< Yakobo 1 >
1 Mimi Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, nawaandikia ninyi, makabila kumi na mawili, yaliyotawanyika ulimwenguni! Salaam!
Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo: Kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni: Salamu.
2 Ndugu zangu, muwe na furaha mnapopatwa na majaribu mbalimbali,
Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali,
3 kwani mwajua kwamba imani yenu ikisha stahimili, itawapatieni uvumilivu.
kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.
4 Muwe na hakika kwamba uvumilivu wenu utawategemeza mpaka mwisho, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa chochote.
Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu chochote.
5 Lakini kama mmoja wenu ametindikiwa hekima, basi, anapaswa kumwomba Mungu ambaye atampatia; kwani Mungu huwapa wote kwa wingi na kwa ukarimu.
Kama mtu yeyote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa.
6 Lakini anapaswa kuomba kwa imani bila mashaka yoyote. Mtu aliye na mashaka ni kama mawimbi ya bahari ambayo husukumwa na kutupwatupwa na upepo.
Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku.
7 Mtu wa namna hiyo, mwenye nia mbili na asiye na msimamo katika mwenendo wake wote,
Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu chochote kutoka kwa Bwana.
8 asidhani ya kwamba atapata chochote kile kutoka kwa Bwana.
Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.
9 Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza,
Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa.
10 naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini.
Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani.
11 Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.
Kwa maana jua kali lenye kuchoma huchomoza na kuliunguza, likayakausha majani, na ua lake likapukutika, nao uzuri wake huharibika. Vivyo hivyo tajiri naye atanyauka akiwa anaendelea na shughuli zake.
12 Heri mtu anayebaki mwaminifu katika majaribu, kwani akisha stahimili atapewa tuzo la uzima ambalo Mungu aliwaahidia wale wanaompenda.
Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji la uzima Mungu alilowaahidia wale wampendao.
13 Kama mtu akijaribiwa, asiseme: “Ninajaribiwa na Mungu.” Maana Mungu hawezi kujaribiwa na uovu, wala yeye hamjaribu mtu yeyote.
Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu yeyote.
14 Lakini mtu hujaribiwa anapovutwa na kunaswa na tamaa zake mbaya.
Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya.
15 Tamaa ikiiva huzaa dhambi; nayo dhambi ikikomaa huzaa kifo.
Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti.
16 Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike!
Ndugu zangu wapendwa, msidanganyike.
17 Kila kipaji chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni; hutoka kwa Baba, Muumba wa mianga, ambaye habadiliki wala hana alama yoyote ya ugeugeu.
Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili, hutoka juu, na hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka.
18 Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli, ili tuwe namna ya matunda ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.
Kwa mapenzi yake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mazao ya kwanza katika viumbe vyake vyote.
19 Ndugu zangu wapenzi, kumbukeni jambo hili! Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia lakini asiwe mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika.
Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika.
20 Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki.
Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu.
21 Kwa hiyo, tupilieni mbali mwenendo mchafu na tabia zote mbovu; jiwekeni chini ya Mungu na kupokea ule ujumbe uliopandwa mioyoni mwenu, ambao waweza kuziokoa nafsi zenu.
Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.
22 Msijidanganye wenyewe kwa kusikiliza tu neno lake, bali litekelezeni kwa vitendo.
Basi kuweni watendaji wa Neno wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu.
23 Yeyote anayesikiliza hilo neno lakini halitekelezi, huyo ni kama mtu anayejiangalia sura yake mwenyewe katika kioo.
Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo
24 Hujiangalia mwenyewe, kisha huenda zake, na mara husahau jinsi alivyo.
na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara husahau jinsi alivyo.
25 Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.
Lakini yeye anayeangalia kwa bidii katika sheria kamilifu, ile iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau alichosikia, bali akalitenda, atabarikiwa katika kile anachofanya.
26 Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe.
Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake mtu huyo haifai kitu.
27 Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.
Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.