< Ufunuo 22 +
1 Kisha malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima maangavu kama kioo yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo.
Kisha malaika akanionesha mto wa maji ya uzima, maji yalikuwa ya mng'ao kama wa bilauri. Yalikuwa yakitiririka kutoka katika kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana Kondoo
2 Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uzima unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa.
Kupitia katikati ya mtaa wa mji. Katika kila pembe ya mto palikuwa na mti wa uzima, unaozaa aina kumi na mbili za matunda, na huzaa matunda kila mwezi. Majani ya mti ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa.
3 Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu.
Wala hapatakuwa na laana yoyote tena. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana Kondoo kitakuwemo ndani ya mji, na watumishi wake watamtumikia.
4 Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao.
Watamuona uso wake, na jina lake litakuwa juu ya vipaji vya nyuso zao.
5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele. (aiōn )
Hapatakuwa na usiku tena; wala hapatakuwa na hitaji la mwanga wa taa au jua kwa sababu Bwana Mungu ataangaza juu yao. Nao watatawala milele na milele. (aiōn )
6 Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde.
Malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kuaminika na kweli. Bwana Mungu wa roho za manabii alimtuma malaika wake kuwaonesha watumishi wake kitakachotokea hivi karibuni.”
7 “Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.”
“Tazama! Ninakuja upesi! Amebarikiwa yeye anayeyatii maneno ya unabii wa kitabu hiki.”
8 Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionyesha mambo hayo, nikataka kumwabudu.
Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuona mambo haya. Nilipoyasikia na kuyaona, nilianguka chini mwenyewe mbele ya miguu ya malaika kumwabudu, malaika aliyenionesha mambo haya.
9 Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!”
Akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi mwenzako, pamoja na ndugu zako manabii, pamoja na wale wanaotii maneno ya kitabu hiki. Mwabudu Mungu!”
10 Tena akaniambia, “Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia.
Akaniambia, “Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, maana wakati umekaribia.
11 Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu.”
Asiye mwenye haki, aendelee kutokuwa mwenye haki. Ambaye ni mchafu kimaadili, na aendelee kuwa mchafu kimaadili. Mwenye haki, na aendelee kuwa mwenye haki. Aliye mtakatifu, na aendelee kuwa mtakatifu.”
12 “Sikiliza!” Asema Yesu, “Naja upesi, pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake.
“Tazama! Naja upesi. Ujira wangu uko pamoja nami, kumlipa kila mmoja kulingana na alichokifanya.
13 Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wa kwanza na wa mwisho.”
Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
14 Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, kwani watakuwa na haki ya kula tunda la mti wa uzima, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake.
Wamebarikiwa wale waoshao mavazi yao ili kwamba wapate haki ya kula kutoka katika mti wa uzima na kuuingia mji kupitia malangoni.
15 Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji.
Nje kuna mbwa, wachawi, wazinzi, wauwaji, waabudu sanamu, na kila apendaye na ashuhudiaye ushahidi wa uongo.
16 “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!”
Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia kuhusu mambo haya kwa makanisa. Mimi ni mzizi wa uzao wa Daudi, Nyota ya Asubuhi ing'aayo.”
17 Roho na Bibiarusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na aseme, “Njoo!” Kisha, yeyote aliye na kiu na aje; anayetaka maji ya uzima na apokee bila malipo yoyote.
Roho na Bibi harusi asema, “Njoo!” Na yeye asikiaye aseme, “Njoo!” Yeyote aliye na kiu, na aje, na yeyote anayetamani, na apate maji ya uzima bure.
18 Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
Namshuhudia kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Kama yeyote ataongeza katika hayo, Mungu atamuongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
19 Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang'anya sehemu yake katika ule mti wa uzima, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki.
Kama mtu yeyote atayaondoa maneno ya kitabu hiki cha unabii, Mungu ataondoa sehemu yake katika mti wa uzima na katika mji mtakatifu, ambayo habari zake zimeandikwa ndani ya kitabu hiki.
20 Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: “Naam! Naja upesi.” Amina. Na iwe hivyo! Njoo Bwana Yesu!
Yeye ashuhudiaye mambo haya asema, “Ndiyo! Naja upesi.” Amina! Njoo, Bwana Yesu!
21 Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amen.
Neema ya Bwana Yesu iwe na kila mtu. Amina.