< Matendo 18 >
1 Baada ya hayo, Paulo aliondoka Athene, akaenda Korintho.
Baada ya haya, Paulo akaondoka Athene akaenda Korintho.
2 Huko Korintho, alimkuta Myahudi mmoja aitwaye Akula, mzaliwa wa Ponto. Akula pamoja na mkewe aitwaye Priskila, walikuwa wamerudi kutoka Italia siku hizohizo kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Roma. Paulo alikwenda kuwaona,
Huko akakutana na Myahudi mmoja jina lake Akila, mwenyeji wa Ponto, ambaye alikuwa amewasili karibuni kutoka Italia pamoja na mkewe Prisila, kwa sababu Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo akaenda kuwaona,
3 na kwa vile wao walikuwa mafundi wa kushona mahema kama alivyokuwa yeye, Paulo alikaa nao akafanya kazi.
naye kwa kuwa alikuwa mtengeneza mahema kama wao, akakaa na kufanya kazi pamoja nao.
4 Kila Sabato alifanya majadiliano katika sunagogi akijaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki.
Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi, akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani.
5 Baada ya Sila na Timotheo kuwasili kutoka Makedonia, Paulo alianza kutumia wakati wake wote kwa ajili ya kuhubiri, akawathibitishia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo.
Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo
6 Walipompinga na kuanza kumtukana, aliyakung'uta mavazi yake mbele yao akisema, “Mkipotea ni shauri lenu wenyewe; mimi sina lawama yoyote juu ya jambo hilo. Na tangu sasa nitawaendea watu na mataifa mengine.”
Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakungʼuta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu wa Mataifa.”
7 Basi, akatoka hapo akaenda kukaa nyumbani kwa mtu mmoja mcha Mungu aitwaye Tito Yusto. Nyumba yake Tito ilikuwa karibu na lile sunagogi.
Kisha akaondoka mle kwenye sinagogi, akaenda nyumbani kwa mtu mmoja jina lake Tito Yusto, aliyekuwa mcha Mungu. Nyumba yake ilikuwa karibu na sinagogi.
8 Lakini Krispo, mkuu wa sunagogi, alimwamini Bwana yeye pamoja na jamaa yake yote. Wakorintho wengi waliusikiliza ujumbe huo, wakaamini na kubatizwa.
Kiongozi wa hilo sinagogi, aliyeitwa Krispo, akamwamini Bwana, yeye pamoja na watu wote wa nyumbani mwake. Nao Wakorintho wengi waliomsikia Paulo pia wakaamini na kubatizwa.
9 Siku moja usiku, Bwana alimwambia Paulo katika maono: “Usiogope, endelea kuhubiri tu bila kufa moyo,
Usiku mmoja Bwana akamwambia Paulo katika maono, “Usiogope, lakini endelea kusema wala usinyamaze,
10 maana mimi niko pamoja nawe. Hakuna mtu atakayejaribu kukudhuru maana hapa mjini pana watu wengi walio upande wangu.”
kwa maana mimi niko pamoja nawe, wala hakuna mtu atakayeweza kukushambulia ili kukudhuru, kwa kuwa ninao watu wengi katika mji huu ambao ni watu wangu.”
11 Basi, Paulo alikaa huko akifundisha neno la Mungu kati yao kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.
Hivyo Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, akiwafundisha neno la Mungu.
12 Lakini wakati Galio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Akaya, Wayahudi walimvamia Paulo kwa pamoja na kumpeleka mahakamani.
Lakini wakati Galio alipokuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala huko Akaya, Wayahudi waliungana kumshambulia Paulo, wakamkamata na kumpeleka mahakamani.
13 Wakasema, “Tunamshtaki mtu huyu kwa sababu ya kuwashawishi watu wamwabudu Mungu kwa namna inayopingana na Sheria.”
Wakamshtaki wakisema, “Mtu huyu anawashawishi watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.”
14 Kabla tu Paulo hajaanza kusema, Galio aliwaambia Wayahudi, “Sikilizeni enyi Wayahudi! Kama kweli jambo hili lingekuwa juu ya uhalifu au uovu ningekuwa tayari kuwasikilizeni.
Paulo alipotaka kujitetea, Galio akawaambia Wayahudi, “Kama ninyi Wayahudi mlikuwa mkilalamika kuhusu makosa makubwa ya uhalifu ingekuwa haki kwangu kuwasikiliza.
15 Lakini kama ni shauri la ubishi kuhusu maneno na majina ya Sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitaki kuwa hakimu wa mambo haya!”
Lakini kwa kuwa linahusu maneno, majina na sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitakuwa mwamuzi wa mambo haya.”
16 Basi, akawafukuza kutoka mahakamani.
Akawafukuza kutoka mahakamani.
17 Nao wote wakamkamata Sosthene ambaye alikuwa kiongozi wa sunagogi, wakampiga palepale mbele ya mahakama. Lakini Galio hakujali kitendo hicho hata kidogo.
Ndipo wote wakamkamata Sosthene kiongozi wa sinagogi, wakampiga mbele ya mahakama, lakini Galio hakujali kitendo chao hata kidogo.
18 Paulo alikaa bado na wale ndugu huko Korintho kwa siku nyingi. Kisha aliwaaga, akapanda meli kwenda Siria pamoja na Priskila na Akula. Huko Kenkrea, alinyoa nywele zake kwa sababu ya nadhiri aliyokuwa ameweka.
Baada ya kukaa Korintho kwa muda, Paulo akaagana na wale ndugu walioamini, akasafiri kwa njia ya bahari kwenda Shamu akiwa amefuatana na Prisila na Akila. Walipofika Kenkrea, Paulo alinyoa nywele zake kwa kuwa alikuwa ameweka nadhiri.
19 Walifika Efeso na hapo Paulo aliwaacha Priskila na Akula, akaenda katika sunagogi, akajadiliana na Wayahudi.
Walipofika Efeso, Paulo aliwaacha Prisila na Akila huko, lakini yeye akaingia kwenye sinagogi akawa anajadiliana na Wayahudi.
20 Walimwomba akae nao muda mrefu zaidi, lakini hakupenda.
Walipomwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi hakukubali.
21 Bali alipokuwa anaondoka, alisema, “Mungu akipenda nitakuja kwenu tena.” Akaondoka Efeso kwa meli.
Lakini alipokuwa akiondoka, akaahidi, “Nitarudi kama Mungu akipenda.” Kisha akasafiri kwa njia ya bahari kutoka Efeso.
22 Meli ilitia nanga Kaisarea, naye Paulo akaenda Yerusalemu kulisalimia lile kanisa, kisha akaenda Antiokia.
Alitia nanga Kaisaria, akaenda Yerusalemu na kulisalimu kanisa, kisha akaenda Antiokia.
23 Alikaa huko muda mfupi, halafu akaendelea na safari kwa kupitia sehemu za Galatia na Frugia akiwatia moyo wafuasi wote.
Baada ya kukaa huko kwa muda, akaondoka na kwenda sehemu moja hadi nyingine huko Galatia na Frigia, akiwaimarisha wanafunzi wote.
24 Myahudi mmoja aitwaye Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, alifika Efeso. Alikuwa mtu mwenye ufasaha wa kuongea na mwenye ujuzi mkubwa wa Maandiko Matakatifu.
Basi akaja Efeso Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mwenyeji wa Iskanderia. Yeye alikuwa na elimu kubwa, pia alikuwa hodari katika Maandiko.
25 Alikuwa amefundishwa juu ya hiyo njia ya Bwana, na akiwa motomoto, aliongea juu ya habari za Yesu. Akafundisha kwa usahihi ingawa alikuwa amepata ubatizo wa Yohane tu.
Alikuwa amefundishwa katika njia ya Bwana, naye alikuwa na bidii katika roho, akafundisha kwa usahihi juu ya Yesu, ingawa alijua tu ubatizo wa Yohana.
26 Priskila na Akula walipomsikia akiongea kwa uhodari ndani ya sunagogi, walimchukua kwao wakamfundisha hiyo Njia ya Mungu kwa usahihi zaidi.
Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi. Lakini Prisila na Akila walipomsikia, walimchukua kando na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi.
27 Apolo alipoamua kwenda Akaya, wale ndugu walimtia moyo kwa kuwaandikia wafuasi kule Akaya wampokee. Alipofika huko, aliweza kwa msaada wa neema ya Mungu, kuwasaidia sana wale ndugu waliopata kuwa waumini;
Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo, wakawaandikia wanafunzi huko ili wamkaribishe. Alipofika huko, aliwasaidia sana wale ambao, kwa neema ya Mungu, walikuwa wameamini.
28 kwa maana aliendelea kwa uhodari kuwashinda Wayahudi hadharani akithibitisha kwa Maandiko Matakatifu kuwa Yesu ni Kristo.
Kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akionyesha kwa njia ya Maandiko kwamba Yesu ndiye Kristo.