< 2 Yohana 1 >

1 Mimi Mzee nakuandikia wewe Bimkubwa mteule, pamoja na watoto wako ninaowapenda kweli. Wala si mimi tu ninayewapenda, bali pia wote wanaoujua ule ukweli wanawapenda ninyi,
Kutoka kwa mzee kwenda kwa mwanamke mteule na watoto wake, ambao niwapendao katika kweli na si mimi tu, bali na wote wale wanao ifahamu kweli,
2 kwa sababu ukweli unakaa nasi milele. (aiōn g165)
kwa sababu ya kweli iliyomo ndani yetu na itakayodumu pamoja nasi milele. (aiōn g165)
3 Neema na huruma na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika ukweli na upendo.
Neema, rehema, amani zitakuwa nasi kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, katika kweli na pendo.
4 Nilifurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako wanaishi katika ukweli kama Baba alivyotuamuru.
Ninafurahi sana kwamba nimegundua baadhi ya watoto wanaenenda katika kweli, kama vile tu tulivyoipokea amri hii kutoka kwa Baba.
5 Basi, Bimkubwa, ninalo ombi moja kwako: tupendane. Ombi hili si amri mpya, bali ni amri ileile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo.
Na sasa nakusihi wewe, mwanamke, siyo kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tokea mwanzo, kwamba tunapaswa kupendana sisi kwa sisi. Na huu ndiyo upendo, tunaopaswa kuenenda, kulingana na amri yake.
6 Upendo maana yake ni kuishi kwa kuzitii amri zake Mungu. Amri niliyoisikia tangu mwanzo ndiyo hii: mnapaswa nyote kuishi katika upendo.
Hii ndiyo ile amri, kama mlivyoisikia tokea mwanzo, kwamba mnapaswa kuenenda katika hiyo.
7 Wadanganyifu wengi wamezuka duniani, watu ambao hawakiri kwamba Yesu Kristo amekuja kwetu akawa binadamu. Mtu asemaye hivyo ni mdanganyifu na ni Adui wa Kristo.
Kwa kuwa wadanganyifu wengi wamesambaa katika ulimwengu, na hawakiri kwamba Yesu Kristo alikuja katika mwili. Huyu ndiye mdanganyifu na mpinga Kristo.
8 Basi, jihadharini ninyi wenyewe ili msije mkapoteza kile mlichokishugulikia, bali mpate tuzo lenu kamili.
Jiangalieni wenyewe kwamba hampotezi mambo yale tuliyokwisha fanyia kazi, lakini ili kwamba mweze kuipokea tuzo kamili.
9 Asiyezingatia na kudumu katika mafundisho ya Kristo, bali anayakiuka, hana Mungu. Lakini anayedumu katika mafundisho hayo anaye Baba na Mwana.
Yeyote aendeleae mbele na hadumu katika fundisho la Kristo, hana Mungu. Yeye adumuye katika fundisho anaye Baba na Mwana pia.
10 Basi, kama mtu akija kwenu bila kuwaleteeni mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu.
Kama mtu anakuja kwenu na haleti fundisho hili, msimkaribishe katika nyumba zenu na msimsalimie.
11 Maana anayemsalimu mtu huyo, anashirikiana naye katika matendo yake maovu.
Kwa kuwa amsalimuye hushiriki katika matendo yake maovu.
12 Ninayo mengi ya kuwaambieni lakini sipendi kufanya hivyo kwa karatasi na wino; badala yake, natumaini kuwatembeleeni na kuzungumza nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ikamilike.
Ninayo mambo mengi ya kukuandikia, na sikutaka kuyaandika kwa karatasi na wino. Lakini natumaini kuja kwenu na kuongea uso kwa uso, kwamba furaha yetu ipate kufanywa kamili.
13 Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu.
Watoto wa dada yenu mteule wanawasalimia.

< 2 Yohana 1 >