< 2 Wakorintho 8 >
1 Ndugu, tunapenda kuwapa habari juu ya neema ambazo Mungu ameyajalia makanisa ya Makedonia.
2 Waumini wa huko walijaribiwa sana kwa taabu; lakini furaha yao ilikuwa kubwa hivi hata wakawa wakarimu kupita kiasi, ingawaje walikuwa maskini sana.
3 Naweza kushuhudia kwamba walikuwa wakarimu kadiri ya nguvu zao na hata zaidi. Kwa hiari yao wenyewe,
4 walitusihi sana wapewe nafasi ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watu wa Mungu.
5 Hilo lilikuwa jambo ambalo hatukulitazamia kabisa! Kwanza walijitolea wao wenyewe kwa Bwana, kisha wakajitolea wenyewe kwetu pia, kufuatana na mapenzi ya Mungu.
6 Kwa sababu hiyo, tulimsihi Tito aliyeianza kazi hiyo awasaidieni pia muitekeleze huduma hii ya upendo miongoni mwenu.
7 Ninyi mna kila kitu: imani, uwezo wa kusema, elimu; bidii yote ya kutenda mema, na upendo wenu kwetu. Hivyo, tunatazamia muwe wakarimu katika huduma hii ya upendo.
8 Siwapi ninyi amri, lakini nataka tu kuonyesha jinsi wengine walivyo na bidii ya kusaidia ili nipate kujua jinsi upendo wenu ulivyo wa kweli.
9 Maana, ninyi mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo: yeye, ingawa alikuwa na kila kitu, alijifanya maskini kwa ajili yenu, ili kutokana na umaskini wake, awatajirishe.
10 Kuhusu jambo hili, basi, nawapeni shauri hili: inafaa kwenu kutekeleza sasa yale mliyoanza mwaka jana. Ninyi mlikuwa wa kwanza kuchukua hatua na kuamua kufanya hivyo.
11 Basi, kamilisheni shughuli hiyo; na kama vile mlivyokuwa na hamu kubwa ya kusaidia, basi, fanyeni bidii vivyo hivyo, kadiri ya uwezo wenu, kuikamilisha.
12 Maana ikiwa mtu ana moyo wa kusaidia, Mungu hupokea kila anachoweza kutoa: hadai zaidi.
13 Ninyi hampaswi kuongezewa taabu kusudi wengine wapunguziwe mzigo wao; sivyo, ila ni lazima tujali usawa na haki.
14 Kila mlicho nacho sasa cha ziada kiwasaidie wale wanaohitaji, ili nao wakati watakapokuwa na ziada, wawasaidie ninyi katika mahitaji yenu, na hivyo kuwe na usawa.
15 Kama Maandiko yasemavyo: “Aliyekusanya kwa wingi hakuwa na ziada, na yule aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”
16 Namshukuru Mungu aliyeweka ndani ya moyo wa Tito hamu hiyo niliyo nayo mimi ya kuwasaidia.
17 Si tu kwamba alikubali ombi letu, ila pia alikuwa na hamu kubwa ya kusaidia, hata akaamua kwa hiari yake mwenyewe kuja kwenu.
18 Pamoja naye, tunamtuma ndugu mmoja ambaye sifa zake katika kueneza Habari Njema zimeenea katika makanisa yote.
19 Zaidi ya hayo, yeye amechaguliwa na makanisa awe mwenzetu safarini wakati tunapopeleka huduma hii yetu ya upendo, huduma tunayoifanya kwa ajili ya utukufu wa Bwana na uthibitisho wa nia yetu njema.
20 Tunataka kuepa lawama zinazoweza kutokea kuhusu usimamizi wetu juu ya zawadi hii karimu.
21 Nia yetu ni kufanya vema, si tu mbele ya Bwana, lakini pia mbele ya watu.
22 Basi, pamoja na ndugu hao, tumemtuma ndugu yetu mwingine ambaye mara nyingi tumempa majaribio mbalimbali, tukamwona kuwa ni mwenye hamu kubwa ya kusaidia; hata sasa amekuwa na moyo zaidi kwa sababu ana imani sana nanyi.
23 Tito ni mwenzangu; tunafanya kazi pamoja kwa ajili yenu; lakini kuhusu hawa ndugu zetu wengine, wanaokuja pamoja nao, hao ni wajumbe wa makanisa, na utukufu kwa Kristo.
24 Basi, waonyesheni uthabiti wa upendo wenu, makanisa yapate kuona kweli kwamba fahari ninayoona juu yenu ni ya halali.