< Wahebrania 8 >
1 Basi, jambo muhimu katika hayo tunayosema ni hili: sisi tunaye Kuhani Mkuu wa namna hiyo, ambaye anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu mbinguni.
2 Yeye hutoa huduma ya Kuhani Mkuu katika Mahali Patakatifu sana, yaani ndani ya ile hema ya kweli iliyojengwa na Bwana, siyo na binadamu.
3 Kila Kuhani Mkuu ameteuliwa kumtolea Mungu vipawa na dhabihu, na hivyo Kuhani Mkuu wetu lazima pia awe na kitu cha kutolea.
4 Kama yeye angekuwa wa hapa duninani, asingekuwa kamwe kuhani, kwani wako makuhani wengine wanaotoa sadaka kufuatana na Sheria.
5 Huduma zao za kikuhani ni mfano tu na kivuli cha yale yaliyoko mbinguni. Ndivyo pia ilivyokuwa kwa Mose. Wakati alipokuwa karibu kuitengeneza ile hema, Mungu alimwambia: “Tengeneza kila kitu kufuatana na ule mfano ulioonyeshwa kule mlimani.”
6 Lakini sasa Yesu amepewa huduma ya kikuhani iliyo bora zaidi kuliko yao, kama vile agano alilothibitisha kati ya watu na Mungu ni bora zaidi, kwani lina msingi wake katika ahadi za mambo yaliyo bora zaidi.
7 Maana kama lile agano la kwanza halingalikuwa na dosari, hakungalikuwa na haja ya agano la pili.
8 Lakini Mungu aliwalaumu watu wake aliposema: “Siku zinakuja, asema Bwana, ambapo nitafanya agano jipya na watu wa Israeli na kabila la Yuda.
9 Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na babu zao siku ile nilipowaongoza kwa mkono kutoka nchi ya Misri. Hawakuwa waaminifu kwa agano langu; na hivyo mimi sikuwajali, asema Bwana.
10 Na hili ndilo agano nitakalofanya na watu wa Israeli siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu akilini mwao, na kuziandika mioyoni mwao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
11 Hakuna mtu atakayemfundisha mwananchi mwenzake, wala atakayemwambia ndugu yake: Mjue Bwana. Maana watu wote, wadogo na wakubwa, watanijua mimi.
12 Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao.”
13 Kwa kusema juu ya agano jipya, Mungu alilichakaza lile la kwanza; na chochote kinachochakaa na kuwa kikuukuu kitatoweka karibuni.