< 2 Wakorintho 3 >
1 Je, tunaanza tena kujipendekeza? Je, tunahitaji barua ya utambulisho kwenu, au kutoka kwenu, kama watu wengine?
2 Ninyi wenyewe ni barua yetu; barua iliyoandikwa mioyoni mwetu kila mtu aione na kuisoma.
3 Ni dhahiri kwamba ninyi ni barua ya Kristo aliyoipeleka kwa mikono yetu. Barua yenyewe imeandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu hai; imeandikwa si juu ya kipande cha jiwe, bali juu ya mioyo ya watu.
4 Tunaweza kusema hayo kwa sababu ya tumaini letu tulilo nalo kwa Mungu kwa njia ya Kristo.
5 Si kwamba sisi tunaweza kufanya chochote kwa nguvu zetu wenyewe, ila uwezo wetu wote hutoka kwa Mungu:
6 maana yeye ndiye aliyetuwezesha kulihudumia Agano Jipya ambalo si agano la sheria iliyoandikwa, bali Agano la Roho. Maana sheria iliyoandikwa huleta kifo, lakini Roho huleta uzima.
7 Sheria iliwekwa kwa kuandikwa juu ya vipande vya mawe. Ingawaje mwisho wake umekuwa kifo, utukufu wake ulikuwa mkuu mno hata wana wa Israeli wasiweze kuutazama uso wa Mose kwa sababu ya mng'ao wake. Tena mng'ao huo ulikuwa wa muda tu. Basi, ikiwa huduma ya kile ambacho kimesababisha kifo imefanyika kwa utukufu mwingi kiasi hicho,
8 basi, huduma ya Roho ina utukufu mkuu zaidi.
9 Ikiwa basi, kulikuwa na utukufu katika huduma ile iliyoleta hukumu, ni wazi kwamba huduma ile iletayo kukubaliwa kuwa waadilifu itakuwa na utukufu mkuu zaidi.
10 Sasa utukufu mkuu zaidi umechukua nafasi ya ule utukufu uliokuja hapo awali, ambao fahari yake imekwisha toweka.
11 Maana ikiwa kile kilichokuwa cha muda tu kilikuwa na utukufu wake, bila shaka kile chenye kudumu milele kitakuwa na utukufu mkuu zaidi.
12 Kwa vile hili ndilo tumaini letu, sisi twasema kwa uhodari mkuu.
13 Sisi hatufanyi kama Mose ambaye alilazimika kuufunika uso wake kwa kitambaa ili watu wa Israeli wasiuone ule mwisho wa mng'ao uliokuwa unafifia.
14 Lakini akili zao zilipumbazwa. Mpaka leo hii lisomwapo Agano la Kale, kifuniko hicho bado kipo. Kifuniko hicho kitaondolewa tu mtu anapoungana na Kristo.
15 Naam, mpaka hivi leo kila isomwapo Sheria ya Mose akili zao huwa zimefunikwa.
16 Lakini, wakati mtu amgeukiapo Bwana, kifuniko hicho huondolewa.
17 Hapa “Bwana” ni Roho; na pale alipo Roho wa Bwana ndipo ulipo uhuru.
18 Basi, sisi sote ambao nyuso zetu hazikufunikwa, twaonyesha kama katika kioo, utukufu wa Bwana; tunabadilishwa tufanane zaidi na huo mfano wake kwa utukufu mwingi zaidi. Hiyo ni kazi yake Roho wa Bwana.