< Yuda 1 >
1 Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, nawaandikia ninyi mlioitwa na Mungu na ambao mnaishi katika upendo wa Mungu Baba, na katika ulinzi wa Yesu Kristo.
2 Nawatakieni huruma, amani na upendo kwa wingi.
3 Ndugu wapenzi, wakati nimo katika jitihada ya kuwaandikieni juu ya ule wokovu tunaoshiriki sote, nimeona lazima ya kuwaandikieni na kuwahimizeni mwendelee kupigana kwa ajili ya imani ambayo Mungu amewajalia watu wake mara moja tu kwa wakati wote.
4 Maana watu wasiomcha Mungu wamepata kujiingiza kwa siri miongoni mwetu, watu ambao, kwa faida ya maisha yao mabaya, wanaupotosha ujumbe wa neema ya Mungu wetu na kumkana Yesu Kristo aliye peke yake kiongozi na Bwana wetu. Maandiko Matakatifu yalikwisha bashiri tangu awali hukumu inayowangojea watu hao.
5 Nataka kuwakumbusheni mambo fulani ambayo mmekwisha yajua: kumbukeni jinsi Bwana alivyowaokoa watu wa Israeli na kuwatoa katika nchi ya Misri, lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini.
6 Na, malaika ambao hawakuridhika na cheo chao, wakayaacha makao yao ya asili, Mungu amewafunga gizani kwa minyororo ya milele wahukumiwe Siku ile kuu. (aïdios )
7 Kumbukeni pia Sodoma na Gomora, na miji ya kandokando yake; wenyeji wake walifanya kama wale malaika; walifanya uzinzi na mambo yaliyo kinyume cha maumbile, wakapewa hukumu ya moto wa milele, iwe onyo kwa watu wote. (aiōnios )
8 Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu.
9 Hata Mikaeli, malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi waliobishana juu ya mwili wa Mose, Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi; ila alisema: “Bwana mwenyewe na akukaripie.”
10 Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama vile wanyama wanayoyajua ndiyo yanayowaangamiza.
11 Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Baalamu. Wameasi kama Kora alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa.
12 Kwa makelele yao yasiyo na adabu, watu hao ni kama madoa machafu katika mikutano yenu ya karamu ya Bwana. Hujipendelea wao wenyewe tu, na wako kama mawingu yanayopeperushwa huko na huko na upepo bila ya kuleta mvua. Wao ni kama miti isiyozaa matunda hata wakati wa majira yake, wamekufa kabisa.
13 Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanaonekana dhahiri kama vile mapovu ya mawimbi. Wao ni kama nyota zinazotangatanga, ambao Mungu amewawekea mahali pao milele katika giza kuu. (aiōn )
14 Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hawa: “Sikilizeni! Bwana atakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu
15 kutoa hukumu juu ya binadamu wote, kuwahukumu wote kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.”
16 Watu hawa wananung'unika daima na kuwalaumu watu wengine. Hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kusudi wafaulu katika mipango yao.
17 Lakini ninyi wapenzi wangu, kumbukeni yale mliyoambiwa hapo awali ni mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo.
18 Waliwaambieni: “Siku za mwisho zitakapofika, watatokea watu watakaowadhihaki ninyi, watu wafuatao tamaa zao mbaya.”
19 Hao ndio watu wanaosababisha mafarakano, watu wanaotawaliwa na tamaa zao za kidunia, watu wasio na Roho wa Mungu.
20 Lakini ninyi, wapenzi wangu, endeleeni kujijenga kikamilifu katika imani yenu takatifu. Salini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu,
21 na kubaki katika upendo wa Mungu, mkiwa mnamngojea Bwana wetu Yesu Kristo awapeni uzima wa milele kwa huruma yake. (aiōnios )
22 Muwe na huruma kwa watu walio na mashaka;
23 waokoeni kwa kuwanyakua kutoka motoni; na kwa wengine muwe na huruma pamoja na hofu, lakini chukieni hata mavazi yao ambayo yamechafuliwa na tamaa zao mbaya.
24 Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta ninyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake,
25 kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina. (aiōn )