< Ufunuo 3 >
1 “Kwa malaika wa kanisa la Sarde andika hivi: “Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye na roho saba za Mungu na nyota saba. Nayajua mambo yako yote; najua unajulikana kuwa na uhai kumbe umekufa!
2 Amka! Imarisha chochote chema kilichokubakia kabla nacho hakijatoweka kabisa. Maana, mpaka sasa, sijayaona matendo yako kuwa ni makamilifu mbele ya Mungu wangu.
3 Kumbuka, basi, yale uliyofundishwa na jinsi ulivyoyasikia, uyatii na ubadili nia yako mbaya. Usipokesha nitakujia ghafla kama mwizi, na wala hutaijua saa nitakapokujia.
4 Lakini wako wachache huko Sarde ambao hawakuyachafua mavazi yao. Hao wanastahili kutembea pamoja nami wakiwa wamevaa mavazi meupe.
5 “Wale wanaoshinda, watavikwa mavazi meupe kama hao. Nami sitayafuta majina yao kutoka katika kitabu cha uzima; tena nitawakiri kwamba ni wangu mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika wake.
6 “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!
7 “Kwa malaika wa kanisa la Filadelfia andika hivi: “Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye mtakatifu na wa kweli, ambaye anao ule ufunguo wa Daudi, na ambaye hufungua na hakuna mtu awezaye kufungua.
8 Nayajua mambo yako yote! Sasa, nimefungua mbele yako mlango ambao hakuna mtu awezaye kuufunga; najua kwamba ingawa huna nguvu sana, hata hivyo, umezishika amri zangu, umelitii neno langu wala hukulikana jina langu.
9 Sikiliza! Nitawapeleka kwako watu wa kundi lake Shetani, watu ambao hujisema kuwa ni Wayahudi, kumbe ni wadanganyifu. Naam, nitawapeleka kwako na kuwafanya wapige magoti mbele yako wapate kujua kwamba kweli nakupenda wewe.
10 Kwa kuwa wewe umezingatia agizo langu la kuwa na uvumilivu, nami pia nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia ulimwengu mzima kuwajaribu wote wanaoishi duniani.
11 Naja kwako upesi! Linda, basi, ulicho nacho sasa, ili usije ukanyang'anywa na mtu yeyote taji yako ya ushindi.
12 “Wale wanaoshinda nitawafanya wawe minara katika Hekalu la Mungu wangu, na hawatatoka humo kamwe. Pia nitaandika juu yao jina la Mungu wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani Yerusalemu mpya, mji ambao utashuka kutoka juu mbinguni kwa Mungu wangu. Tena nitaandika juu yao jina langu jipya.
13 “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!
14 “Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi: “Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aitwaye Amina. Yeye ni shahidi mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba Mungu.
15 Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: baridi au moto.
16 Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto, nitakutapika!
17 Wewe unajisema, Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina haja ya kitu chochote. Kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji kuhurumiwa, maskini, kipofu tena uko uchi!
18 Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto upate kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona.
19 Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote ninayempenda. Kwa hiyo kaza moyo, achana na dhambi zako.
20 Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami.
21 “Wale wanaoshinda nitawaketisha pamoja nami juu ya kiti changu cha enzi, kama vile mimi mwenyewe nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi.
22 “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!”