< 2 Wakorintho 9 >
1 Si lazima kuandika zaidi kuhusu huduma hiyo yenu kwa ajili ya watu wa Mungu.
2 Ninajua jinsi mlivyo na moyo wa kusaidia, na nilijivuna juu yenu kuhusu jambo hilo mbele ya watu wa Makedonia. Niliwaambia: “Ndugu zetu wa Akaya wako tayari tangu mwaka jana.” Hivyo, moto wenu umekwisha wahimiza watu wengi zaidi.
3 Basi, nimewatuma ndugu zetu hao, ili fahari yetu juu yenu ionekane kwamba si maneno matupu, na kwamba mko tayari kabisa na msaada wenu kama nilivyosema.
4 Isije ikawa kwamba watu wa Makedonia watakapokuja pamoja nami tukawakuta hamko tayari, hapo sisi tutaaibika—bila kutaja aibu mtakayopata ninyi wenyewe—kwa sababu tutakuwa tumewatumainia kupita kiasi.
5 Kwa hiyo, nimeona ni lazima kuwaomba hawa ndugu watutangulie kuja kwenu, wapate kuweka tayari zawadi yenu kubwa mliyoahidi; nayo ionyeshe kweli kwamba ni zawadi iliyotolewa kwa hiari na si kwa kulazimishwa.
6 Kumbukeni: “Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi.”
7 Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha.
8 Mungu anaweza kuwapeni ninyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema.
9 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini, wema wahudumu milele.” (aiōn )
10 Na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula, atawapa ninyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, ziwe na kuwapa mavuno mengi ya ukarimu wenu.
11 Yeye atawatajirisha ninyi daima kwa kila kitu, ili watu wapate kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi zenu wanazozipokea kwa mikono yetu.
12 Maana huduma hii takatifu mnayoifanya si tu kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu.
13 Kutokana na uthibitisho unaoonyeshwa kwa huduma hii yetu, watu watamtukuza Mungu kwa sababu ya uaminifu wenu kwa Habari Njema ya Kristo mnayoiungama, na pia kwa sababu ya ukarimu mnaowapa wao na watu wote.
14 Kwa hiyo watawaombea ninyi kwa moyo kwa sababu ya neema ya pekee aliyowajalieni Mungu.
15 Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi yake isiyo na kifani!