< Mathayo 20 >

1 “Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake.
Kwa maana ufalme wa mbinguni unafanana na mmliki wa shamba, aliyeamka asubuhi na mapema ili kuajiri wafanyakazi katika shamba lake la mizabibu.
2 Akapatana nao kuwalipa dinari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu.
Baada ya kuwa amekubaliana na wafanyakazi dinari moja kwa kutwa, aliwatuma kwenda katika shamba lake la mizabibu.
3 Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi.
Alienda tena baada ya masaa matatu hivi na aliona wafanyakazi wengine wakiwa wamesimama bila kazi katika eneo la soko.
4 Akawaambia, Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.
Akawaambia, 'Ninyi pia, nendeni katika shamba la mizabibu, na chochote kilicho halali nitawapa.' Hivyo wakaenda kufanya kazi.
5 Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo.
Akaenda tena baada ya masaa sita na tena katika saa ya tisa, na alifanya hivyo hivyo.
6 Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?
Mara nyingine tena mnamo saa kumi na moja, alienda na kuwakuta watu wengine wamesimama bila kazi. Aliwaambia, 'kwanini mmesimama hapa bila kazi yoyote kwa siku nzima?
7 Wakamjibu: Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Yeye akawaambia, Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.
Wakamwambia, kwasababu hakuna mtu yeyote aliyetuajiri. Akawaambia, 'Nanyi ninyi pia nendeni katika shamba la mizabibu.'
8 “Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.
Wakati wa jioni ulipofika, mwenye shamba la mizabibu alimwambia msimamizi wake, 'Waite wafanyakazi na uwalipe mishahara, kwa kuanza na wa mwisho hadi wa kwanza.'
9 Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja dinari moja.
Walipokuja wale walioajiriwa saa kumi na moja, kila mmoja wao alipokea dinari.
10 Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja.
Walipokuja wafanyakazi wa kwanza, walifikiri kuwa watapokea zaidi, lakini walipokea pia kila mmoja dinari moja kila mtu.
11 Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnung'unikia yule bwana.
Baada ya kupokea malipo yao, walimlalamikia mmiliki wa shamba.
12 Wakasema, Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?
Wakasema, 'Hawa wafanyakazi wa mwisho wametumia saa moja tu katika kufanya kazi, lakini umewalinganisha na sisi, sisi tumebeba mzigo kwa siku nzima na kuungua na joto.'
13 “Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa denari moja?
Lakini mwenye shamba akajibu na kusema kwa mmoja wao, 'Rafiki, sikutenda jambo baya. Je! hatukukubaliana na mimi kwa dinari moja?
14 Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.
Pokea kile kilicho halali yako na uende zako. Ni furaha yangu kuwapa hawa wafanyakazi walioajiriwa mwisho sawa sawa na wewe.
15 Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?”
Je! Si haki kwangu kufanya kile ninachotaka na mali zangu? Au jicho lako ni ovu kwa sababu mimi ni mwema?
16 Yesu akamaliza kwa kusema, “Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
Hivyo wa mwisho atakuwa kwanza na wa kwanza wa mwisho''
17 Yesu alipokuwa anakwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia,
Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalem, aliwachukuwa wanafunzi wake kumi na mbili pembeni, na njiani akawaambia,
18 “Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe.
''Tazama tunaelekea Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa katika mikono ya wakuu wa makuhani na waandishi. Watamhukumu kifo
19 Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa.”
na watamtoa kwa watu wa mataifa ili kumdhihaki, kumchapa na kumsulibisha. Lakini katika siku ya tatu atafufuka.''
20 Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu.
Kisha mama wa wana wa Zebedayo alikuja kwa Yesu na wana wake. Alipiga magoti mbele yake na kumwomba kitu kutoka kwake.
21 Yesu akamwuliza, “Unataka nini?” Huyo mama akamwambia, “Ahidi kwamba katika Ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto.”
Yesu akamwambia, “Unataka nini?” Akamwambia, ''Amuru kuwa hawa wanangu wawili wakae, mmoja mkono wako wa kulia na mmoja mkono wako wa kushoto katika ufalme wako.''
22 Yesu akajibu, “Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?” Wakamjibu, “Tunaweza.”
Lakini Yesu akajibu na kusema, “Haujui kile unachoomba. Je! Unaweza kukinywea kikombe ambacho nitakinywea?” wakamwambia, “Tunaweza.”
23 Yesu akawaambia, “Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu.”
Akawaambia, “Kikombe changu hakika mtakinywea. Lakini kukaa mkono wangu wa kulia na mkono wangu wa kushoto si jukumu langu kuwapa, lakini ni kwa wale ambao wamekwisha kuandaliwa na Baba yangu.”
24 Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili.
Wanafunzi wengine kumi waliposikia hivyo, wakahuzunishwa sana na wale ndugu wawili.
25 Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, “Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu na wakuu hao huwamiliki watu wao.
Lakini Yesu aliwaita mwenyewe na kuwaambia, “Mnafahamu ya kuwa watawala wa mataifa huwatiisha, na wakuu wao hutekeleza mamlaka juu yao.
26 Lakini kwenu isiwe hivyo, ila yeyote anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote;
Lakini isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote atakayetaka kuwa mkubwa miongoni mwenu lazima awe mtumishi wenu.
27 na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu.
Na atakaye kuwa wa kwanza miongoni mwenu lazima awe mtumishi wenu.
28 Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi.”
Kama vile Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa uhai wake kuwa ukombozi kwa wengi.”
29 Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata.
Wakati wakitoka Yeriko, umati mkubwa ulimfuata.
30 Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaaza sauti: “Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!”
Na waliwaona vipofu wawili wameketi kando ya barabara. Waliposikia kuwa Yesu alikuwa anapita, walipaza sauti na kusema, “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie.”
31 Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaaza sauti: “Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!”
Lakini umati ukawakemea, na kuwaambia nyamazeni. Hata hivyo, wao wakapaza sauti zaidi na kusema, “Bwana, Mwana wa Daudi, utuhurumie.”
32 Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
Kisha Yesu alisimama na aliwaita na kuwauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
33 Wakamjibu, “Mheshimiwa, tunaomba macho yetu yafumbuliwe.”
Wakamwambia, “Bwana kwamba macho yetu yafumbuliwe.”
34 Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.
Basi Yesu, akiwa amevutwa na huruma, akayagusa macho yao, mara hiyo, wakapokea uwezo wa kuona na wakamfuata.

< Mathayo 20 >