< Ufunuo 14 >
1 Kisha nikaona mlima Sioni, na Mwanakondoo amesimama juu yake; pamoja naye walikuwa watu mia moja arobaini na nne elfu ambao juu ya paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake.
Kisha nikatazama na hapo mbele yangu alikuwepo Mwana-Kondoo, akiwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale 144,000 wenye Jina la Mwana-Kondoo na Jina la Baba yake likiwa limeandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao.
2 Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama sauti ya maji mengi na kama sauti ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao.
Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kwa kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao.
3 Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu mia moja arobaini na nne elfu waliokombolewa duniani.
Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao 144,000 waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani.
4 Watu hao ndio wale waliojiweka safi kwa kutoonana kimwili na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako. Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo.
Hawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.
5 Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote.
Vinywani mwao hapakuonekana uongo, wala hawakuwa na hatia yoyote.
6 Kisha nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa na Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu wote waishio duniani, kwa mataifa yote, makabila yote, watu wa lugha zote na rangi zote. (aiōnios )
Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, yaani, kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa. (aiōnios )
7 Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na nchi, bahari na chemchemi za maji.”
Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”
8 Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema, “Ameanguka! Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa yote wainywe divai yake—divai kali ya uzinzi wake!”
Malaika wa pili akafuata akisema, “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu, ule uliyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”
9 Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake,
Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu yeyote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake,
10 yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu, ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji. Mtu huyo atateseka ndani ya moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwanakondoo.
yeye pia atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo.
11 Moshi wa moto unaowatesa kupanda juu milele na milele. Watu hao waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake, na kutiwa alama ya jina lake, hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana.” (aiōn )
Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa yeyote anayepokea chapa ya jina lake.” (aiōn )
12 Kutokana na hayo, ni lazima watu wa Mungu, yaani watu wanaotii amri ya Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu.
Hapa ndipo penye wito wa subira na uvumilivu wa watakatifu; wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu katika uaminifu kwa Yesu.
13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika! Heri watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana.” Naye Roho asema, “Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao yatawafuata.”
Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wafu wafao katika Bwana tangu sasa.” “Naam,” asema Roho, “watapumzika kutoka taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”
14 Kisha nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya wingu hilo kulikuwa na kiumbe kama mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu kichwani, na kushika mundu mkononi mwake.
Nikatazama, hapo mbele yangu palikuwa na wingu jeupe, na aliyekuwa ameketi juu ya hilo wingu alikuwa “kama Mwana wa Adamu” mwenye taji ya dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake.
15 Kisha malaika mwingine akatoka Hekaluni, na kwa sauti kubwa akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, “Tafadhali, tumia mundu wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia yameiva.”
Kisha malaika mwingine akaja kutoka hekaluni naye akamwita kwa sauti kubwa yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa wakati wa mavuno umewadia, kwa maana mavuno ya dunia yamekomaa.”
16 Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa.
Hivyo yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akauzungusha mundu wake duniani, nayo dunia ikavunwa.
17 Kisha malaika mwingine akatoka katika Hekalu mbinguni akiwa na mundu wenye makali.
Malaika mwingine akatoka katika hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali.
18 Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali, “Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva!”
Kisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.”
19 Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha ghadhabu ya Mungu.
Hivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu.
20 Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji, na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko mrefu kiasi cha mita mia tatu na kina chake kiasi cha mita mia mbili.
Lile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi, kwa umbali wa maili 200.