< 2 Wakorintho 1 >
1 Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu kila mahali katika Akaya.
2 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
3 Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote.
4 Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.
5 Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye.
6 Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji ninyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi.
7 Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu.
8 Ndugu, tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi.
9 Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe.
10 Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena,
11 ninyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu.
12 Sisi tunajivunia kitu kimoja: dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali neema ya Mungu.
13 Tunawaandikia ninyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa,
14 maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile Siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea ninyi fahari.
15 Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu.
16 Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia, na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea.
17 Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema “Ndiyo” na “Siyo” papo hapo?
18 Mungu ni ukweli mtupu; basi, kile tulichowaambia ninyi si jambo la “Ndiyo” na “Siyo”.
19 Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa “Ndiyo” na “Siyo”; bali yeye daima ni “Ndiyo” ya Mungu.
20 Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa “Ndiyo”. Kwa sababu hiyo, “Amina” yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu.
21 Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na ninyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu;
22 ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.
23 Mungu ndiye shahidi wangu—yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho, kwa sababu tu ya kuwahurumieni.
24 Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; ninyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.