewe wajua!” Naye akaniambia, “Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa.
Nikamjibu, “Bwana, wewe wajua.” Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa.
15 Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika Hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda.
Kwa hiyo, “Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na kumtumikia usiku na mchana katika hekalu lake; naye aketiye katika kile kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao.
16 Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena,
Kamwe hawataona njaa wala kiu tena. Jua halitawapiga wala joto lolote liunguzalo.
17 kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.”
Kwa maana Mwana-Kondoo aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi atakuwa Mchungaji wao; naye atawaongoza kwenda kwenye chemchemi za maji yaliyo hai. Naye Mungu atafuta kila chozi kutoka macho yao.”