< Ufunuo 1 >

1 Hizi ni habari za mambo ambayo yalifunuliwa na Yesu Kristo. Mungu alimpa Kristo ufunuo huu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe Yohane, mtumishi wake, mambo hayo,
Huu ni ufunuo wa Yesu Kristo ambao Mungu alimpa ili kuwaonesha watumishi wake mambo ambayo lazima yatokee karibuni. Aliyafanya yajulikane kwa kumtuma malaika wake kwa mtumishi wake Yohana.
2 naye Yohane, ameyasema yote aliyoyaona. Na hii ndio taarifa yake kuhusu ujumbe wa Mungu na ukweli uliofunuliwa na Yesu Kristo.
Yohana alitoa ushuhuda wa kila kitu alichoona kuhusiana na neno la Mungu na kwa ushuhuda uliotolewa kuhusu Yesu Kristo.
3 Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki; heri yao wale wanaosikiliza maneno ya ujumbe huu wa kinabii na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati umekaribia ambapo mambo haya yatatukia.
Amebarikiwa yeye asomaye kwa sauti na wale wote wanaoyasikia maneno ya unabii huu na kutii kilichoandikwa humo, kwa sababu muda umekaribia.
4 Mimi Yohane nayaandikia makanisa yaliyoko mkoani Asia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi,
Yohana, kwa makanisa saba yaliyoko Asia: neema iwe kwenu na amani kutoka kwake aliyepo, aliyekuwepo, na atakayekuja, na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi,
5 na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia. Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu,
na kutoka kwa Yesu Kristo ambaye ni shahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mtawala wa wafalme wa dunia hii. Kwake yeye atupendaye na ametuweka huru kutoka katika dhambi zetu kwa damu yake,
6 akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina. (aiōn g165)
ametufanya kuwa ufalme, makuhani wa Mungu na Baba yake - kwake kuwa utukufu na nguvu milele daima. Amina. (aiōn g165)
7 Tazama! Anakuja katika mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale waliomchoma. Makabila yote duniani yataomboleza juu yake. Naam! Amina.
Tazama, anakuja na mawingu; kila jicho litamwona, pamoja na wote waliomchoma. Na kabila zote za dunia wataomboleza kwake. Ndiyo, Amina.
8 “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu Mwenye Uwezo, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja.
“Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu, “Yeye aliyepo, na aliyekuwepo, na ambaye anakuja, Mwenye nguvu.”
9 Mimi ni Yohane, ndugu yenu; na kwa kuungana na Kristo nashiriki pamoja nanyi katika kustahimili mateso yanayowapata wale walio wa Utawala wake. Mimi nilikuwa kisiwani Patmo kwa sababu ya kuhubiri ujumbe wa Mungu na ukweli wa Yesu.
Mimi, Yohana - ndugu yenu na mmoja anayeshiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na uvumilivu thabiti ulio katika Yesu; nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patimo kwa sababu ya neno la Mungu na ushuhuda kuhusu Yesu.
10 Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta.
Nilikuwa katika Roho siku ya Bwana. Nilisikia nyuma yangu sauti ya juu kama ya tarumbeta,
11 Nayo ilisema, “Andika katika kitabu yote unayoyaona, ukipeleke kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamoni, Thuatira, Sarde, Filadelfia na Laodikea.”
ikisema, “andika katika kitabu unayo yaona, na uyatume kwa makanisa saba, kwenda Efeso, kwenda Smirna, kwenda Pergamo, kwenda Thiatira, kwenda Sardi, kwenda Philadelphia, na kwenda Laodikia.”
12 Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya taa saba vya dhahabu,
Nikageuka kuona ni sauti ya nani aliyekuwa akiongea nami, na nilipogeuka niliona kinara cha dhahabu cha taa saba.
13 na katikati yake kulikuwa na kitu kama mtu, naye alikuwa amevaa kanzu ndefu na ukanda wa dhahabu kifuani.
Katikati ya kinara cha taa alikuwemo mmoja kama Mwana wa Adamu, amevaa kanzu ndefu iliyofika chini ya miguu yake, na mkanda wa dhababu kuzunguka kifua chake.
14 Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba safi, kama theluji; macho yake yalimetameta kama moto;
Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe kama theluji, na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto.
15 miguu yake iling'aa kama shaba iliyosafishwa katika tanuru ya moto na kusuguliwa, na sauti yake ilikuwa, kama sauti ya poromoko la maji.
Nyayo zake zilikuwa kama shaba iliyosuguliwa sana, kama shaba ambayo imekwisha pitishwa katika moto, na sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi yanayotiririka kwa kasi.
16 Katika mkono wake wa kulia, alikuwa na nyota saba, na kinywani mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling'aa kama jua kali.
Alikuwa ameshikilia nyota saba katika mkono wake wa kuume, na kutoka kinywani mwake kulikuwa na upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa uking'aa kama mwanga mkali wa jua.
17 Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti. Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa mwisho.
Nilipomwona, nikaanguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kulia juu yangu na kusema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa Mwisho,
18 Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa ni mzima milele na milele. Ninazo funguo za kifo na Kuzimu. (aiōn g165, Hadēs g86)
na ambaye ninaishi. Nalikuwa nimekufa, lakini tazama, ninaishi milele! Na ninazo funguo za mauti na kuzimu. (aiōn g165, Hadēs g86)
19 Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa na yale yatakayotukia baadaye.
Kwa hiyo, yaandike uliyoyaona, yaliyopo sasa, na yale yatakayotokea baada ya haya.
20 Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia, na siri ya vile vinara saba vya taa hii: zile nyota saba ni malaika wa makanisa; na vile vinara saba vya taa ni makanisa saba.
Kwa maana iliyojificha kuhusu nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na kile kinara cha dhahabu cha taa saba: nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, na kinara cha taa saba ni yale makanisa saba.”

< Ufunuo 1 >