< 2 Wakorintho 6 >
1 Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure.
2 Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia.” Basi, sasa ndio wakati wa kufaa, sasa ndiyo siku ya wokovu!
3 Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuio chochote.
4 Badala yake, tunajionyesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu.
5 Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula.
6 Tunajionyesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki,
7 kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu upande wa kulia na upande wa kushoto.
8 Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli;
9 kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote, kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni wazima kabisa.
10 Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini hohehahe, lakini twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu.
11 Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa.
12 Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu ninyi wenyewe, na si kwa upande wetu.
13 Sasa nasema nanyi kama watoto wangu, wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya.
14 Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja?
15 Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Muumini ana uhusiano gani na asiyeamini?
16 Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema: “Nitafanya makao yangu kwao, na kuishi kati yao; Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”
17 Kwa hiyo Bwana asema pia: “Ondokeni kati yao, mkajitenge nao, msiguse kitu najisi, nami nitawapokea.
18 Mimi nitakuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa watoto wangu, waume kwa wake, asema Bwana Mwenye Uwezo.”