< Mathayo 21 >
1 Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,
Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili,
2 akawaambia, “Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu.
akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu, nanyi mtamkuta punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee.
3 Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, Bwana anawahitaji, naye atawaachieni mara.”
Kama mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara.”
4 Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie:
Haya yalitukia ili litimie lile lililonenwa na nabii, akisema:
5 “Uambieni mji wa Sioni: Tazama, Mfalme wako anakujia! Ni mpole na amepanda punda, mwana punda, mtoto wa punda.”
“Mwambieni Binti Sayuni, ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako, ni mnyenyekevu, naye amepanda punda, juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’”
6 Hivyo, wale wanafunzi walienda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza.
Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza.
7 Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake.
Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Yesu akaketi juu yake.
8 Umati mkubwa wa watu ukatandaza nguo zao barabarani, na watu wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani.
Umati mkubwa wa watu ukatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kutoka kwenye miti, wakayatandaza barabarani.
9 Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaaza sauti: “Hosana Mwana wa Daudi! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Hosana Mungu juu mbinguni!”
Ule umati wa watu uliomtangulia na ule uliomfuata ukapiga kelele ukisema, “Hosana, Mwana wa Daudi!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Hosana juu mbinguni!”
10 Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawa wanauliza, “Huyu ni nani?”
Yesu alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?”
11 Watu katika ule umati wakasema, “Huyu ni nabii Yesu, kutoka Nazareti katika mkoa wa Galilaya.”
Ule umati wa watu ukajibu, “Huyu ni Yesu, yule nabii kutoka Nazareti katika Galilaya.”
12 Basi, Yesu akaingia Hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya Hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa.
Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa.
13 Akawaambia, “Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala. Lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.”
Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.”
14 Vipofu na vilema walimwendea huko Hekaluni, naye Yesu akawaponya.
Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya.
15 Basi, makuhani wakuu na walimu wa Sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaaza sauti zao Hekaluni wakisema: “Sifa kwa Mwana wa Daudi,” wakakasirika.
Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika.
16 Hivyo wakamwambia, “Je, husikii wanachosema?” Yesu akawajibu, “Naam, nasikia! Je hamjasoma Maandiko haya Matakatifu? Kwa vinywa vya watoto wadogo na wanyonyao unajipatia sifa kamilifu.”
Wakamuuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?” Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma, “‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao umeamuru sifa’?”
17 Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko.
Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.
18 Yesu alipokuwa anarudi mjini asubuhi na mapema, aliona njaa.
Asubuhi na mapema, Yesu alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa.
19 Akauona mtini mmoja kando ya njia, akauendea; lakini aliukuta hauma chochote ila majani matupu. Basi akauambia, “Usizae tena matunda milele!” Papo hapo huo mtini ukanyauka. (aiōn )
Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka. (aiōn )
20 Wanafunzi walipouona walishangaa wakisema, “Kwa nini mtini huu umenyauka ghafla?”
Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?”
21 Yesu akawajibu, “Kweli nawaambieni, kama mkiwa na imani bila kuwa na mashaka, mnaweza si tu kufanya hivyo, bali hata mkiuambia mlima huu: Ng'oka ukajitose baharini, itafanyika hivyo.
Yesu akawajibu, “Amin, nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ngʼoka, ukatupwe baharini,’ litafanyika.
22 Na mkiwa na imani, chochote mtakachoomba katika sala, mtapata.”
Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”
23 Yesu aliingia Hekaluni, akawa anafundisha. Alipokuwa akifundisha, makuhani wakuu na wazee wa watu wakamwuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Nani amekupa mamlaka haya?”
Yesu alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha na kusema, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka hayo?”
24 Yesu akawajibu, “Na mimi nitawaulizeni swali moja; mkinijibu, basi nami nitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.
Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Kama mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya.
25 Je, mamlaka ya Yohane ya kubatiza yalitoka kwa nani? Je, yalitoka mbinguni ama kwa watu?” Lakini wakajadiliana wao kwa wao hivi: “Tukisema, Yalitoka mbinguni, atatuuliza, Basi, mbona hamkumsadiki?
Ubatizo wa Yohana, ulitoka wapi? Je, ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?” Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema ulitoka mbinguni atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’
26 Na tukisema, Yalitoka kwa watu, tunaogopa umati wa watu maana wote wanakubali kwamba Yohane ni nabii.”
Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yohana kuwa ni nabii.”
27 Basi, wakamjibu, “Hatujui!” Naye Yesu akawaambia, “Nami pia sitawaambieni ninafanya mambo haya kwa mamlaka gani.
Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.” Naye akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”
28 “Ninyi mnaonaje; mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwambia yule wa kwanza, Mwanangu, leo nenda ukafanye kazi katika shamba la mizabibu.
“Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’
29 Yule kijana akamwambia, Sitaki! Lakini baadaye akabadili nia, akaenda kufanya kazi.
“Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitakwenda.’ Baadaye akabadili mawazo yake akaenda.
30 Yule baba akamwambia mtoto wake wa pili vivyo hivyo, naye akamjibu, Naam baba! Lakini hakwenda kazini.
“Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine akamwambia vilevile. Yeye akajibu, ‘Nitakwenda, bwana,’ lakini hakwenda.
31 Je, ni nani kati ya hawa wawili aliyetimiza matakwa ya baba yake?” Wakamjibu, “Yule mtoto wa kwanza.” Basi, Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, watoza ushuru na waasherati wataingia katika Ufalme wa Mungu kabla yenu.
“Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?” Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.” Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika Ufalme wa Mungu.
32 Maana Yohane alikuja kwenu akawaonyesha njia njema ya kuishi, nanyi hamkumwamini; lakini watoza ushuru na waasherati walimwamini. Hata baada ya kuona hayo yote ninyi hamkubadili mioyo yenu, na hamkusadiki.”
Kwa maana Yohana alikuja kwenu kuwaonyesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.
33 Yesu akasema, “Sikilizeni mfano mwingine. Mtu mmoja mwenye nyumba alilima shamba la mizabibu; akalizungushia ukuta, akachimba kisima cha kusindikia divai, akajenga humo mnara pia. Kisha akalikodisha kwa wakulima, akasafiri kwenda nchi ya mbali.
“Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo ndani yake na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri kwenda nchi nyingine.
34 Wakati wa mavuno ulipofika, aliwatuma watumishi wake kwa wale wakulima, ili wakachukue sehemu ya mavuno yake.
Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake.
35 Wale wakulima wakawakamata hao watumishi; mmoja wakampiga, mwingine wakamwua na mwingine wakampiga mawe.
“Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe.
36 Huyo mtu akawatuma tena watumishi wengine, wengi kuliko wa safari ya kwanza. Wale wakulima wakawatendea namna ileile.
Kisha akawatuma kwao watumishi wengine, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile.
37 Mwishowe akamtuma mwanawe huku akifikiri: Watamheshimu mwanangu.
Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’
38 Lakini wale wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: Huyu ndiye mrithi; na tumuue ili tuuchukue urithi wake!
“Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’
39 Basi, wakamkamata, wakamtoa nje ya lile shamba la mizabibu, wakamwua.
Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.
40 “Sasa, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyaje hao wakulima?”
“Kwa hiyo, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?”
41 Wao wakamjibu, “Atawaangamiza vibaya hao waovu, na lile shamba atawapa wakulima wengine ambao watampa sehemu ya mavuno wakati wa mavuno.”
Wakamjibu, “Kwa huzuni kuu atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.”
42 Hapo Yesu akawaambia, “Je, hamkusoma jambo hili katika Maandiko Matakatifu? Jiwe walilokataa waashi sasa limekuwa jiwe kuu la msingi. Bwana ndiye aliyefanya jambo hili, nalo ni la ajabu sana kwetu!
Yesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba: “‘Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni. Bwana ndiye alitenda jambo hili, nalo ni la ajabu machoni petu’?
43 “Kwa hiyo nawaambieni, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wa mataifa mengine wenye kutoa matunda yake.”
“Kwa hiyo ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake.
44 “Atakayeanguka juu ya jiwe hilo atavunjika vipandevipande; na likimwangukia mtu yeyote, litamponda.”
Yeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”
45 Makuhani wakuu na Mafarisayo waliposikia hiyo mifano yake walitambua kwamba alikuwa anawasema wao.
Viongozi wa Makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano ya Yesu, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao.
46 Kwa hiyo wakawa wanatafuta njia ya kumtia nguvuni, lakini waliwaogopa watu kwa sababu wao walimtambua yeye kuwa nabii.
Wakatafuta njia ya kumkamata, lakini wakaogopa umati wa watu, kwa kuwa watu walimwona Yesu kuwa ni nabii.