< Ufunuo 7 >
1 Baada ya hayo nikawaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za dunia wakishika pepo nne za dunia ili upepo usivume hata kidogo: wala katika nchi, wala baharini, wala kwenye miti.
2 Kisha nikamwona malaika mwingine akipanda juu kutoka mashariki akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai. Akapaaza sauti na kuwaambia hao malaika wanne waliokabidhiwa jukumu la kuiharibu nchi na bahari,
3 “Msiharibu nchi, wala bahari, wala miti, mpaka tutakapokwisha wapiga mhuri watumishi wa Mungu wetu katika paji la uso.”
4 Kisha nikasikia idadi ya hao waliopigwa mhuri: Watu mia moja arobaini na nne elfu wa makabila yote ya watu wa Israeli.
5 Kabila la Yuda walikuwa watu kumi na mbili elfu; kabila la Reubeni, kumi na mbili elfu, kabila la Gadi, kumi na mbili elfu;
6 Kabila la Asheri, kumi na mbili elfu; kabila la Naftali, kumi na mbili elfu; kabila la Manase, kumi na mbili elfu;
7 kabila la Simeoni, kumi na mbili elfu, kabila la Lawi, kumi na mbili elfu, kabila la Isakari, kumi na mbili elfu;
8 kabila la Zabuloni, kumi na mbili elfu; kabila la Yosefu, kumi na mbili elfu, na kabila la Benyamini, kumi na mbili elfu.
9 Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wakiwa wamevaa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao.
10 Wakapaaza sauti: “Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!”
11 Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na vile viumbe hai vinne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu,
12 wakisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!” (aiōn )
13 Mmoja wa hao wazee akaniuliza, “Hawa waliovaa mavazi meupe ni watu gani? Na wametoka wapi?”
14 Nami nikamjibu, “Mheshimiwa, wewe wajua!” Naye akaniambia, “Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa.
15 Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika Hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda.
16 Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena,
17 kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.”