< Yakobo 1 >
1 Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia ninyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salaam!
Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, kwa makabila kumi na mbili yaliyotawanyika, salaam.
2 Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali,
Hesabuni kuwa ni furaha zaidi, ndugu zangu, mnapopita katika matatizo mbali mbali,
3 kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu.
mkijua kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huwapa uvumilivu.
4 Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
Acheni uvumilivu uikamilishe kazi yake, kwamba muweze kukomaa kikamilifu, bila kupungukiwa katika lolote.
5 Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.
Lakini kama mtu kati yenu anahitaji hekima, aiombe kutoka kwa Mungu, ambaye hutoa kwa ukarimu na pasipo kukemea kwa wote wamwombao, na atawapa hekima.
6 Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo.
Lakini omba kwa imani, bila shaka, kwa kuwa mwenye kutia shaka ni kama mawimbi katika bahari, huchukuliwa na upepo na kutupwa huku na huko.
7 Mtu wa namna hiyo, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote,
Kwa hakika mtu huyu asifikirie kwamba atapokelewa ombi lake kutoka kwa Bwana;
8 asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.
mtu huyu ana nia mbili, si imara katika njia zake zote.
9 Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza,
Ndugu maskini anapaswa kujivuna katika kusimama kwake juu,
10 naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini.
wakati huo huo ndugu tajiri katika unyenyekevu wake, kwa sababu atatoweka kama ua la kondeni katika shamba analopita.
11 Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.
Jua huchomoza na joto la kuunguza kukausha mimea, na maua huanguka na uzuri wake hufa. Vivyo hivyo watu matajiri watachakaa katikati ya kazi zao.
12 Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili atapewa tuzo la uzima ambalo Mungu aliwaahidia wale wanaompenda.
Amebarikiwa mtu yule anayevumilia majaribu, kwa kuwa baada ya kushinda jaribu hilo, atapokea taji ya uzima, ambayo imeahidiwa kwa wale wampendao Mungu.
13 Kama mtu akijaribiwa, asiseme: “Ninajaribiwa na Mungu.” Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote.
Mtu yeyote hapaswi kusema anapojaribiwa, “Jaribu hili linatoka kwa Mungu,” kwa sababu Mungu hajaribiwi na uovu, na Mungu mwenyewe hamjaribu yeyote.
14 Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya.
Kila mtu hujaribiwa na tamaa zake mbaya zinazomshawishi na kumvuta mbali.
15 Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo.
Ndipo baada ya tamaa ya dhambi kubeba mimba, dhambi huzaliwa, na baada ya dhambi kukomaa sawasawa, huishia katika mauti.
16 Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike!
Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike.
17 Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu.
Kila zawadi iliyo nzuri na kila zawadi iliyokamilika hutoka juu, hushuka chini kutoka kwa Baba wa nuru. Kamwe habadiliki kama kivuli kibadilikavyo.
18 Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe namna ya matunda ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.
Mungu alichagua kutupa sisi uzima kwa Neno la kweli, ili kwamba tuweze kuwa kama uzao wa kwanza miongoni mwa viumbe vyake.
19 Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini asiwe mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika.
Mnajua hili, ndugu zangu wapendwa. Kila mmoja anapaswa kuwa mwepesi wa kusikia, siyo mwepesi wa kuongea wala kukasirika,
20 Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki.
kwa kuwa hasira ya mwanadamu haiwezi kutenda haki ya Mungu.
21 Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea ule ujumbe uliopandwa mioyoni mwenu, ambao waweza kuziokoa nafsi zenu.
Kwa hiyo wekeni mbali uchafu wa dhambi na ubaya wote ulio mahali popote, na kwa unyenyekevu lipokeeni neno lililopandwa ndani yenu, ambalo lina uwezo wa kuokoa roho zenu.
22 Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo.
Litiini neno, msilisikie tu, mkijidanganya nafsi zenu wenyewe.
23 Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo.
Kwa kuwa kama yeyote alisikiaye neno bila kulitendea kazi ni sawa na mtu ajiangaliaye uso wake halisi katika kioo.
24 Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo.
Hujitathimini uso wake, na huenda zake na baada ya muda mfupi husahau anavyofanana.
25 Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.
Bali mtu yule anayeiangalia kwa uangalifu sheria kamili, sheria ya uhuru, na kuendelea kuitii, si kwa sababu yeye ni msikilizaji anayesahau, huyu mtu atabarikiwa anapoitenda.
26 Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe.
Ikiwa mtu yeyote atafikiri mwenyewe kuwa ni mtu wa dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, huudanganya moyo wake na dini yake ni bure.
27 Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.
Dini iliyo safi na isiyoharibiwa mbele za Mungu wetu na Baba ni hii: kuwasaidia yatima na wajane katika mateso yao, na kujilinda wenyewe na ufisadi wa dunia.